CHELSEA
wanakubali kuwa uwanja wao sasa unatakiwa kufanyiwa mabadiliko,
wanataka kuujenga mwingine wa kisasa ambao utakuwa na uwezo wa kuingiza
watu 60,000 waliokaa vitini.
Uamuzi
huo unafuatia baada ya mafanikio makubwa mfululizo kwa klabu hiyo ya
Jiji la London ambayo inaona kweli haistahili kuwa katika Uwanja wa
Stamford Bridge, maarufu kama darajani.
Championi
limekuwa tena gazeti la kwanza nchini kufika na kufanya ziara katika
uwanja huo na kujifunza mambo mengi yanayohusiana na uwanja huo maarufu.
Uwanja
huo uko katika Jiji la London katika eneo linalojulikana kwa jina la
Fulham, takriban kilomita 20 kutoka ulipo Uwanja wa Emirates
unaomilikiwa na Klabu ya Arsenal.
Jiji
la London ni kati ya miji maarufu zaidi duniani kati ya miji 1,831
ingawa miji maarufu duniani iko 1,935. Katika Umoja wa Ulaya ambao
Uingereza wako katika mchakato wa kujitoa, London inashika nafasi ya
pili kwa kuwa na watu wengi ukiwa na wakati wanaokadiriwa kufikia
milioni 10 baada ya Paris, Ufaransa ambao una watu milioni 13.5.
Moja
ya vitu vinavyoufanya mji huo kuwa maarufu zaidi ni michezo kwa kuwa
kuna klabu nyingi zaidi za soka zinazoshiriki Ligi Kuu England ambayo ni
ligi maarufu zaidi ya soka duniani.
Kuna
Klabu za Arsenal, Chelsea, Tottenham, West Ham, Crystal Palace na
Watford na sasa Chelsea imekuwa ikijipanga kufanya kila inavyoweza
kuipiku Arsenal kwa thamani ya kifedha.
Kwa
sasa, Arsenal ndiyo klabu tajiri na maarufu zaidi katika jiji hilo kwa
kuwa ina thamani ya pauni bilioni 1.118 baada ya pato lake kuongezeka
kwa asilimia 19 kutokana na mapato. Jambo ambalo limewashawishi Chelsea
kuchukua uamuzi wa kuujenga upya uwanja wao wa Stamford Bridge ambao
wanaamini ndani ya miaka mitano ijayo utakuwa umekamilika.
Chelsea
imebeba makombe matano ya Ligi Kuu England tangu mwaka 2004 Arsenal
ilipobeba kombe lake la mwisho. Lakini kwa thamani inaonekana Arsenal
iko mbali, kwani thamani ya Chelsea pamoja na kupanda kwa asilimia 38
kutokana na kubeba mataji mfululizo ni pauni milioni 826.
Hii
inaifanya Chelsea ione suala la kujenga uwanja halina mjadala ingawa
kumekuwa na hofu. Kwani hali inaonyesha Arsenal ilianza kuyumba baada ya
kuanza kujenga uwanja. Kuvihimili vyote kwa pamoja, yaani usajili,
uendeshaji wa klabu na ujenzi si jambo dogo hata kidogo.
Mmiliki
wa Chelsea, Mrusi, Roman Abramovic anaonekana kujipanga kwa hilo ingawa
anajua haitakuwa kazi rahisi. Anajua hawezi kuacha kwa kuwa klabu
nyingine kubwa ya London ya Tottenham imeanza ujenzi wa uwanja wake
wenye uwezo wa kubeba watazamaji 61,000.
Chelsea
haiwezi kuacha kuibadilisha Stamford Bridge na ukweli wanastahili
kufanya hivyo kwa kuwa katika ziara ya Championi kwenye uwanja huo
katika eneo la Fulham, unaonekana umechoka kweli.
Uchovu
wa Stamford Bridge si ule ambao utakufanya usikie kero, lakini kwa kuwa
gazeti hili lilifika katika viwanja vya Old Trafford jijini Manchester
na baadaye Emirates jijini London, Stamford Bridge unaonekana kuwa
umechoka kwa maana ya mfumo ambao unaweza kusema hauendani sana na hadhi
ya Chelsea.
Unapoingia
dimbani, hakuna tofauti kubwa kwa mwonekano na majengo ya viwanja
vingine maarufu, lakini uchakavu wa sehemu kadhaa nyuma ya jukwaa pia
viti. Lakini utaona hata sehemu kadhaa kama vile chumba cha kupumzikia
na kile cha waandishi, kuna tofauti kubwa na viwanja hivyo viwili.
Wataalamu
wa sehemu ya historia ya klabu hiyo, wanasema mara kadhaa walilazimika
kufanya marekebisho kikiwemo chumba cha kubadilishia nguo ili kuufanya
uwanja huo bora kabisa.
Lakini
wanakubali, kuwa kama watataka kuendelea kuifanya Chelsea ni yenye
hadhi ya juu ni lazima wajenge uwanja mpya na tayari wameomba kuhamia
kwenye Dimba la Wembley na wameipata ruhusa hiyo. Tayari kwa sasa uwanja
huo unatumiwa na Tottenham ambao si wapinzani wakubwa sana wa Chelsea
kama ilivyo kwa Arsenal.
Katika
klabu za Ligi Kuu England, tofauti na wengi wanavyodhani, mapato ya
mlangoni ni jambo muhimu sana na klabu nyingi zenye viwanja vikubwa
zimekuwa zikifaidika sana (hili tutalizungumzia siku chache zijazo).
Ndiyo maana klabu nyingi baada ya kupata umaarufu, zimekuwa zikipambana kuongeza ukubwa wa uwanja.
Unapoona
klabu inapambana kuona timu yake inabeba makombe, usidhani mafanikio
hayo ni kwa ajili ya kujionyesha badala yake ni hesabu za kuongeza
umaarufu ambao ni kuongeza mashabiki kwa ajili ya kuongeza fedha
zinazoingia au faida kwa neno zuri.
Ukiachana
na uchakavu wa ndani, Stamford Bridge kwa nje una mvuto zaidi na
unaonyesha ni uwanja wa mfanyabiashara kweli maana kuna takriban hoteli
nne zilizouzunguka uwanja huo pamoja na migahawa kadhaa.
Hivyo
kuwafanya mashabiki wengi kuwa na nafasi ya kuishi katika eneo hilo na
pia ni kati ya viwanja vilivyo rahisi kufikika kwa kuwa uko karibu na
stesheni ya London Broadway pamoja na vituo kadhaa vya mabasi.
Kwa
sasa watu wanaokaa vitini katika Dimba la Stamford Bridge ni 41,631 na
kama kweli watafanikiwa kufikisha watu 60,000 kwenye uwanja wao mpya,
nafasi ya kuipiku Arsenal ipo lakini lazima wahakikishe wanaendelea
kujenga uwanja huku wakifanya kila linalowezekana kushinda zaidi
makombe ya England na Ulaya zaidi ambayo yamewajengea umaarufu mkubwa.
No comments:
Post a Comment