WAZIRI wa Fedha na Mipango,
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameliambia Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwamba Serikali imejipanga kikamilifu
kuhakikisha kuwa sekta muhimu za uzalishaji zinaongezewa fedha ili
kuongeza tija katika sekta hizo.
Dkt. Nchemba aliyasema hayo
alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Shirika hilo ukiongozwa
na Mwakilishi wake Mkazi Bi. Christine Musisi, Jijini Dodoma.
“Katika
Bajeti ya mwaka 2022/2023, na zijazo, tutawekeza fedha nyingi kwenye
maeneo ya uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kuongeza huduma za umwagiliaji
na uzalishaji wa mbegu bora, uhifadhi wa mazao, mifugo bora, uvuvi na
kuboresha mazingira ya biashara kwa wamachinga” alieleza Dkt. Nchemba
Alisema
kuwa sekta hizo ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita,
inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na inakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya
Taifa ya mwaka 2025 na Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Miaka Mitano.
Dkt. Nchemba, alilipongeza Shirika hilo la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa – UNDP kwa kuchangia maendeleo ya nchi
katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kuliomba Shirika hilo
kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi
maendeleo.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi.
Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano unakadiriwa kugharimu shilingi trilioni 114.8 ambapo
kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 40.6 zinatakiwa zitoke Sekta
Binafsi na kuliomba UNDP, kusaidia upatikanaji wa fedha hizo kwa
kushirikiana na washirika wake mbalimbali.
Kwa upande wake
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa mataifa-UNDP, Bi.
Christine Musisi, ameihakikishia Tanzania kwamba Shirika lake
litaendelea kushirikiana nayo kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii
kupitia miradi mbalimbali iliyowekeza fedha nchini ikiwemo kilimo,
uchumi wa bluu na kuboresha sekta nyingine za uzalishaji.
Aliahidi
kuwa Shirika lake litaendelea kutoa fedha kwenye maeneo ya uzalishaji
na uwekezaji kupitia Wizara ya Fedha na Mipango lakini pia kuwashawishi
wadau wengine kote duniani kuwekeza fedha katika maeneo mbalimbali ya
uwekezaji yatakayochangia kuondoa umasikini na kutanzua changamoto zote
za uzalishaji mali kupitia sekta binafsi na wajasiriamali.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati),
akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi
wake Mkazi, Bi. Christine Musisi, Jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban na kushoto ni
Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara hiyo, Bi. Sauda Msemo.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisisitiza
jambo, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi,
Bi. Christine Musisi (hayupo pichani), Jijini Dodoma
Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, Bi. Christine
Musisi akizungumza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)
(hayupo pichani), Jijini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa
katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa-UNDP, Bi. Christine Musisi, baada ya kumaliza
mazungumzo yao Jijini Dodoma.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Katikati),
akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la
Umoja wa Mataifa-UNDP, ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi, Bi.
Christine Musisi (wa nne kushoto), pamoja Ujumbe kutoka Wizara ya Fedha
na Mipango, Jijini Dodoma.
Post Top Ad
Your Ad Spot
Saturday, April 2, 2022
DKT. NCHEMBA: SERIKALI KUWEKEZA ZAIDI KWENYE SEKTA ZA UZALISHAJI
Tags
LOCAL#
Share This
About kilole mzee
LOCAL
Labels:
LOCAL
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment