KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Murilo Jumanne na Kamishna wa Jeshi la Zimamoto mkoa wa Zimamoto wa Kinondoni na Ubungo, Christina Sunga wamepongeza jitihada zilizofanywa na kampuni ya SGA Security ambayo iliwahi eneo la kiwanda cha GSM kilichopo Mikocheni Dar ambacho kilikuwa kikiteketea kwa moto.
Moto huo uliokuwa ukiteketeza kiwanda hicho kinachotengeneza magodoro, bati na nyaya ulidaiwa kuanza kuonekana majira ya saa kumi na moja alfajiri.
Katika moto huo Kikosi cha Zimamoto na uokoaji cha SGA kilionekana kupambana na kuingia sehemu ya ndani zaidi iliyokuwa imeshika moto ambako wengine wasiokuwa na vifaa maalum walizuiliwa kuingia.
Jitihada hizo zilileta matunda ambapo mida ya saa nne asubuhi sehemu kubwa iliyokuwa ikiteketea ilidhibitiwa.
Baada ya utulivu huo ndipo Kamishna wa Zimamoto Mkoa wa Kinondoni na Ubungo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo, Christina Sunga alianza kuzungumza na wanahabari akivisifu vikosi binafsi vya zimamoto kikiwemo kikosi cha SGA vilivyoshirikiana kuuzima moto huo.
Kamishna Sunga alisema moto usingedhibitiwa mapema ungeweza kusababisha madhara makubwa mpaka kwenye maeneo jirani na kiwanda hicho.
Mwingine aliyetoa pongezi hizo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Ramadhani Kingai aliyekuwa eneo hilo akiwajibika katika zoezi la uokoaji.
Katika tukio hilo magari ya zimamoto kutoka kampuni ya SGA yalionekana kuingia na kutoka eneo hilo huku askari wake wakionekana kuwa tayari kuzima moto huo na uokoaji wa binadamu.
Hata hivyo Kamanda Murilo alisema katika tukio hilo pamoja na kusababisha hasara kubwa ya mali hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.
Kwa upande wake, Rais wa GSM kwa kupitia msaidizi wake ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha Manunuzi, Chenedzo Mupukuta, aliipongeza SGA kwa kuwahi eneo la tukio huku ikiwa imejiandaa vizuri. “Baada ya moto kuzimwa, timu ya maafa iliamua SGA iendelee kukaa katika eneo la tukio usiku wote ili kupambana na jambo lolote ambalo lingetokea baadaye,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Tanzania, Eric Sambu, alisema ushirikiano katia ya Jeshi la Polisi, Zimamoto na wadau wengine ulisaidia kuepusha madhara zaidi. “Tunafurahi kwa kuwa tulitoa mchango wetu katika kuepusha madhara zaidi kutokana na moto huo,” alisema Sambu.
SGA ndio kampuni kongwe ya binafsi ya ulinzi nchini na imeajiri wafanyakazi zaidi ya 6000 katika matawi yake kote nchini.
No comments:
Post a Comment