WAHASIBU
wa Serikali wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuondoa
changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.
Baadhi
ya wahasibu waliyohudhuria semina inayohusu usimamizi na Udhibiti wa
Fedha za Umma, huko Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni jijini
Zanzibar.
(PICHA NA MARYAM KIDIKO/MAELEZO)
Hayo
yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa serikali, Dkt.Said Seif wakati akifungua
semina ya usimamizi na udhibiti wa fedha za umma, hafla ambayo
ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Kikwajuni.
Alisema,
kumekuwa na malalamiko mbalimbali yanayojitokeza katika taasisi zao
jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linasababisha kuvuruga mfumo
mzima wa utekelezaji wa majukumu yao na kuishushia hadhi tasnia hiyo.
Mhasibu
huyo alisema fani ya uhasibu hivi sasa imekuwa na changamoto kubwa
ikiwemo kutoaminiwa na badala yake kuonekana watu ambao wanaojali
maslahi yao kwanza.
Hata
hivyo, alisema kutokana na hali hiyo ipo haja hivi sasa kuwapima
watendaji hao kulingana na ripoti ya mkaguzi wa ndani wa hesabu na
endapo wakibaini kuna mapungufu ni vyema kujiandaa kuondoka.
Mhasibu
Mkuu wa Serikali, Dkt.Said Seif Mzee akitoa nasaha na maagizo ya
usimamizi na udhibiti wa fedha za umma katika semina iliyofanyika Ukumbi
wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.
"Nimekua
nikipokea malalamiko mengine kutoka kwa taasisi na idara tofauti
kunitaka kuwaondosha wahasibu katika taasisi zao, hivyo imefika wakati
sasa kwa wahasibu kujitambua na kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili
kujiepusha na hoja zilizokua hazina msingi,"alisema.
Akizungumzia
umuhimu wa kutunza siri za ofisi alisema wapo baadhi ya wahasibu
wamekuwa wakivujisha siri za taasisi zao jambo ambalo limekuwa
likisababisha kukosekana unadhifu na uadilifu.
Mbali na hayo aliwasisitiza watumishi hao kujiongeza kielimu ili kwenda sambamba na wakati uliyopo.
Nae
Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali, Ame Burhan aliwataka wahasibu hao
kufuata miongozo ya sheria, kanuni na taratibu za kazi zao ili kuondosha
changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema
zipo sheria na kanuni tayari zimeshapitishwa katika Baraza la
Wawakilishi, lakini wapo baadhi ya wahasibu hawazijui hivyo ni vyema
kuzifuatilia ili ziwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao.
Nao
washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia
taaluma hiyo kwani itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao.
Semina
hiyo ya siku moja iliyowashirikisha wahasibu wa serikali na jumla ya
mada nne zimewasilishwa ikiwemo udhibiti wa rushwa katika usimamizi wa
fedha za umma, maadili na msingi mkuu wa usimamizi wa fedha za umma,
majukumu ya kusimamia fedha za umma naudhaifu wa usimamizi fedha katika
taasisi za serikali.
No comments:
Post a Comment