SERIKALI
ya Tanzania na Kenya zimekamilisha zoezi la uwekaji vigingi katika
mpaka unaoigawa Tanzania na nchi jirani ya Kenya katika Mbuga ya
Serengeti na hivyo kufanikiwa kumaliza mgogoro wa mpaka uliokuwepo
hususani katika sekta ya utalii kati ya nchi zote mbili.
Miongoni
mwa vigingi vya mpaka wa Tanzania na Kenya vilivyowekwa katika Mbuga ya
Serengeti mkoani Mara ili kumaliza mgogoro wa mpaka uliokuwepo hususani
katika sekta ya utalii kati ya nchi zote mbili.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete
amesema hayo wakati yeye na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na
Utalii walipofika katika Mbuga ya Serengeti kujionea utekelezaji huo
unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa
Kikwete amesema, zoezi la uwekaji vigingi katika mpaka huo wenye zaidi
ya kilomita 60 utaiwezesha Serikali kupata mapato na sifa ambayo mbuga
ya Serengeti iko nayo, akiongeza kuwa vigingi hivyo vimewekwa karibu
zaidi tofauti na awali ambapo vingingi hivyo viliwekwa kwa umbali mkubwa
na kuwa ngumu zaidi kuvitambua.
‘’Katika
kipindi cha mwaka mmoja Serikali ya Rais Samia na ile ya Kenya ziliweza
kuingia katika makubaliano ambayo matokeo yake yamewezesha kutatua
mgogoro uliokuwepo katika mpaka ndani ya mbuga ya Serengeti na kuleta
heshima kubwa kwa nchi zote mbili,"amesema.
Naibu
Waziri huyo alitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio ya Serikali kwa
kipindi cha mwaka mmoja na kubainisha kuwa zoezi kama hilo pia
litaendelea kati ya mipaka ya nchi nyingine jirani ikiwemo Uganda,
Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hasa katika mipaka iliyo
ndani ya maji.
Naye
Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii,
Ally Makoa amewaagiza watendaji wa wizara kuhakikisha wanatekeleza zoezi
hilo na kuharakisha uwekaji vingingi katika mpaka, ili kuondokana na
hadha iliyopo katika utambuzi wa mipaka inayoigawa Tanzania na nchi
jirani.
“Kazi
hii iliyofanyika ni kazi nzuri sana na tunatamani sasa maeneo yetu yote
yaliyohifadhiwa yawe na vigingi vya mipaka vinayoonekana kwa malengo
yaleyale tuliyoyafanya hapa katika maeneo yote ya nje na ndani ya nchi
kuwe na vigingi vivyoonekana ili pasiwe na uvamizi,”Makoa aliongeza.
Wizara
ya Ardhi imesema, itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na yale
ya kibajeti na kutoa kipaumbele katika utatuzi wa migogoro baina ya nchi
jirani kwa kuweka vingingi katika mipaka ambavyo awali viliwekwa na
wakoloni katika umbali mrefu na kusababisha sintofahamu katika baadhi ya
maeneo.
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imehitimisha ziara ya
kikazi kwa kutembelea programu mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada kufuatilia utekelezaji wa
miradi hiyo katika Mkoa wa Singida, Mwanza na Mara.
No comments:
Post a Comment