SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imewaasa wananchi kulinda afya zao za kinywa na meno kwa kufuata njia sahihi za kujikinga.
Hayo
yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi
katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani
yaliyofanyika kitaifa mkoani Ruvuma.
Prof.
Makubi amesema swala la kujikinga na Magonjwa ya Kinywa na Meno ni
muhimu zaidi kuliko kusubiri kuingia kwenye hatua ya matibabu.
"Usafishaji
wa kinywa kwa usahihi, matumizi ya miswaki yenye sifa stahiki, na
udhibiti wa ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kufanya
uchunguzi wa Kinywa na Meno walau mara moja kwa mwaka ni miongoni mwa
mambo ya msingi na ya lazima ili kuwa na Kinywa chenye Afya njema,"
amesema Prof Makubi. Aidha,
amesema matumizi ya sigara na bidhaa za tumbaku pamoja na unywaji wa
pombe uliopitiliza huchangia kupata madhara ya magonjwa ya fizi,
saratani kwenye ulimi, mdomoni na koo.
Hata
hivyo Prof. Makubi amewahimiza wananchi Kujiunga na mfuko wa bima ya
afya ili kuweza kupata huduma kwa gharama nafuu na haraka.
"Wito
wangu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na taifa nzima tuendelee
kujitokeza kwa hiari kujiunga na mfuko wetu wa bima ambao utasaidia
kuboresha huduma zetu na kupata huduma bora,"amesema Prof. Makubi.
Prof.
Makubi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha huduma ya Kinywa na Meno
zinaimarika, kwa kuendelea kununua vifaa tiba vya kisasa na kuboresha
miundombinu ya matibabu hayo katika hospitali na vituo vya afya.
"Takwimu
zinaonyesha jumla ya Wagonjwa 685,224 walihudhuria kwa ajili ya
matibabu ya Kinywa na Meno katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya
kwa mwaka 2021, Wagonjwa 506,950 (74%) walikuwa na tatizo la kutoboka
kwa meno ilihali watu 69,318 walikuwa na Magonjwa ya Fizi,"amesema.
Kwa
upande mwingine Prof. Makubi amemshukuru Rais wa Awamu ya Sita,
Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za afya zina imarika kwa
kuendelea kununua vifaa vya kisasa, kujenga miundombinu na kuboresha
matibabu kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment