MAKAMU
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip
Mpango amezindua Wiki ya Maji pamoja na kuweka jiwe la msingi mradi wa
maji wa Orkesumet unaogharimu sh.bilioni 41.5 uliopo Simanjiro mkoani
Manyara.
Dkt.Mpango
ameweka jiwe la msingi mradi huo uliofadhiliwa kwa asilimia 100 na
Serikali ya Tanzania ambao umekamilika kwa asilimia 99.
Akizungumza
na wananchi wa Loiborsoit mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika
mradi huo, Makamu wa Rais amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea
kulinda mradi huo ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira ili kutopoteza
chanzo cha maji kilichopo katika eneo hilo kinachotegemewa katika mradi
mkubwa wa maji wa Orkesumet.
Amesema,
serikali imetumia fedha nyingi sana kugharamia mradi huo, ili wananchi
wake waweze kupata huduma ya maji ambayo ni suala muhimu na ndio uhai.
"Hakika
mradi huu utawanufaisha wananchi na kuwapunguzia mzigo wanawake
waliokuwa wanatumia saa tano kufuata maji kwa punda,"amesema Dkt.Mpango.
Aidha,
amesema mradi huo umekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Simanjiro,
kwani Kwa kipindi chote hawajawahi kupata Maji , hivyo kupata maji kwao
ndio kila kitu, kikubwa ni kuhakikisha mradi huo unatunza ili kuja
kuwanufaisha vizazi na vizazi.
Kwa
upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wanawake wa Simanjiro
awali walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 40 kufuatia Maji, kiasi
ambacho kwenda na kurudi ni sawa na kilomita 80, ambapo kwa sasa adha
hiyo imebaki kuwa historia.
Aweso
amesema wizara itaendelea kutekeleza miradi kwa ufanisi pamoja na
kuokoa gharama zisizo za lazima katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Waziri
Aweso amesema, utekelezwaji wa mradi huo kwa kutumia wakandarasi wa
ndani unatoa fursa ya kuaminiwa kwa wakandarasi wa ndani ya nchi huku
akiwataka watendaji katika wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii ili
kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Aidha,
mmoja wa madiwani wa viti maalum wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro
mkoani Manyara humo, Bahati Patison Mosses anaishukuru Serikali ya Awamu
ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbuka katika
kuwapatia mradi huo wa maji ambao kwao ni tunu kubwa.
Hata
hivyo, Mosses ameongeza kuwa, mradi huo ni msaada mkubwa kwa jamii ya
Simanjiro kwani kwa jamii ya Kimasai wanaotakiwa kutafuta maji ni akina
mama, hivyo akina mama hao walikuwa wakilazimika hata kulala siku mbili
hadi tatu kukesha kusubiria maji.
No comments:
Post a Comment