KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana tarehe 31 Machi,
2022 ilitembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
(IJC) Morogoro ambapo imeonyesha kuridhishwa na Mradi huo na kusema kuwa
unaendana na thamani ya fedha iliyotumika.
Akizungumza
kwa niaba ya Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati,
Mhandisi Isack Kamwele amesema kuwa Mradi wa Ujenzi wa vituo sita vya
Utoaji Haki nchini ikiwemo kituo cha Morogoro ni mradi wenye mafanikio
kwa kuwa inaonyesha wazi kuwa fedha iliyotumika kwa ajili ya ujenzi wake
imetumika kihalali kutokana na ubora wa majengo hayo.
“Tumekagua
Kituo hiki cha Morogoro, na tulianza kukagua Vituo vya Temeke na
Kinondoni Dar es Salaam, napenda kusema wazi kuwa tumeridhishwa na
ujenzi wa majengo haya ambayo yanaonyesha thamani ya fedha iliyotumia na
yana muonekano wa kimataifa,” alisema Mhandisi Kamwele.
Aidha
Mhandisi Kamwele alifafanua kuwa kamati imekuwa jicho la Bunge katika
kuhakikisha pesa inayotolewa na Serikali inaenda kwenye matumizi sahihi
hivyo basi wameridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Mahakama kwani
thamani ya pesa inaonekana, “Nafurahi Value for Money unaiona, wabunge
wote tunafikiri kazi imefanyika vizuri” aliongeza.
Mhandisi
Kamwele alielezea kuwa uwepo wa vituo Jumuishi nchini umesaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani kwani hudumu
zote zinapatikana katika jengo moja na hivyo kurahisisha mchakati wa
upatikanaji wa huduma ya utoaji haki huku ikiondoa gharama na kuokoa
muda.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Prof.Elisante Ole Gabriel
amesema kuwa vituo Jumuishi vya utoaji Haki vimejengwa sita nchini na
matarajio ni kujengwa vituo vipya tisa hadi kumi na mbili nchi nzima
hii ikiwa ni jitihada inayofanywa na serikali kuhakikisha wanaboresha
upatikanaji wa huduma ya haki kwa wananchi.
Akitoa
shukrani zake kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Prof.Ole
Gabriel ameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa vituo hivyo na
kuongeza kuwa lengo la Mahakama ni kuendelea kusogeza huduma ya haki
katika maeneo yasiyokuwa na Mahakama ili huduma ya haki iweze kuwafikia
wananchi popote walipo.
Aliongeza
kuwa kuwepo kwa vituo hivyo kumepokelewa kwa namna chanya na wananchi
kwa kuwa kiu ya huduma kama hii kwa wananchi ilikuwa ni kubwa.
“Sisi
kama Mahakama tunaomba Watanzania wathamini jitihada zinazofanywa na
Serikali sanjari na kutambua juhudi zinazofanywa na Mahakama katika
kuhakikisha huduma ya utoaji haki inapatikana kwa wakati na bila vikwazo
vya aina yoyote ile”alisema Mtendaji Mkuu.
Jengo
la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro lenye sakafu nne limegharimu
Bilioni 9.13 ukiondoa gharama za Mkandalasi likiwa na ukubwa wa
‘Square meters’ 6178 na inaelezwa kuwa jengo hilo limemsogezea Mwananchi
wa Morogoro huduma ambayo awali alilazimika kuifuata Dar es salaam
hususani huduma za Mahakama Kuu.
Kabla
ya ujenzi wa kituo hicho, Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro iliyokuwa
ikitumika ilikuwa ikipokea watu mia moja kwa siku lakini mara baada ya
uwepo wa kituo hiko sasa Mahakama imekuwa ikipokea watu zaidi ya 350
mpaka 400 kwa siku moja hii ni ishara kuwa muitikio wa watu na imani ya
wananchi juu ya Mahakama yao imeongezeka.
Vituo
hivyo vya hadhi ya kimataifa vyenye vifaa vya kisasa vya TEHAMA Vituo
hivyo vimejengwa pia Dar es Salaam (Kinondoni &Temeke) Morogoro,
Arusha, Dodoma na Mwanza.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha
mkono) akiwaonyesha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro
walipofika katika Kituo hicho jana tarehe 31 Machi, 2022 kwa ajili ya
ukaguzi.
Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (waliosimama
kushoto) wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel (kulia) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Kanda ya Morogoro kilichokaguliwa na Kamati
hiyo.
Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali wakiwa katika moja
ya kumbi za Mahakama katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
Kanda ya Morogoro.
Ukaguzi ukiendelea.
Kaimu
Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Isack Kamwele (aliyeshika jembe)
akipanda mti wa kumbukumbu mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki-Morogoro.
Mjumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Mhe. Aida Kenani
akichangia jambo wakati ya ukaguzi wa jengo la 'IJC' Morogoro.
Kulia
ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki katika
mapokezi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.
Picha
ya pamoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) na baadhi ya Watumishi wa Mahakama. Aliyeketi katikati ni
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Isack Kamwelwe na wa pili
kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel.
Picha
ya pamoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel ( wa pili kushoto).
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
No comments:
Post a Comment