kilole mzee blog
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Serikali
imeahidi kuendelea kushirikiana na kujenga mahusiano mazuri na
Washirika wa Maendeleo ili kuwezesha kufanikisha azma ya kushirikiana
katika kuleta maendeleo nchini.
Hayo
yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa Awamu ya
pili ya Mradi wa kulijengea uwezo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, leo mjini Dodoma.
“Kwa
nia ya kuhakikisha miradi kama hii inayofadhiliwa na Washirika wa
Maendeleo inaleta tija, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na
kujenga mahusiano mazuri kwa lengo la kufanikisha azma katika kuleta
maendeleo,” alisema Majaliwa.
Aidha
Majaliwa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa
karibu utekelezaji wa miradi kama hii ili kuhakikisha masharti na
vigezo mbalimbali vilivyowekwa vinazingatiwa wakati wa utekelezaji wake.
Mbali
na hayo waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa
kushirikiana na Bunge ikiwa ni pamoja na kuendelea kulijengea uwezo
Bunge hilo ili liweze kuisaidia Serikali katika kuleta maendeleo na
kupunguza umaskini.
Kwa
upande wake Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah amesema kuwa Mradi
huo ni matokeo ya mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Bunge la Tanzania na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
“Lengo
la mradi ni kuongeza uwezo kwa wabunge, watumishi na wananchi kwa
ujumla ambapo Mradi umejikita katika masuala ya Utungaji wa Sheria,
Usimamizi wa Bajeti ya Serikali pamoja na ushirikishwaji wa wananchi
katika shughuli za kibunge” ameongeza Dkt. kashilila
Nae
Balozi wa Ireland nchini Tanzania Paul Sherlock amesema Mradi huo
utawezesha Bunge kuimarisha wabunge na watumishi wa bunge kupata elimu
na ujuzi katika maeneo yao ya kazi.
Mradi
huo umefadhiliwa na Washirika wa Maendeleo wakiwemo UNDP, Serikali ya
Ireland, Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Maendeleo la
DFID, Serikali ya Dermark pamoja na Serikali ya Sweden.
No comments:
Post a Comment