"Mwaka
2021 nikiwa hapo hapo Sober Bomang'ombe (Halmashauri ya Wilaya ya Hai
mkoani Kilimanjaro) baada ya kuona majukumu yameshakuwa mengi mtoto
anakuwa na chumba kimoja hakistahili tena,ikabidi nijaribu kwenda tena
Mwanza katika Halmashauri ya Misungwi kwenda kufuatilia ajira yangu
niliyoajiriwa mwaka 2012 ila baada ya kukutana na Afisa Elimu
alinikutanisha na Afisa Utumishi.
"Nikaongea
nae kwa kina na kumwambia matatizo ambayo niliyapitia alinisikiliza
vizuri sana mpaka mwisho akaniambia...daaah pole sana, Endelea sehemu ya
sita..
Hakuna kazi tena
"Sasa
ipo hivi (Afisa Utumishi anamweleza Twaha Amani), wakati Magufuli
(hayati Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli) anaingia madarakani 2015
alifanya mabadiliko makubwa sana kwenye wafanyakazi hewa, mishahara hewa
pamoja na vyeti feki, kwa hiyo ni bora nianze ku-apply upya,basi baada
ya kuniambia hivyo ikabidi nirudi zangu Moshi, kule Bomang'ombe Sober
kwa kuwa huko ndipo nilikuwa nikifanya kazi na kupata riziki, huku
nikiwa nimepanga chumba kimoja mimi na familia yangu.
Mkufunzi
na Mkurugenzi wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda
(Himo) Sober House mkoani Kilimanjaro,Bw.Twaha Amani akitoa mafunzo kwa
waraibu ambao wapo katika kituo hicho ili waweze kujinasua katika janga
hilo. (DIRAMAKINI).
"Kwa
hiyo nikawa ninaendelea kutafuta kila namna ili kupata riziki ya
kusaidia familia yangu,kwa sababu tayari kulikuwa kuna watu wawili
wananitegemea, mtoto anakuwa, ikanilizamu kutafuta vyumba viwili, pale
pale ikabidi nitafute vyumba viwili kwa shilingi 120,000, ile shilingi
100,000 ambayo nilikuwa ninalipwa pale Sober House ikawa haitoshi. Mambo
yanazidi kuwa magumu.
Maisha magumu
"Watu
wanatakiwa wale, kununua gesi, umeme, kulipia king'amuzi (DSTV) ile
hela ikawa haitoshi chochote, nikamuomba bosi wangu aniongezee, lakini
hataki, anasema nitakuongezea nitakuongezea... hakawa hataki, ikaonekana
amekuwa mbinafsi kupita kiasi.
"Basi
tukaendelea hivyo hivyo, mambo yakazidi kuwa magumu kwangu. Ilipofika
mwaka 2021, kwa sababu tayari nimeshakuwa na uzoefu wa kutosha wa hii
programu wa kufundisha watu, nikapata fedha yangu mahali kama shilingi
milioni 10, ndiyo na mimi nikasema nije kufungua Sober yangu huku Njia
Panda (Himo).
Kufungua Sober
"Baada
ya kupata mhamko wa kuja kufungua Sober yangu huku Njia Panda, kuna
Bwana tulikuwa tunafanya naye naye kazi pale Sober, nikampa taarifa
awali alikuwa ananiambia kuwa Twaha, bwana tuko hapa tunafanya kazi,
lakini hatupati kitu chochote, maisha yanazidi kuwa magumu.Nikamwambia
ninataka kwenda kufungua Sober Njia Panda, je? Upo tayari tukafanye
kazi.
"Kumbe
yule Bwana ninamueleza mambo yangu na yeye ananizunguka, akaenda kwa
bosi wangu akamueleza kila kitu ili nifukuze ili aweze kukaimu nafasi ya
assistant manager (meneja msaidizi) ambayo nilikuwa nayo, sasa nikiwa
nyumbani ilikuwa tarehe 31, mwezi wa 10 siku ya Jumapili, mwaka 2021
ndiyo naenda Sober,ambapo nilikuwa naenda kugawa dawa, ninafika Sober.
"Nilipofika
getini nje nikaona kama kuna hali ya tofauti, wana kikao chao,
walishanijadili tangu jana ili nikifika pale wanifukuze, basi yule bosi
wangu akaanza kunitukana matusi yote ya nguoni na kunifukuza akisema
kumbe unataka kufungua Sober bwana, nikamwambia sasa kufungua Sober
yangu ndiyo unitukane na kunifukuza. Shida ipo wapi hapo?
"Akaniambia
ondoka sikuhitaji hapa, na hata nilikuwa sijapata hata nyumba ya
kupanga wala sijaandaa chochote na wakati nilitaka nikishafanikiwa ndipo
nitoe taarifa kwa bosi wangu.
"Basi
ilibidi niondoke nirudi nyumbani kwa uchungu na mawazo, nilipofika
nyumbani mke wangu akaona sipo sawa kabisa, nikamwambia nimefukuzwa,
akaniambia nilikwambia usiwe unamwambia mtu mambo yako, angalia sasa
hata hujafanya chochote.
Kazi inaanza
"Nikiwa
nyumbani na mawazo ikabidi nianze kwenda Njia Panda kufuatilia mambo
yangu ya nyumba na mambo mengine niliipata nikalipia kila kitu na baadae
nikaenda Arusha kumtafuta mwana sheria kwa ajili ya kunitengenezea
taarifa.
"Hali
hiyo ikanisaidia kufanya mambo yangu vizuri, maana pale Sober nilikuwa
nabanwa ,nilikuwa wa kwanza kufika na wa mwisho kutoka hapo Sober
(Bomang'ombe) lazima niwape watu wote dawa.
"Ndipo
safari ikaanzia hapo ila kuna dada mmoja yuko Wizara ya Maendeleo ya
Jamii ana cheo cheo huko akanipigia simu, akaniambia Twaha unaweza
kuanza kukusanya watu kwa kuwa mchakato wa leseni yako unaendelea
vizuri, haina shida, haikuzuii uko kwenye 'process' nzuri, hizi nyumba
za Sober House zinaruhusiwa kuanza
"Nikaanza
taratibu watu wachache, mara wanane mpaka watu kumi sikukata tamaa.
Mchakato ulianzia hapo, nashukuru Mungu mpaka sasa nina clients 27 na
yule jamaa niliyekuwa naye Tabora alikuja kunipigia simu baada ya kujua
nimefungua kituo kwani alishindwa kuacha unga ilibidi aje ambapo tuko
wote hapa,"amesema Bw.Twaha Amani.
Wito wa Twaha
"Vijana
tuachane na makundi ambayo hayana umuhimu kwetu, tujikite katika mambo
ambayo yanalenga kutuwezesha kuzifikia ndoto zetu, kufanya kazi kwa
bidii, kuachana na vishawishi ambavyo havina tija.
"Mimi
nilianguka, sasa nimesimama tena nikiwa imara, nitasonga mbele kwa
kuhakikisha ninashirikiana na jamii, Serikali ili kuhakikisha vita dhidi
ya dawa za kuelvya tunaishinda, Tanzania bila dawa za kulevya
inawezekana,"anasema Bw.Twaha ambaye kwa sasa ni mkufunzi na Mkurugenzi
wa Surrender for Freedom Teatment Center Njia Panda (Himo) Sober House
mkoani Kilimanjaro, lakini pia shuhuda mzuri wa yale aliyopitia.Wanamzungumziaje
Bw.Nongwe
S. Nongwe ni miongoni mwa watu ambao wanamfahamu kwa karibu, Bw.Twaha
Amani kutoka Pasua mkoani Kilimanjaro anasema kuwa, miaka zaidi ya 15
iliyopita walisoma pamoja katika Kidato cha Tano na Sita Shule ya
Sekondari Singe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara.
"Ili
uwe mwalimu, lazima uwe umepitia ama unakijua unachokifundisha.Wakati
ninamfahamu, tulikuwa kidato cha tano Singe High School, moja ya kitu
ninakikumbuka alikuwa mtanashati sana (smart) muda wote, aliijua dini,
lakini pia alikuwa akivuta bangi.
"Tulikuwa
watano tukijiita GoatFaceFamily (GFF) japo kwenye matumizi ya bangi
hakupata mshirika, japo hatukumtenga kwenye mambo mengine ya kijamii.
"Baada
ya kumaliza, pamoja na mambo mengine aliamua kuwa mlevi sana, lakini
pia akawa mvuta unga mahiri sana (drug user).Kwa umahiri huo,
ulimsababishia kufukuzwa kazi ya upolisi ambao alidumu kwa miaka miwili,
lakini pia ualimu ambao aliutumikia kwa mwaka mmoja tu.
"Mama
yake mzazi ni miongoni mwa waathirika sana na uteja wake (Twaha
Amani),ukiacha fedheha aliyompa, pia alimfilisi kwa kumuibia vitu vya
ndani na pesa.
"Baada
ya kuishi miaka mingi ya uteja, na kupitia magumu aliamua kuingia Sober
House ambapo alikaa zaidi ya mwaka mmoja, na kuamua kubadilika na kuwa
mtu poa, na baadae kuwa moja ya wanafunzi wazuri, na akabakizwa chuo
(Sober House) kama mkufunzi amapo aliweza kuwasaidia wengine wenye hali
aliyopitia.
"Huyo
ndiye Twaha ambaye baadae aliamua kufungua Sober House yake, na kupitia
hiyo amekuwa akisaidia watu tofauti, wenye addiction (vilevi) tofauti
kama madawa ya kulevya (dawa za kulevya), uvutaji wa bangi na ulevi wa
pombe akiwa kama, Mkurugenzi, Mkufunzi wa Surrender for Freedom Teatment
Center Njia Panda (Himo) Sober House lakini pia shuhuda mzuri wa yale
aliyopitia.
"Baada
ya miaka 15, nilimtembelea nyumban kwake, kazini kwake nimeshuhudia
jinsi Mungu alivyombadilisha Twaha Amani ambaye kwa sasa anaishi na
familia yake (mke na mtoto) pia ni mcha Mungu sana. 'God bless you Twaha
(Mungu akubariki Twaha), lipo la kujifunza,"anasema Bw.Nongwe.
Mama afunguka
Katika
mahojiano maalumu na DIRAMAKINI BLOG, mama mazazi wa Bw. Twaha Amani,
Bi.Hadija Shayo anasema kuwa, anamshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kumvusha
katika kipindi cha miaka zaidi ya 10 chenye mapito magumu ya kupanda na
kushuka milima na mabonde isiyokuwa na nuru kwa mtu ambaye ang’ekata
tamaa katika maisha yake.
“Ni
kipindi ambacho ilifika mahali nikakata tamaa, lakini nikafikia hatua
nikajiuliza nikakata tamaa kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa mimi,
niliamua kujipa moyo nikaamua kujitolea kwa hali na mali ili kumuokoa
mwanangu katika tabu alizokuwa anapitia.
“Nilitumia
rasilimali fedha,hekima, maarifa na akili nyingi kuhakikisha ninafanya
kila linalowezekana ili kumuondoa mwanangu Twaha katika uraibu wa dawa
za kulevya,wakati mwingine nilihisi nimefanikiwa kumnasua huko, lakini
kumbe ninapojipa moyo nimemnasua huko, naye ananizunguka anaendelea
kuyavuta,yaliharibu kabisa mipango ya maisha yake,”amesema Bi.Hadija
Shayo ambaye pia aliwahi kuwa mtumishi wa umma katika Manispaa ya Moshi
mkoani Kilimanjaro kabla ya kustaafu hivi karibuni.
Bi.Hadija
anasema kuwa, Bw.Twaha uvutaji wa unga (heroine) ulianza kuchachamaa
tangu alipoanza ajira ya uaskari wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora mwaka
2008, ingawa kumbe hakuwa na taarifa kama tabia za uvutaji dawa za
kulevya zilianza miaka ya nyuma akiwa shuleni.
Anasema,
kama angefahamu kuwa, mwanaye alikuwa anjihusisha na dawa za kulevya
mapema angetumia kila mbinu kuhakikisha anakaa naye ili kujifunza na
kufahamu vishawisi ambavyo vilikuwa vinamhamasisha aweze kuyatumia,
lengo likiwa ni kumtenganisha navyo ili aweze kuziendea ndoto zake.
“Ilikuwa
ni ndoto yangu, mwanangu aweze kuwa na kazi nzuri, itakayomuwezesha
kuendesha maisha yake, Twaha ni mtoto wangu, mwenye moyo wa huruma na
upendo, mchapa kazi na bidi. Lakini kutokana na ile hali iliyomkuta
alijikuta ghafla amefifisha malengo yake, nililia, nilikata tamaa,
nilisemwa na kunyooshewa kidole.
"Kwa
sababu familia yangu ni ya watu maarufu sana hapa mjini Moshi, lakini
machozi yangu niliyaelekeza kwa Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema,
nilimkabidhi Twaha mbele zake, nilitoa sadaka maalumu kwa ajili ya
maombezi kwake ili tu, aweze kurejea katika hali yake ya kawaida,na
baada ya miaka zaidi ya 10 Mwenyenzi Mungu alisikia kilio changu, akatoa
jawabu.
“Ninamshukuru
sana Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema kwa namna ambavyo aliweza
kunipigania na kunipa ujasiri katika kipindi chote cha mapito magumu,si
kwa uwezo wangu wala kwa nguvu zangu, bali kwa msaada wa Mungu,”amesema
Bi.Hadija Shayo ambaye alikuwa anazungumza huku akionekana kutokwa na
machozi.
Alipoteza vitu
Bi.Hadija
anasema, wakati wa kuhakikisha kijana wake, Bw. Twaha anarejea katika
hali yake ya kawaida alitumia rasilimali fedha nyingi ikiwemo kulipia
gharama kwa ajili ya Sober House,kumtoa katika vituo vya polisi na
mahakamani ili aweze kurejea nyumbani.
“Wakati
mwingine, mwanangu aliponea kuuawa kutokana na wizi wa mali za watu ili
aweze kupata fedha kwa ajili ya kununulia hayo madude machafu
(unga-heroine),Fedha ambazo nilikuwa ninatumia ilikuwa ni sehemu ya
mshahara wangu, nilijikuta ninashindwa kutimiza malengo mengine kwa
ajili ya maendeleo katika familia ili kuhakikisha ninamsaidia,”anasema
Bi.Hadija.
Anasema,
jambo ambalo lilkuwa linamsononesha ni pamoja na wakati mwingine,
Bw.Twaha alifikia hatua ya kumuibia hadi kanga zake, nguo na mashuka kwa
ajili ya kwenda kuziuza ili akanunulie unga.
“Sasa
unajikuta katika wakati mgumu sana katika maisha, maana fedha unazopata
unazitumia kwa ajili ya kumuwezesha aweze kundoka huko alipo, lakini
wakati huo huo kile kinachopatikana na chenyewe kinachukuliwa, ilifika
hatua hata akitandikiwa shuka, unakuta ameshalichukua na kuondoka nalo,
ilikuwa tabu sana, ila ninamshukuru Mwenyenzi Mungu,”amesema.
Waenda mbali zaidi
Kutokana
na matendo ambayo yalikuwa yanafanywa na Bw.Twaha, mama yake amesema
kuna wakati ulifika wakaamua kwenda mbali zaidi wakiamini labda chanzo
kinatokana na mizimu ya kifamilia.
“Tuliamua
kwenda kwa upande wa familia ya baba yake ili kuangalia kama matendo
ambayo alikuwa anayatenda yanatokana na mizimu ya upande huo, baada ya
wazee kuangalia wakaona hamna kitu, tukarejea kwa upande wa familia
yangu, wazee wakaangalia wakaona hamna kitu. Kikubwa ambacho nilibaini
kilimfanya Twaha kujikuta katika uraibu hatari namna hiyo ilikuwa ni
ushawishi na makundi ambayo alikuwa anakutana nayo,”amesema.
Wito
Bi.Hadija
ameiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya (DCEA) kuongeza nguvu kubwa ya kudhibiti biashara ya dawa hizo
kuanzia mijini hadi vijijini na kuhakikisha wanayazuia kuanzia nchi
kavu, angani na baharini ili yasiweze kupenya kuingia nchini Tanzania.
“Kwa
sababu, dawa za kulevya ni kati ya matishio makubwa ya usalama wa rai
na mali zao, uvutaji huo unashawishi mambo mengi ikiwemo wizi, uharibifu
wa mali na kudhoofisha utendaji kazi, hivyo kuwafanya vijana kudhoofika
kiafya na kushindwa kufanya kazi za kuwaingizia kipato na hata
kulitumikia Taifa,”anasema Bi.Hadija.
Anasema,
wazazi ambao wana watoto waliopitia au wanapitia mapito kama yake,
hawapaswi kukata tamaa bali wajitolee kuwaombea kwa Mungu na kusaidia
kwa hali na mali ili kuwaondoa katika uraibu.
Pia
amesema, elimu dhidi ya masuala yahusuyo dawa za kulevya inapaswa kuwa
ndani ya mitaala au somo la lazima kuanzia elimu ya awali hadi chuo
kikuu ili vijana na watoto waweze kujifunza kuhusu athari za kujiingiza
katika biashara, utumiaji au kwa namna nyingine yoyote kwa lengo la
kukiandaa kizazi kinachotoa kisogo kwa dawa za kulevya na kujikita
katika mambo ya msingi kwa ajili ya maisha yao, jamii na Taifa kwa
ujumla kabla na baada ya masomo.
“Tukifanikiwa
kuhusu somo linalohusu dawa za kulevya kuwa la lazima katika shule za
msingi hadi vyuo vikuu, tutakuwa tumeokoa vijana wengi ambao wanapotea
kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa sasa,”anasema
Bi.Hadija.
Ombi
Pia
ameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuona namna ambavyo inawatumia
vijana kama Twaha ili kuwa mabalozi wema wa kutoa elimu kwa jamii na
vijana kuhusu athari za dawa za kulevya nchini.
WANASEMAJE?
Kwa
nyakati tofauti baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya ambao wapo
chini ya uangalizi wa nyumba ya upataji nafuu (sober house) ya Free at
Last iliyopo mjini Morogoro wamesema, unyanyapaa ni moja wapo ya sababu
kubwa inayowafanya waumie nafsi zao.
Mmoja
wa waraibu, Abel Leonard ambaye anaendelea na uangalizi kutoka mkoani
Mbeya anasema kuwa, hawafurahi kuwa katika hali hiyo, kwani hata yeye
alijikuta ameangukia katika janga hilo baada ya kupoteza wazazi wote na
kukosa marafiki wema wa kumuongoza.
Amesema,
anajutia kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, kwani
yamemvurugia mfumo wa maisha yake na anaamini akipona ataenda kuwa
balozi mwema huko mtaani, kwa kuwa matumizi ya dawa hizo hayana faida
badala yake amepoteza muda na kila kitu.
Ameyasema
hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliokuwa katika kikao kazi
cha siku tatu kuanzia Novemba 10 hadi 12, 2021 cha Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) mjini Morogoro.
Ziara
hiyo ya Novemba 11, 2021 ilikuwa sehemu ya mafunzo ambapo msimamizi wa
nyumba ya Free At Last, Michael Cassian amesema, jamii ikifanikiwa
kuushinda unyanyasaji na unyanyapaa kwa waathirika wa dawa za kulevya
huo utakuwa ni uponyaji tosha kwao.
Pia
amesema, ukosefu wa elimu sahihi kwa jamii kuhusu watu waliothiriwa na
dawa za kulevya umesababisha kukithiri kwa matukio ya udhalilishaji kwa
waathiriwa hao ikiwemo kuigizwa na kuitwa majina yasiyofaa kama vile
mateja na mengine mengi jambo ambalo halipaswi kuungwa mkono.
"Huko
mitaani jamii inatuita majina ya kila aina na wengine hata wanatuigiza
jambo ambalo siyo sahihi kwani linazidi kutukandamiza sisi
waathiriwa,mimi nadhani hii inatokana na jamii kutokuwa na elimu ya
kutosha kuhusu tatizo la uraibu wa dawa za kulevya,"amesema.
Mraibu anapelekwa jela?
Kamishna
wa Tiba na Kinga wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya (DCEA),Dkt.Peter Mfisi amesema, sheria inatambua kuwa uraibu ni
ugonjwa, hivyo hukumu pekee ni kumpeleka mraibu hospitali na siyo jela
kama jamii inavyofikiria.
Dkt.Mfisi
anasema kuwa,Jeshi la Polisi limekuwa likitumia weledi mkubwa
wanapowakamata waraibu wa dawa za kulevya ambapo hushirikiana na familia
zao kuwasainisha matibabu ya lazima ya kuondokana na uraibu kwa muda wa
miezi sita.
"Jambo la kushangaza,wengi wao wamekuwa hawafuati adhabu hiyo na kurudi kwenye matumizi ya dawa hizo haramu,"amesema.
Tuleteeni taarifa
"Mamlaka
tunafanya kazi kutokana na jamii. Kwa niaba ya Kamishina Jenerali wa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Gerald
Kusaya niwahakikishie kuwa, mtu au watu ambao wataleta taarifa zao
katika mamlaka zinazohusiana na uhalifu wa dawa za kulevya, tutazipokea
kwa uaminifu wa hali ya juu na tutamtunzia siri, hivyo msiwe na hofu
yoyote kama mna taarifa, tuleteeni taarifa,"Anasema Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Bi.Florence Khambi.
Kwa
sheria ya Tanzania, mtu ukifanya kilimo cha dawa za kulevya mfano
ukilima bangi na mirungi (dawa za mashambani) au ukikutwa na mbegu zake,
ukikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 na kosa
hili halina dhamana.
Hii
ni kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
namba 5 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika kuanzia Mwezi Septemba
2015 na kurejewa mwaka 2019.
Wakati
huo huo, Khambi amesema kuwa, dira yao kama mamlaka ni kujenga jamii ya
Tanzania isiyotumia dawa za kulevya au kushiriki katika biashara ya
dawa hizo na hivyo kuchangia lengo kuu la kuwa na maisha bora nchini
kama ilivyochagizwa kwenye Malengo ya Maendeleo ya 2025.
"Na
dhima yetu ni kujenga mfumo bora wa kudhibiti na kupambana na matumizi
na biashara ya dawa za kulevya na kuendeleza ushirikiano katika hatua
mbalimbali za udhibiti wa dawa za kulevya na kujenga uwezo wa taasisi na
asasi zisizo za kiserikali katika mapambano dhidi ya dawa za
kulevya,"amefafanua.
DCEA yakoleza moto
Ili
kuhakikisha Tanzania inakuwa salama bila dawa za kulevya,Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) katika kipindi
cha mwaka mmoja uliopita, imedhibiti uingizwaji wa tani 120.5 za
kemikali bashirifu aina ya yabisi, pamoja na lita 40 za kemikali hiyo
aina ya kimiminika ambazo zilikuwa zikiingizwa nchini.
Mamlaka
hiyo katika kipindi hicho pia, iliweza kukamata wafanyabiashara na
watumiaji wa dawa za kulevya 11,716 ambao walidaiwa kukutwa na kilo 35,
227. 25 za dawa za aina mbalimbali.
Akitoa
taarifa ya mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan
madarakani, Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya, amesema pia
wameteketeza ekari 185 za mashamba ya bangi katika maeneo mbalimbali
nchini, na mashamba ya mirungi ekari 10 ambapo katika zoezi hilo, wapo
watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea kusikilizwa.
"Katika
kipindi hicho jumla ya watuhumiwa 100 walikutwa na dawa aina ya
Cocaine, lakini pia katika kipindi hicho watuhumiwa 588 walikamatwa
wakiwa wanajihusisha na biashara na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya
Heroine, watuhumiwa 9,484 walikamatwa wakijihusisha na dawa za kulevya
aina ya bangi, watuhumiwa 1,395 walikutwa wafitumia na kufanya biashara
ya mirungi, katika kipindi hicho mashamba 132 ya watuhumiwa 132 wa
mashamba ya bangi walikamatwa,"amesema.

Kusaya
amesema, kufuatia Tanzania kufanya vizuri kwenye udhibiti wa kemikali
hizo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na
Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kuwa nchi kinara katika udhibiti wa
kemikali bashirifu, na kuipa jukumu la kutoa elimu kuhusu udhibiti wake
katika nchi tisa barani Afrika.
"Watanzania
wenzangu, kutokana na taasisi yenu kufanya vizuri sana kwenye udhibiti
wa dawa bashirifu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya na Uhalifu-UNODC imeiteua Tanzania kutoa elimu kuhusu udhibiti
huo kwa nchi za Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia,
Msumbiji, Eritrea na Mauritius," amesema Kusaya.
Aidha,
amebainisha kuwa DCEA kwa kushirikiana na taasisi na za Serikali za
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali,
Bohari ya Dawa (MSD) na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya
wanasaidiana katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu.
Lengo
ni kuondokana na dawa za kulevya ambapo wameanzisha mradi wa
ushirikiano kati ya Serikali na taasisi 27 za kemikali hiyo, na vyama
viwili vya dawa za binadamu, ambapo wametia saini mkataba wa makubaliano
ya udhibiti huo.


No comments:
Post a Comment