NAIBU
Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewataka wasindikaji wa mkonge
kuhakikisha wanaboresha mitambo yao ili isiathiri ubora wa nyuzi
zinazozalishwa kupitia mkonge ili kumuhakikishia mkulima soko la
uhakika.
Mhe.
Mavunde ameyasema hayo Machi 15, 2022 alipotembelea mashamba ya AMCOS
za Magoma na Magunga zilizopo Wilayani Korogwe,Mkoani Tanga na kupata
nafasi ya kuzungumza na wakulima ili kusikiliza changamoto
zinazowakabili.
“Ni
maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aliyoyatoa kupitia kwa Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa ya kulifanya zao la mkonge kuwa la kimkakati ili kuhakikisha
mkulima wa mkonge anazalisha kwa tija na kunufaika na zao lake, hivyo
Wizara itaendelea kufuatilia kwa ukaribu zao hili na
kuliendeleza,"amesema.
"Tutaipitia
taarifa ya gharama za usindikaji wa mkonge kwa kushirikiana na Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa ili tupate gharama stahiki ya usindikaji,na wakati huo
huo wasindikaji lazima waboreshe mitambo yao ili mkonge mwingi wa
wakulima usipotee na kutoakuathiri ubora wa zao lenyewe baada ya
usindikaji,"amesema.
"Serikali
imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kuhakikisha inanunua mashine
za kusindika mkonge (KORONA) kupitia Bodi ya Mkonge ili kuongeza wigo wa
usindikaji na kupunguza mkonge unaokaukia shambani kwa kushindwa
kuvunwa kwa wakati kutokana na upungufu wa mitambo,”amesema Mavunde.
Naye
mkulima wa mkonge aliyejitambulisha kwa jina la Omary Juma, alimweleza
Mhe. Mavunde kuwa baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja
ukosefu wa maji kwenye korona hali inayopelekea kupata daraja la chini
la mkonge uliochakatwa, kutokuwepo na mkataba baina ya SISALANA
(Msindikaji) na AMCOS, uchakavu wa mitambo ya mwekezaji na uhaba wa
korona hali inayopelekea mkonge kuvunwa mara moja badala ya mara mbili
kwa mwaka.
Naye
Mkurugenzi wa Kampuni ya SISALANA,Bi.Elizabeth Kalambo alieleza kuwa
Kampuni inafahamu changamoto zilizopo na tayari imeanza kuchukua hatua
kadhaa ikiwemo kununua pampu za maji, na kufanya upembuzi yakinifu kwa
ajili ya ujenzi wa visima vipya; maelezo ambayo yalionekana
kutomridhisha Naibu Waziri Mavunde.
Mhe.
Mavunde aliagiza kuwa anahitaji kuona pampu mpya ya maji imefungwa
katika Korona ya Magoma ndani ya siku mbili. Vilevile, alimuomba Mhe.
Basila Mwanukuzi, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kukutana na viongozi wa
AMCOS zote tano za Korogwe pamoja na Kampuni ya Sisalana kwa lengo la
kujadili na hatimaye kutatua changamoto zilizopo baina yao ili wakulima
wanufaike pasipo kuumizwa.
No comments:
Post a Comment