Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali
Mwinyi ameeleza kwamba Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ataendelea
kukumbukwa kutokana na uongozi wake mahiri.
Dkt.Mwinyi
ameyasema hayo katika salamu za pole alizozituma kwa familia, ndugu
jamaa, marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa kutimia mwaka mmoja tangu kutokea kifo cha Hayati
Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa (CCM)
Taifa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika
salamu zake hizo za pole, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, anaungana na
ndugu, jamaa na marafiki, wananchi pamoja na wanachama na viongozi wa
CCM katika siku hii ya kumbukizi.
Aidha,
Rais Dkt. Mwinyi ameendelea kusisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itaendelea kumuenzi Hayati Magufuli kutokana na mchango wake
mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ndani ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Rais
Dkt. Mwinyi katika salamu hizo pia, aliwasihi wananchi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania waendelee kumuunga mkono na kumuombea dua Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aendelee
kuongoza vyema ili nchi izidi kupata maendeleo endelevu.
Hayati
Rais Dkt.Magufuli aliyezaliwa Oktoba 29, 1959 alifariki dunia Machi
17,2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar-es-Salaam ambako alikuwa
akitibiwa.
No comments:
Post a Comment