MKUU
wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaangukia wananchi wa Kijiji cha
Visezi Kata ya Vigwaza katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuruhusu
mradi wa ujenzi wa barabara ya Vigwaza-Kwala kuendelea wakati Serikali
ikiwa inashughulikia malalamiko yao ya kulipwa fidia.
Barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege kwa barabara mbili kwenda na barabara mbili kurudi.
Wananchi
wa Visezi wamekuwa wakilalamika juu ya kulipwa fidia kwa ajili ya
kupisha mradi huo hali ambayo imepelekea mradi huo kusimama na hivyo
mkandarasi kuwa katika wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza
katika mkutano wake na wananchi wa eneo hilo uliofanyika leo Mkuu huyo
wa mkoa amesema kuwa, ziara yake kijijini hapo imelenga kuleta ustawi
wa wananchi na Serikali yao hasa katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Kunenge
amesema kuwa, mradi wa ujenzi wa barabara ya Vigwaza - Kwala unatumia
fedha nyingi kiasi cha shilingi Bilioni 31 na endapo ukikamilika utakuwa
manufaa makubwa kwa wananchi wa eneo hilo na Taifa kiujumla.
Amesema,barabara
hiyo ni ya kimkakati na ina umuhimu mkubwa kwa kuwa inaelekea katika
Bandari ya Nchi Kavu (Dry Port) inayojengwa Kwala pamoja na mradi
mwingine wa uwekezaji (Industrial Park) ambayo utakuwa mkubwa Afrika.
Kunenge
amesema kukamilika kwa barabara hiyo pamoja na miradi hiyo itakuwa na
manufaa makubwa kwa wananchi hususani wa Vigwaza na Kwala kupata ajira
pamoja na kuongeza mapato ya Taifa kupitia kodi zitakazokuwa
zinakusanywa kupitia miradi hiyo.
Amesema,hakuna
sababu ya wananchi kuzuia ujenzi wa barabara hiyo kwasababu hawajalipwa
fidia kwani kufanya hivyo ni aibu kubwa kwa Taifa na kwamba waache
mradi huo uendelee huku changamoto yao ikifanyiwa kazi.
Aidha,
Kunenge ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anafanyakazi kubwa kwa ajili ya maendeleo
ya wananchi wake na wananchi wa Vigwaza-Visezi- Kwala wamepata bahati
kubwa ya mradi huo hivyo kinachotakiwa ni kuhakikisha wanaruhusu mradi
kutekelezwa kwa faida yao.
"Nimekuja
hapa kuwaambia mambo makubwa mawili,kwanza kuwaeleza umuhimu wa mradi
huu na pili kuwaomba muwe watulivu kwa kuwa Serikali inashughulika na
jambo lenu na sio busara kuzuia mradi wa Bilioni 31 kwa sababu ya
fidia,"amesema Kunenge.
Kunenge
amesema kuwa, Bandari Kavu inajengwa kwa gharama ya Sh.Bilioni 37 huku
ekari 4000 zitatumika kujenga mradi mkubwa wa viwanda Afrika ambapo
mpaka sasa tayari mkandarasi amepatikana na amepewa ekari 2500.
"Serikali
inategemea mradi huu kutoa ajira,kodi na kuendelea kutoa huduma za
jamii kwa wananchi ikiwemo maji,afya ,umeme na huduma nyingine lakini
barabara imesimama kwa ajili ya wananchi kulipwa fidia,hii si
sawa,lakini eneo hili linaenda kuwa Mji mkubwa ambao utasaidia watoto
kuwa na maisha mazuri,"ameongeza Kunenge.
Kunenge
amesema, Serikali inalifanyia kazi suala la fidia wanayolalamikia na
muda si mrefu watapata majibu sahihi ya Serikali endapo wanastahili
fidia au hawastahili lakini kikubwa ni kuhakikisha mradi wa ujenzi wa
barabara hiyo unaendelea.
"Nimekuja
hapa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, mwakilishi wa Rais na sisi tunafanya kazi
ya kuwasaidia wananchi na nyinyi ninaamini niwaelewa,naomba mnipe imani
mimi mkuu wenu kwa kuwa jambo hili linafanyiwa kazi,"amesema Kunenge.
Amesema
kuwa,anajua wengine wamelipwa na wengine hawajalipwa kwa sababu
Serikali ina utaratibu wake kwa hiyo kulipwa au kutokulipwa ni mpaka
taratibu zikamilike lakini kikubwa ni kuwa na subira.
Mkuu
wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallah amesema, amefurahishwa na na
ziara ya Mkuu wa Mkoa katika eneo hilo kwakuwa imani yake ni kupatikana
kwa Suluhu ili mradi huo uendelee.
Zainabu
amesema, baadhi ya wananchi waliopitiwa na mradi huo wamelipwa
isipokuwa wananchi 109 bado hawajalipwa na kupelekea mkandarasi kusimama
kazi ambapo amemuomba Mkuu wa Mkoa kulisimamia jambo hilo ili kusudi
mradi huo upate kuendelea.
Baadhi
ya wakazi wa eneo hilo akiwemo Mohamed Mataya na Juma
Chanzi,wamemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kufanya ziara kijijini hapo
kwa kuwa wanaimani changamoto yao itapata majibu haraka huku wakiomba
majibu yao wayapate mapema ili kusudi wajue namna ya kujipanga.
No comments:
Post a Comment