Kufuati kusambaa kwa taarifa juu
ya uwepo wa ugonjwa wa mlipuko wa Polio nchini Malawi, baadhi ya Wilaya
hapa nchini zilizopo mipakana mwa nchi hiyo ikiwemo Wilaya ya Ludewa
Mkoani Njombe zimeanza kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo kwa kuanza
kampeni shirikishi ya chanjo ya Polio.
Akizungumza katika kikao
cha Kamati ya Afya ya Msingi wilayani Ludewa Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo
Stanley Mlayi amesema tayari wameshaandaa timu ya kuendesha zoezi hilo
la utoaji chanjo ambalo litafanyika kuanza tarehe 24 mpaka 27 mwezi huu
na litahusisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano.
Amesema
tayari wameshaunda timu ya kuendesha zoezi hilo ambalo litafanyika
katika vituo vya afya pamoja na kuzunguka nyumba kwa nyumba ili
kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata chanjo na watakaochanjwa watakuwa
na alama itakayowaonyesha kuwa tayari wamepatiwa chanjo hiyo.
Sanjari
na hilo mganga mkuu amesema kuwa kumekuwa na upotoshaji kwa baadhi ya
watu juu ya chanjo mbalimbali zitolewazo kitu ambacho kinawapa mazingira
magumu ya kufanikiwa hivyo ameiomba kamati ya ulinzi na usalama ya
Wilaya hiyo kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya
upotoshaji huo.
"Kwa sasa zoezi la kutoa chanjo yoyote ile
limekuwa gumu katika jamii, wakati timu husika inapita kutoa elimu ya
watu kupata chanjo huku nyuma watu wengine wanapita kuwapotosha watu
kutopata chanjo, yaani watu wamekuwa wepesi kuelewa kampeni za kisiasa
kuliko kampeni za chanjo", Amesema Mlayi.
Aidha kwa upande wake
Mratibu wa chanjo wilayani hapo James Kadege amesema kuwa chanjo hiyo
itawahusu watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano na hata kama
alikwisha pata atalazimika kupatiwa tena ili kujiridhisha na chanjo mpya
kwani inawezekana awali alipatiwa lakini haikuwa imekamilika.
Ameongeza
kuwa utoaji wa chanjo hii wakazi wa mwambao watapewa kipaumbe zaidi
kwakuwa ukanda huo ndio upo jirani zaidi na nchi ya Malawi hivyo
amewaomba wananchi wote wa mwambao na Ludewa kwa ujumla kuhakikisha
walengwa wanapata chanjo hiyo.
Linus Malamba ni Kaimu Katibu
Tawala wa Wilaya hiyo ambaye amehudhuria kikao hicho kwa niaba ya mkuu
wa wilaya amesema timu hiyo iliyoundwa inapaswa kutoa elimu ya kutosha
katika maeneo ya mikusanyiko kama Makanisani, Msikitini na sokoni ili
watu waweze kupata uelewa juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.
"Watu
walikuwa wanapotoshana sana juu ya chanjo ya UVICO-19 lakini pamoja na
upotoshaji huo elimu ilitolewa na jambo hili likafanikiwa hivyo ni
matumaini yetu pia katika hili elimu ikitolewa litafanikiwa kama
yalivyofanikiwa mengine", Amesema Malamba.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ludewa Linus Malamba akiwa amemuwakisha Mkuu wa Wilaya katika kikao cha kamati ya Afya ya Msingi ya Wilaya Kwa ajilinya uhamasishaji wa chanjo ya Polio.Mratibu wa Chanjo wilaya ya Ludewa James Kadege akiwasilisha mada katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya, kwaajili ya Uhamasishaji wa chanjo ya Polio.Baadhi ya Wanakamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Ludewa wakifuatilia mjadala wa namna ya utoaji chanjo ya Polio kwa watoto walio chini ya miaka 5
No comments:
Post a Comment