OFISI
ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu imebainisha
mipango mikakati ya kiutendaji katika majukumu inayoyaratibu ili
kuhakikisha Maelekezo ya Mhe. Rais na Mhe. Waziri Mkuu yanatekelezwa
kwa ufanisi na weledi katika kuboresha huduma za ofisi hiyo, baada ya
mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan.
Akieleza
mwelekeo wa ofisi hiyo, kwa waandishi wa habari Machi 20,2022 jijini
Dar es Salaam, Mhe. Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu),Patrobas Katambi amefafanua kuwa pamoja na kuwa
ofisi hiyo imetekeleza kwa mafanikio majukumu yake, hatua inayofuata ni
kujikita katika tafiti katika masuala inayoratibu ya Kazi, Ajira,
Vijana na Wenye Ulemavu.
“Tumeanza
kufanya upembuzi katika baadhi ya maeneo, Kwa sasa tatizo la ukosefu
wa ajira duniani ni 13.6 kwa mujibu wa UNESCO, ambapo 75% ya Vijana wapo
katika ajira ya Sekta isiyo rasmi. Kwa Afrika na Asia 96% ya nguvu kazi
ni vijana. Kwa mantiki hiyo tunakusudia kuiwezesha sekta Binafsi kwa
kuwa ndiyo inayo ajiri vijana wengi,"amesema Katambi.
Mhe.
Katambi amefafanua kuwa, Mhe. Rais amewataka waandae programu maalum ya
kutengeneza fursa za Ajira kwa vijana, ambapo programu hiyo itahusisha
wizara, idara, wakala na taasisi zote za serikali, Sekta Binafsi.
"Programu
hiyo itahakikisha kuwa kila fedha inayotokana na serikali kwa hapa
ndani au tunazozipata kutoka nje ya nchi, iweze kuzalisha fursa za ajira
kwa vijana waliojiajiri au kutengeneza ajira,”amesisitiza Katambi
Ameongeza
kuwa, programu hiyo itajikita pia katika katika miradi mikubwa ya
maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ambapo utekezaji wa miradi hiyo
utaweza kuzalisha ajira za moja kwa moja na ambazo sio za moja kwa moja.
“Viongozi
wetu wameshaanza Mipango mikakati ya mashauriano, vikao vya kikanda na
kimataifa katika kufungua na kupanua wigo zaidi wa kutengeneza fursa za
kimtaji na ajira. Aidha, Mkakati mwingine ni kuiwezesha Sekta Binafsi
kwa kuwa ndiyo inayo ajiri zaidi kwa sekta zisizo rasmi. Pia tunaendelea
na kufanya tafiti za mifumo ili kulegeza masharti ya ukopeshaji na riba
za kibenki pamoja na taasisi za kimaendeleo,”amesema Katambi.
Amefafanua
kuwa, mkakati mwingine ambao ofisi hiyo iliyonao ni kuzitafuta taasisi
na wadau wa kimaendeleo watakao weza kutoa ruzuku, misaada pamoja na
fedha zitakazo wawezesha vijana kujiajiri.
Aidha,
ameongeza kuwa wamejipanga kufanya Ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na
halmashauri kwa ajili ya kuwakopesha Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu
ambapo hadi sasa, zaidi ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kote
nchini.
“Serikali
hii imeelekeza, baada ya kuwawezesha vijana kuweza kukopesheka katika
vikundi, lazima 30% ya zabuni zitakazo zinatolewa kwenye Halmashauri
wapewe vijana hao, Pia Mafunzo ya Utambuzi na takwimu hii ikiambatana na
kuwawezesha kupata mikopo na mifuko yetu ya Hifadhi ya jamii imeshaanza
kutekelza hilo,"amesisitiza Katambi.
Aidha,
amefafanua kuwa tayari maelekezo yametolewa ili vijana waliopata
mafunzo ya uanagenzi taribani 14,134, ambapo serikali ilitumia
shilingi bilioni 9 kuwapa mafunzo hayo, hao vijana nao wapewe mikopo
katika halmashauri husika ili waweze kujiajiri.
No comments:
Post a Comment