KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imemtaka Mkuu wa
Wilaya ya Njombe na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe kushirikiana
kwa pamoja katika kuandaa mkakati ambao utaimarisha matumizi ya Stendi
Kuu ya Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuhakikisha shughuli zote za
usafirishaji zinafanyika katika stendi hiyo na sio katika stendi ya
zamani.
Akizungumza
kwa niaba ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa , Mhe.Grace Tendega amesema uwepo wa
matumizi ya stendi ya zamani unahatarisha usalama wa wananchi kutokana
na eneo iliyopo, lakini pia inazorotesha ukusanyaji wa mapato katika
Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Hayo
yamebainishwa Februari 17, 2022 katika ziara ya kamati katika
Halmashauri ya Mji Njombe baada ya kugundua kuwa, shughuli za
usafirishaji bado zinaendelea katika stendi ya zamani badala ya stendi
kuu ya mabasi kama ilivyoagizwa.
Sambamba
na hilo, Mhe. Tendega ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa
ujenzi wa soko la kisasa ambalo linajumuisha biashara mbalimbali,
kutokana na ukubwa wa soko hilo amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo kuhakikisha soko hilo linakatiwa bima, lakini pia uwepo wa vifaa
vya kuzimia moto.
Aidha,
amemtaka kuboresha miundombinu ya vyoo ili kudhibiti maambukizi ya
magonjwa mbalimbali, akisisitiza kutokana na msongamano wa watu wengi
matumizi ya vyoo vya kukaa unahatarisha afya za watumiaji.
Naye
Mhe. Conchesta Rwamulaza ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo amemshauri
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kuhakikisha anasimamia vizuri
ukusanyaji wa mapato ili halmashauri hiyo iweze kujitegemea yenyewe na
kuondokana na utegemezi kutoka Serikali Kuu.
Katika
Halmashauri ya Njombe kamati hiyo imetembelea na kufanya ukaguzi katika
Stendi Kuu ya mabasi na ujenzi wa Soko Kuu, ambapo miundombinu hiyo
imejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na Programu ya
Uimarishaji Mamlaka za Miji (ULGSP) inayofadhiliwa na Serikali kupitia
Benki ya Dunia.
No comments:
Post a Comment