SERIKALI
ya Tanzania inaungana na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) kuadhimisha Siku ya Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika leo
Machi 23, 2022 wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza
na waandishi wa habari Machi 22, 2022 jijini Dodoma Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Utamaduni, Dkt. Emmanuel Temu amesema Siku ya Ukombozi ni
muhimu kuadhimishwa ili kutoa na kuwapa elimu vijana waweze kujua
historia ya nchi zao.
“Waasisi
ya wa Taifa letu chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, nchi yetu ilisimama kidete na tulitumia rasilimali
zetu kwa hali na mali, nguvu za kidiplomasia na za kijeshi kusaidia
mapambano ya vyama vya Ukombozi katika nchi mbalimbali ili kuzisaidia
kupata uhuru na utawala na hatimaye haki kupatikana kikamilifu,”amesema
Dkt. Temu.
Dkt.
Temu amesema kuwa, wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika, Tanzania
ilitoa mchango mkubwa katika kusaidia kwa hali na mali harakati za
ukombozi katika Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Afrika.
Hatua
hiyo, ilizifanya nchi hizo za kusini mwa Afrika kuichangua Machi 23 kwa
kuzingatia siku kama hiyo mwaka 1988 majeshi ya Afrika yalihitimisha
Utawala wa kimabavu na ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini katika Mji wa
Cuito Cuanavale uliopo Kusini mwa Angola na kuulazimisha utawala wa
ubaguzi wa rangi na washirika wao kukubali kuzingatia Azimio la Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSCR) 435/78 ambalo lilipelekea uhuru
wa Namibia.
Katika
kuadhimisha siku hi, wizara imepanga kufanya Kongamano katika Shule ya
Sekondari ya Kongwa mkoani Dodoma, mahali ambapo wapigania uhuru wa
vyama vya Ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika walitumia muda wao
katika kambi kubwa ya Kongwa kupata mafunzo ya Kijeshi ili kuzikomboa
nchi zao mikononi mwa wakoloni.
Aidha,
shughuli nyingine zitakazofanyika siku hiyo ni pamoja na maonesho ya
picha za historia ya Ukombozi na makala, Utoaji wa tuzo na zawadi kwa
wanafunzi walioandika insha bora kuhusu mchango wa Tanzania katika
Ukombozi wa Afrika pamoja na ziara ya kutembelea kumbukumbu zenye urithi
wa Ukombozi zilizopo Kongwa.
Katika
kufanikisha harakati za Ukombozi,lugha adhimu ya Taifa Kiswahili
ilitumika kama lugha ya Ukombozi ambayo hadi sasa imefanikiwa kuwa lugha
ya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na hatimaye sasa
Kiswahili kimetengewa Julai 7 kila mwaka kuwa ni siku ya Kiswahili
Duniani.
Siku
ya Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika iliidhinishwa na Mkutano wa 38
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika Windhoek, nchini
Namibia Agosti 2018 na kupitisha mwezi Machi 23 ya kila mwaka kuwa ni
siku ya kusherehekea ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ambayo ni
njia ya kuenzi na kuhifadhi historia ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika.
No comments:
Post a Comment