JAJI
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck
Mlacha amewataka Wadau wa Mahakama kubadilika kifikra na kuwa tayari
kwenda sambamba na uboreshaji wa matumizi ya TEHAMA mahakamani.
Akizungumza
hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya siku (3) kuhusu mifumo
ya uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kwa wadau na watumishi wa
Mahakama Mkoa wa Kigoma, Jaji Mlacha alisema kuwa na fikra chanya kuhusu
uboreshaji wa Matumizi ya TEHAMA unaoendelea mahakamani utawezesha
mafanikio ya azma ya Mahakama ya kuwa Mahakama Mtandao (e-Judiciary).
“Mahakama
ilishaanza safari ya kuelekea Mahakama Mtandao na leo hii katika
mafunzo haya tunaiongezea mwendo tu ili tuweze kwenda pamoja,” alisema
Jaji Mlacha.
Aliongeza
kuwa usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao pamoja na usikilizaji wake
bado ni dhana mpya hivyo aliwataka Washiriki wa mafunzo hayo kutumia
vyema ujuzi watakaoupata watakaporudi vituoni ili kuboresha utendaji
kazi wa utoaji wa Haki kwa wakati. Alisema ni Muhimu washiriki kujua
kuwa mageuzi katika dunia ya sasa yamejielekeza katika matumizi ya
TEHAMA na mtandao na kwamba hayaepukiki.
“Mtakuwa
mashahidi wa maendeleo makubwa ya matumizi ya akili bandia (Artificial
intelligence), habari za roboti kufanya kazi kama au zaidi ya binadamu
wa kawaida, Anuani za Makazi na ‘Postcode’ hivyo bila TEHAMA kwa sasa
haiwezekani kushindana” alisisitiza Jaji Mlacha.
Naye
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka alisema
kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa uboreshaji wa huduma za Mahakama
yaliyotafsiriwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano
ulioanza mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 kwa awamu ya kwanza na Mpango
Mkakati awamu ya pili ya mwaka 2020/2021 hadi 2024/2025 ambao pamoja na
mambo mengine umelenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki kwa
wakati.
Mtendaji
huyo alieleza kuwa mafunzo hayo yamepangwa pia ili kuwezesha wadau na
Watumishi kutoka Mahakama Wilaya ya Kasulu kusajili na kuendesha kwa
ufanisi mashauri yenye asili ya Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu kwa njia ya
mtandao.
Mwakilishi
wa Shirika linalohudumia Wakimbizi Kituo cha Kigoma, Bw. Innocent
Sangala aliupongeza Uongozi wa Mahakama kuzindua kituo cha kusikiliza
mashauri kwa njia ya mtandao wilayani Kasulu katika Kambi ya wakimbizi
Nyarugusu na kusema kuwa wataendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha
huduma hizo muhimu kwa wananchi.
“Tutajitahidi
kwa kila linalowezekana kuhakikisha rasilimali chache zinazopatikana
zinachangia maboresho ya Mahakama na wadau katika eneo la TEHAMA ili
lengo la utoaji wa haki kwa wakimbizi na wananchi wengine liweze
kufikiwa kwa wakati na kwa wote” alisema Bw. Sangala
Akitoa
neno la Shukrani kwa niaba ya washiriki waliohudhuria mafunzo hayo,
Inspekta wa Polisi, Bw. Dominic Mlolere ambaye pia ni Mwendesha Mashtaka
wa Wilaya ya Kasulu aliupongeza Uongozi wa Shirika linalohudumia
wakimbizi (UNHCR) na Kituo cha msaada wa kisheria kwa Wanawake, Watoto
na Wakimbizi (WLAC), kwa kushirikiana na Uongozi wa Mahakama Kanda ya
Kigoma kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewaongezea ari na nguvu ya
kufanya kazi hivyo kuendana na kasi ya Mahakama kuelekea Mahakama
mtandao.
Washiriki
wa mafunzo walijengewa uwezo kwa nadharia na vitendo kwa mafunzo
yaliyowezeshwa na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Gadiel Mariki,
Mtendaji wa Mahakama, Bw. Moses Mashaka na Afisa TEHAMA Bw. Prosper
Bonaventura.
Mafunzo
hayo yaliwashirikisha washiriki wapatao 45 kutoka Kituo cha Msaada wa
kisheria kwa Wanawake, Watoto na Wakimbizi, kutoka shirika linalohudumia
wakimbizi (UNHCR), Ofisi ya Waendesha Mashtaka Kigoma na Kasulu, Ofisi
ya Huduma za Uangalizi Kigoma (Probation officers), Jeshi la Magereza,
Jeshi la Polisi, Jeshi la Uhamiaji, Shirika la ‘IRC’ na watumishi wa
Mahakama kutoka Kigoma na Kasulu.
Afisa
TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Prosper Bonaventura
akiwapitisha washiriki wa mafunzo katika mada ya Usikilizaji wa mashauri
kwa njia ya Mtandao.
Washiriki
wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
Kigoma Mhe. Lameck Mlacha (hayupo katika picha) wakati akifungua mafunzo
hayo mapema mnamo tarehe 30 Machi, 2022 katika Ukumbi wa Mahakama
Kuu-Kanda ya Kigoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (aliyeketi
mbele) akizungumza na Mwakilishi kutoka Shirika linalohudumia
Wakimbizi (UNHCR), Bw. Innocent Sangala (wa pili kulia) na Mwakilishi
kutoka Kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake, Watoto na wakimbizi
Wakili Amani Mwamgiga (wa kwanza kulia). Kushoto ni Viongozi wa Mahakama
Kanda ya Kigoma
No comments:
Post a Comment