Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Menejimenti ya Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma alipokutana na Menejimenti hiyo kwa lengo
la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dodoma. Kulia kwake
ni Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji
Sivangilwa Mwangesi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Ujenzi
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Loishorwa Likimaitare.
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi
akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama kuzungumza na Menejimenti hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji
na kukagua ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma jijini Dodoma.
Muonekano
wa jengo la ofisi za makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi
wa Umma linaloendelea kujengwa jijini Dodoma na Mkandarasi ambaye ni
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)
Na James K. Mwanamyoto-Dodoma
WAZIRI
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Sekretarieti ya Maadili ya
Viongozi wa Umma kushughulikia malalamiko na tuhuma zinazowasilishwa na
wananchi kuhusu Viongozi wa Umma wanaokiuka maadili ili kuwa na viongozi
waadilifu wanaotekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya taifa.
Mhe.
Jenista ameyasema hayo leo alipokutana na Menejimenti ya Sekretarieti
hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kukagua ujenzi wa Ofisi za
makao makuu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini
Dodoma.
Mhe.
Jenista amesema, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu
mwenendo wa baadhi ya Viongozi wa Umma kwenye eneo la uadilifu, hivyo
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ina jukumu kubwa la kuyapokea
malalamiko hayo na kuyafanyia kazi ili viongozi wawe na maadili na miiko
ya uongozi unaotakiwa.
“Mnapokea
tuhuma zinazohusu ukiukwaji wa maadili ya viongozi, hivyo mna jukumu la
kufanya uchunguzi ili kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo na kuzifanyia
kazi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya Mwaka
1995,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha,
Mhe. Jenista ameitaka Sekretarieti hiyo kutoa elimu ya uzingatiaji wa
maadili kwa Viongozi wa Umma ili wasikiuke maadili na miiko ya uongozi
kwa kutokuwa na uelewa.
“Katika
kipindi hiki tujikite zaidi kutoa elimu ya uzingatiaji wa maadili ili
viongozi wetu wa umma waelewe umuhimu wa kuzingatia maadili katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, hii inatokana na baadhi ya
viongozi kukiuka maadili kwa kutokuelewa na hatimaye kujihusisha na
vitendo vya ukiukaji wa maadili.” Mhe. Jenista amehimiza.
Amesema
azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu
Hassan inamtaka kila Mtanzania ajifunze kutii sheria bila shuruti na
kama ni kiongozi basi atii Sheria ya Maadili ya Viongozi bila
kushurutishwa, hivyo suala ya utoaji wa elimu ya uzingatiaji wa maadili
haliepukiki ili kuwa na uongozi unaozingatia utawala bora.
Kwa
upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili wa Viongozi wa Umma,
Mhe. Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi amezitaja kazi za msingi za
Sekretarieti hiyo kuwa ni pamoja na kupokea matamko yanayotakiwa
kutolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Katiba na Sheria, kupokea
malalamiko na tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, kuanzisha na kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za ukiukwaji wa
maadili na kufanya uhakiki wa Matamko na Rasilimali na Madeni
yanayotolewa na Viongozi wa Umma kwa mujibu wa Sheria.
No comments:
Post a Comment