IKIWA umepita
mwezi mmoja tu tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji
katika Sekta ya Madini wa mwaka 2022, tayari Waziri wa Nishati na Madini
wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Ibrahim Uwizeye amefika nchini kwa lengo la
kujifunza zaidi kuhusu Sekta ya Madini hususani utekelezaji wa mradi
mkubwa wa uchimbaji wa madini ya nikeli.
Waziri
wa Nishati na Madini wa Burundi, Mhe. Ibrahim Uwizeye akiangalia
madini ya nikeli alipotembelea mgodi huo Machi 14, 2022 Wilaya ya Ngara
Mkoa wa Kagera
Ziara
ya Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi nchini inakuja baada ya
kuhudhuria mkutano wa madini ambao ulikuwa wa manufaa kwa nchi hiyo.
Hivyo,
alimuomba Waziri wa Madini kuja kujifunza zaidi kutoka kwa Tanzania
kutokana na namna ilivyofanikiwa katika usimamizi wa Sekta ya Madini
ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya madini ili hatimaye rasilimali
madini zinazopatikana nchini Burundi zilinufaishe taifa hilo.
Akizungumzia
lengo la ziara hiyo, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema imelenga
kujifunza kupitia mradi huo ili kuona namna ambavyo nchi hiyo inaweza
kujifunza kutoka Tanzania na namna ambavyo nchi hizo zinavyoweza
kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya namna hiyo na kuongeza
kuwa, ni mapema sana kusema kitakachofuata baada ya ziara hiyo.
“Mradi
wa Kabanga Nikeli na Msongati nchini Burundi ni mmoja, jiolojia ya
Kabanga na Msongati ni moja na kama mnavyojua jiolojia haina mipaka
isipokuwa mipaka ya kiutawala. Pia, wamefika kuona namna nchi hizi
zinavyoweza kufanya ili hatimaye ziweze kuwa mfano bora wa ushirikiano
kwa mataifa mengine Afrika,” amesema.
Aidha,
Waziri Biteko amemuelezea waziri huyo kuwa ni mtu mwenye kiu na wivu wa
maendeleo ya kuona rasilimali madini inalinufaisha taifa hilo kwa kuwa
amekuwa akifuatilia Sekta ya Madini nchini kwa kipindi kirefu na
kuongeza, “nimpongeze sana waziri wa Burundi kwa kuwa na wivu wa
rasilimali madini kwani tusipokuwa na wivu wa rasilimali zetu baadaye
tutachekwa.’’
Aidha,
Waziri Biteko ameonya kuhusu wale wote wanaotegesha kwa lengo la
kunufaika na malipo ya fidia na kueleza kuwa hawatalipwa chochote
isipokuwa tu kwa wananchi wenye uhalali wa kulipwa.
Pia, ameongeza kuwa, Serikali haitawavumilia wale wote wanaofanya vitendo vya tegesha.
Kwa
upande wake, Waziri Uwizeye amesema ujumbe wake umefika nchini
kujifunza ili mradi huo uweze kuzinufaisha nchi zote ikiwemo kuhakikisha
nchi hiyo pia inachimba madini hayo na hivyo kuiomba Tanzania kuipa
nafasi ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa jiolojia ya
madini hayo pia inapatikana nchini humo.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi amemhakikishia Waziri
Biteko kuwa, Wilaya hiyo haitokuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi wa
uchimbaji wa nikeli.
Ametumia
fursa hiyo kuelezea masuala muhimu matatu ambayo tayari yamefanywa na
wilaya hiyo, ikiwemo kufanya zoezi la kutambua maeneo ya kupisha mradi;
mazungumzo ya awali kati ya wawekezaji na wananchi katika ngazi zote; na
mapitio ya makubaliano ya kuhamisha wananchi.
Aidha,
Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo pia kumuomba Waziri Biteko
kuweka msukumo ili kuwezesha mradi huo kuanza kwa wakati uliopangwa.
Akizungumza
katika ziara hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Gilly Maleko
amesema baada ya kuwepo mahusiano mazuri ya kidiplomasia kwa nchi hizo
ambazo zimekuwa marafiki kwa miongo mingi, ilionekana kuwa ipo haja ya
kukuza mahusiano ya kiuchumi.
Naye,
Balozi wa Jamhuri ya Burundi nchini Tanzania, Gervouis Abayeho, amesema
baada ya kufahamu kuwa Tanzania ina uzoefu wa muda mrefu katika Sekta
ya Madini, nchi hiyo imeona ipo haja ya kujifunza kutoka Tanzania ili
kupata uzoefu utakaoiwezesha nchi hiyo kusimamia Sekta ya Madini kwa
manufaa ya nchi hiyo ikiwemo kuzisaidia nchi hizo kugeuza sura za
kiuchumi kwa mataifa hayo.
Kadhalika,
Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba Ruhoro, ameihakikishia
nchi hiyo kuwa kama mbunge wa eneo hilo atahakikisha anapambania ujenzi
wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara na umeme ili utekelezaji wa
mradi huo ufanyike kikamilifu. Ameitaka nchi hiyo kuendelea na mipango
ya kuchimba madini hayo kwa kuwa miundombinu itaboreshwa.
“Burundi
haipo karibu na bandari, ikichimba nikeli itapitisha kwetu tutapata
fedha lakinipia kama nchi, tutanufaika na madini kutoka nchi jirani,’’
amesema Ruhoro.
Kwa
upande wake, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nikeli Benedict Busunzu
akiwasilisha taarifa kuhusu mradi huo amesema uhai wa mgodi unatarajiwa
kuwa zaidi ya miaka 30 na kuongeza kuwa, tayari Kampuni hiyo imepata
mbia mwenza Kampuni ya BHP ambayo ni kampuni kubwa ya madini duniani
inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia katika
utekelezaji wa mradi huo.
Ameitaja
teknolojia hiyo kuwa ni ya Hydrometallurgy kuwa ni ya kwanza
kutekelezwa duniani ambayo pia, itakuwa rafiki mkubwa wa mazingira.
Busunzu
ameitaja nikeli ya Kabanga kuwa ni ya daraja la juu duniani na kuutaja
mradi huo kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Tanzania.
Akizungumzia
soko la madini hayo duniani, amesema ni yanahitajika sana kutokana na
kuhama kwa matumizi ya teknolojia na kueleza kuwa, kabla ya kuzuka kwa
vita ya Urusi na Ukraine bei ya madini hayo kwa tani ilikuwa ni Dola za
Marekani 21,000 na kupanda hadi Dola za Marekani 51,000 na ndani ya
muda mfupi kufikia Dola za Marekani 100,000 kwa tani moja ya nikeli.
Ameongeza kuwa, hivi sasa bei yake imeshushwa hadi kufikia Dola za Marekani 48,000 kwa tani ili kulinda mwenendo wa soko lake.
No comments:
Post a Comment