Mpango kabambe wa kuhakikisha
uzalishaji wa chakula katika kongani ya kilombero inayoshughulika na
kuendeleza kilimo mkoa wa Morogoro chini ya Kituo cha kuendeleza kilimo
nyanda za kusini mwa Tanzania (SAGCOT) umejadiliwa kuhakikisha
uzalishaji wa mazao unaongezeka ili kuihakikishia nchi usalama wa
chakula.
Akizungumza kwenye kikao cha siku mbili
kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na
SAGCOT na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo uliofanyika jana
mjini Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo Bw.Martine Shigela amekipongeza kituo
cha SAGCOT kwa kazi nzuri wanayofanya na kuitaka kuendelea kufanya
kazi na Ofisi yake kwa karibu ili kuleta tija katika uzalishaji na
kuifanya morogoro kuwa kitovu cha uzalishajI mazao hapa nchini.
"Nipende
kuipongeza SAGCOT kwa namna inavyojitoa kuhakikisha yule mkulima mdogo
ananufaika kwa kufanya kilimo chenye tija kwa kumpatia elimu juu ya
kilimo biashara, sambamba na kumkutanisha na wadau katika mnyororo
mzima wa thamani katika Sekta ya kilimo." Alisema Bw. Shigela
Alisema
Safari hiyo ya kilimo waliyoianza haitoishia hapo itakuwa na
muendelezo wa vikao ambavyo zitakavyoleta mrejesho wa utekelezaji kwa
yaliyopendekezwa na zaidi kuendelea kutatua changamoto mbalimbali
zinazomkabili mkulima mdogo ili kuongeza hali ya uzalishaji mazao
hususani katika kongani ya kilombero.
"Huu ni mwanzo
tunategemea kuwa na vikao vingine ambavyo vitawakutanisha wadau wengi
zaidi, wakiwemo wenyeviti wa vyama wilaya na Mkoa, viongozi wa vyama
vya ushirika, viongozi wa wakulima, wazalishaji, wasindikaji, taasisi za
kifedha na wanunuzi wa mazao.’’Alisema Bw.Shigela
Aliongezea
kuwa Morogoro kijiografia inaardhi nzuri kwa kilimo cha mazao mbalimbali
na pia inaendana na mikoa mbalimbali hivyo kwa kuongeza uzalishaji wa
mazao kutapelekea mkoa kupiga hatua kiuchumi na kimaendeleo kupitia
sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa
SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga amesema kikao hicho cha siku mbili
kimehusisha wadau mbalimbali kutoka Sekta binafsi na Umma ambao
mwisho wa kikao watakuja na mbinu za kuhakikisha uzalishaji wa chakula
unaongezeka nchini.
"Lengo la kikao hiki ni kuona kilimo
kinatoa mchango mkubwa kwa taifa sambamba na kumuinua mkulima mdogo
kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji kwa kufanya kilimo endelevu
ambacho ni rafiki kwa mazingira." Alisema Bw. Kirenga
Alisema
Serikali kwa kishirikiana na wabia wa maendeleo wamefanya kazi kubwa
katika kukuza na kuendeleza Sekta ya kilimo nakuongeza kuwa wakati
umefika kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro kuchangamkia fulsa ya
kuwekeza kwenye kilimo.
"Mkoa wa Morogoro ni mkoa
uliobarikiwa kuwa na eneo lenye ardhi kubwa, njema na nzuri ambayo
inakubali mazao mengi hivyo nitoe rai kwa wakazi wa Morogoro kuanza
kuwekeza kwenye kilimo kwani kitawatoa katika dimbwi la
umaskini."Alisema Bw. Kirenga.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Mbegu za Kilimo(ASA), Dkt. Sophia Kashenge alisema kikao
hiko kimeonyesha malengo mazuri katika kuendeleza kilimo nchini hivyo
wao kama wakala wa mbegu wamejipanga vyema kuhakikisha wanazalisha
mbegu zenye ubora ili kuleta tija katika uzalishaji wa mazao nchini kama
sehemu ya maazimio ya kikao hiko.
"Tumejipanga kikamilifu
kuhakikisha tunazalisha mbegu nyingi zenye ubora ambao zitamletea
matokea chanya mkulima, kwani matokeo mazuri katika uzalishaji yaanzia
katika ubora wa mbegu, "alisema Dkt. kashenge
Kikao hicho cha
siku mbili kimeratibiwa na SAGCOT kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu mkuu
wa Mkoa wa Morogoro na kuwakutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya
kilimo pamoja na taasisi binanfsi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Martine Shigela (katikati) akizungumza kwenye kikao cha kwenye kikao cha siku mbili kilicholenga kujadili changamoto na namna ya kukuza uzalishaji mazao katika kongani ya Kilombero kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkoa huo kwa kushirikiana na Kituo cha kuendeleza kilimo nyanda za juu kusini mwa Tanzania(SAGCOT) na kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya Umma na Sekta Binafsi jana mjini Morogoro. Kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja na wapili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga na kulia ni kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu.
No comments:
Post a Comment