RAIS
wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ameshindwa
kujibu swali la kichokonozi lililoulizwa na mwanahabari raia wa Ghana
akitaka kufahamu sababu za shirikisho hilo kuingilia masuala ya kisiasa
lilipoamua kuifungia Urusi kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.
Mwanahabari
huyo, Gary Al-Smith ambaye anafanya kazi na Joy FM ya Ghana aliuliza
swali hilo Alhamisi ya Machi 31,2022 ikiwa ni siku moja kabla ya droo ya
Kombe la Dunia.
Al-Smith
pia alitaka kufahamu, kwa uamuzi huo uliochukuliwa na shirikisho hilo
kwa Urusi, Je? Kuanzia sasa itakuwa sera ya FIFA kwamba nchi yoyote
itakayovamia nyingine itapigwa marufuku kushiriki michuano ya Kimataifa
kama ilivyotokea kwa Urusi.
"Naitwa
Gary Al-Smith, nafanya kazi na Joy FM ya Ghana, Ninakotoka Afrika
tumezoea FIFA kutushukia sana linapokuja suala la kuingiliwa kisiasa
kwenye maamuzi yanayohusu soka.
"Lilikuwa
jambo la kufurahisha sana kwetu barani Afrika na nina hakika kwa watu
wengi Ulimwenguni kuona FIFA ikitoa msimamo wake juu ya Urusi kutangaza
kwamba kinachotokea ni uvunjifu wa haki linapokuja suala la uhusiano wa
kibinadamu, lakini hatuoni jambo la namna hii katika maeneo mengine.
"Tumefikia
hatua ambayo taifa moja linaposhambulia lingine au kuvamia, FIFA
itachukua hatua au hii itakuwa kesi maalum kwa Urusi na
Ukraine?,"alihoji huku zikisikika kelele za shangwe ukumbini.
Katika
jibu lake kwa swali la Al-Smith, Rais wa FIFA Infatino alisema,
shirikisho hilo linafanya kazi kila mahali na wanapaswa kuchukulia hali
hiyo kwa namna sawa.
Mwezi
Februari, mwaka huu Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), lilipiga
marufuku Urusi kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, na mashindano
mengine ya Kimataifa baada ya Rais Vladimir Putin kuivamia Ukraine.
Kutokana
na uamuzi huo, Shirikisho la Soka la Urusi (RFU) katika taarifa yake
lilikaririwa likisema kuwa, hatua hizo ni kinyume na viwango na kanuni
zote za mashindano ya Kimataifa dhidi ya maadili ya ari ya michezo na
haki ya kucheza.
No comments:
Post a Comment