Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Tarehe
23 mwezi Agosti mwaka huu Watanzaia nchi nzima wanatarajia kushiriki
katika zoezi la sensa ya watu. Kufanikiwa kwa zoezi hili kunategemea
sana ushiriki wa waandishi na vyombo vya habari kuelimisha na
kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari
wa mbele kuhimiza uhamasishaji na uelimishaji wananchi kuhusu umuhimu
wa sensa kwa maendeleo ya taifa.
“Uelimishaji na uhamasishaji ni
masuala yanayotakiwa kupewa kipaumbele ili kuwasaidia wananchi kutoa
taarifa kwa ajili ya kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi
zitakazoiwezesha kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii”
alisisitiza Mhe. Rais Samia wakati akizindua Nembo na tarehe ya sensa
jijini Dar es Salaam.
Ingawa kumekuwepo na jitihada za
uhamasishaji na uelimishaji wananchi kuhusu zoezi hilo kupitia maudhui
ya vyombo vya habari na jumbe zinazosambazwa kwa njia ya simu, bado
vyombo vya habari havijaweka msisitizo wa kutosha katika zoezi hili
muhimu.
Hii imejidhihirisha katika uhaba wa maudhui
yanayoelimisha na kuhamasisha wananchi masuala ya sensa yanayozalishwa
na vyombo vya habari vyenyewe. Hali hii inanyima wananchi haki ya kupata
taarifa zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kushiriki na kutoa
taarifa zao wakati wa utekelezaji wa zoezi la sensa mwezi ujao.
Vyombo
vya habari vina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kuwaongezea
uelewa wananchi kuhusu umuhimu wa sensa kwa maendeleo.
Ni muhimu,
angalau kwa kipindi kilichosalia zoezi la sensa liwe agenda kuu
inayotawala maudhui ya vyombo vyote vya habari nchini.
Kuibeba
agenda hii kutatoa fursa kwa wananchi wengi sio tu kupata taarifa bali
pia kuwawezesha kutoa maoni, kuuliza maswali na kutaka ufafanuzi wa
masuala mbalimbali kuhusu sensa kupitia vyombo na majukwaa ya kihabari.
Kwa kufanya hivi kutapanua wigo wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali za sensa.
Ikumbukwe
kwamba zoezi la sensa ya watu na makazi nchini Tanzania lilianza
kutekelezwa kwa mara ya kwanza mwaka 1967 na kuendelea mwaka 1978, 1988,
2002, 2012 na hili linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu 2022.
Sensa
inalenga kujua idadi ya watu kwa kuzingatia vigezo kadha wa kadha
ikiwemo umri, jinsia, mahali walipo, kiwango cha elimu, ajira na makazi.
No comments:
Post a Comment