MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya
Ushindani nchini (FCC) William Erio,amesema wameanza kuchukua hatua
kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa na vifaa mbalimbali vya ujenzi
kunakofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Tume hiyo pia
imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazofanya kitaifa
na kimataifa kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana ikiwemo
kuvutia wawekezaji ndani ya kipindi cha mwaka mmoja madarakani.
Kauli
hiyo ilitolewa na Erio wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini
Mwanza,kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani ambayo
huadhimishwa Machi 15,kila mwaka pamoja na mafanikio ya serikali ya
awamu ya sita kupitia taasisi hiyo.
Alisema FCC inachunguza
ongezeko la bei kwenye bidhaa na vifaa vya sekta ya ujenzi,kuona kama
kupanda kwake kumesababishwa na gharama za uzalishaji au wafanyabiashara
kutaka kujipatia faida kubwa bila kuzingatia kipato cha mwananchi.
Mkurugenzi
mkuu huyo wa FCC alisema ongezeko la bei kwenye biashara ni kitu cha
kawaida kinachoweza kutokana na sababu za ndani au za nje ya nchi zilizo
nje ya uwezo wetu zinazotokea nchini.
“Katika biashara ongezeko
la bei ni jambo la kawaida,pia ongezeko lisilosababishwa na mahitaji
sasa FCC tunafanya nini katika kudhibiti hilo, tunaangalia bidhaa kwa
nini zimepanda kama kuna dalili za uvunjifu wa sheria kwa
wafanyabiashara kutaka kujipatia faida kubwa,hatua za
zitachukuliwa,”alisema.
Erio alisema siku zote wafanyabiashara
wanalenga faida kubwa iwe kwa njia halali au isiyo halali,na kusistiza
taasisi hiyo inachunguza na kupitia nyaraka mbalimbali zinazohusiana na
bidhaa zinazolalamikiwa kupandishwa bei bila kuzingatia sheria na
kuchukua hatua baada ya uchunguzi huo.
Aidha kuhusu mafanikio ya
serikali ya awamu ya sita, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
Rais Samia aingie madarakani, uwekezaji nchini umeimarika ambapo FCC
imepokea maombi 83 ya uwekezaji katika sekta mbalimbali kulinganisha na
maombi 54 mwaka mmoja kabla hajaingia madarakani.
“Tumpongeza
Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya kitaifa na kimataifa kuhakikisha
maendeleo yanapatikana,katika kuhimiza uwekezaji kukuza uchumi na
ushindani shirikishi lakini pia uamuzi wa kuruhusu chanjo ya Covid-19
umefungua milango kwa wageni kuja kuwekeza na kufanya biashara
nchini,”alisema.
Erio alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita
imeonyesha fursa za kuvutia wawekezaji ambazo FCC inaona zilivyoimarika
ambapo kati ya maombi hayo 83, yamo ya sekta ya madini 18,kilimo 4,benki
10,nishati na petrol 6, afya 3, bima 4,uzalishaji 12,mawasilino na simu
11, utalii 2 na sekta mtambuka 11.
Alieleza kuwa ili kuwalinda
watumiaji wamefanya kaguzi kwenye kanda tano, mikoa 10 na taasisi
151,kuona namna gani mlaji analindwa kutokana na mikataba, isipoangaliwa
inaweza kumwuumiza mlaji,lazima masharti na vigezo vizingatiwe vikiwa
kwenye lugha inayoeleweka kwa wananchi.
Pia mkurugenzi mkuu huyo
wa FCC alitumia fursa hiyo kuwaonya wafanyabishara wa vyakula wasitumie
ibada ya mfungo wa Ramadhani itakayoanza karibuni kuacha kujinufaisha
kwa kuficha bidhaa na kupandisha bei ya vyakula mbalimbali vikiwemo
mafuta ya kula na sukari,hivyo waachwe wafanye ibada hiyo bila vikwazo.
“Tabia
ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa kwa kipindi cha msimu wa
sikukuu hasa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kama atafanya au
watafanya hivyo itakuwa ni kuvunja sheria, FCC itachukua hatua,”alisema
Erio
Akizungumzia kilele cha Siku ya Haki ya Mtuhumiaji
Duniani,yenye kauli mbiu ya Kumlinda Mlaji katika Huduma za Fedha
Kidijitali,alisema kitaifa maadhimisho yatafanyika jijini Mwanza Machi
15,ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji,
Dkt. Ashatu Kijaji.
Alisema kuwa yanalenga kutoa elimu kwa
wananchi wapate ufahamu wa haki zao na kuhakikisha zinakuwepo, pia haki
hizo za huduma za mtumiaji kidijitali ni muhimu katika kukuza uchumi.
Alifafanua
kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia huduma nyingi duniani zinafanyika
kidijitali zikiwemo za kifedha,huduma za luku,kulipa tozo, matumizi
Ankara za maji na kodi za serikali,mikopo na bima, kuuza na kununua
bidhaa.
“Huduma nyingi duniani zinafanyika kidijitali na ipo
hatari ya mtumiaji kukutana na wezi,hivyo ni eneo tunaloliangalia katika
kupata huduma huku mtumiaji akichukua tahadhari,hadi mwaka 2024 watu
bilioni 3.6 duniani watakuwa wanapata huduma za fedha kidijitali sawa na
nusu ya watu bilioni 7.2,hivyo Tanzania si kisiwa tutakuwa katika
matumizi hayo,”alisema. Kwa mujibu wa Erio mwaka 2017 asilimia 70 ya
watu wenye akaunti benki walikuwa wakifanya shughuli zao kidijitali
ambapo asilimia 39 ya kampuni zinatumia teknolojia ya Fintec na kuwataka
wazalishaji wa bidhaa na watoa huduma kuzingatia haki na huduma
zinakuwa zenye ubora.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani nchini (FCC),William Erio, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana kuhusiana na kilele cha maadhimisho ya Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani hapo Machi 15, mwaka huu, jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment