Baadhi
ya magari yatakayotumiwa kuchukua data za mitetemo za 3D katika Kitalu
cha Ruvuma yakiwa tayari kabisa katika kambi ya AGS iliyopo Mtwara.
MAANDALIZI
ya uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma
kilichopo Mkoani Mtwara yameshika kasi ambapo mkandarasi atakayefanya
kazi ya uchukuaji wa data hizo (Kampuni ya Africa Geophysical Services –
AGS) kwa niaba ya mwendeshaji wa Kitalu cha Ruvuma (Kampuni ya ARA
Petroleum) anaendelea na kazi ya kusafisha njia zitakazotumiwa wakati wa
uchukuaji data. Aidha, mkandarasi huyo ameendelea na kazi ya kutoa
elimu kuhusiana na kazi tarajiwa kwa wanakijiji wanaoishi eneo la mradi.
AGS
ilianza maandalizi ya kazi hii mwishoni mwa mwaka jana na inatarajiwa
kuanza uchukuaji wa data hizo za mitetemo za 3D siku za usoni,
ikihusisha eneo la kilomita za mraba 334. Magari ya kusafisha njia
zitakazotumiwa wakati wa uchukuaji wa data hizo yanaendelea na kazi eneo
la mradi. Hadi sasa, kupitia kazi za maandalizi ya uchukuaji wa data
tajwa, watanzania zaidi ya 60 wameweza kuajiriwa katika mradi na makumi
ya watoa huduma wakitanzania wamenufaika.
Kazi
ya uchukuaji wa data za mitetemo za 3D inayotekelezwa na ARA Petroleum
kupitia AGS ni miongoni mwa kazi zinazopaswa kutekelezwa kisheria kwa
mujibu wa masharti ya leseni. Kazi zingine ni kuchimba kisima kimoja cha
utafutaji cha Chikumbi 1 na kukamilisha majadiliano ya mauziano ya gesi
(gas terms) kulingana na Mkataba wa Uzalishaji wa Ugawanaji Mapato wa
Kitalu cha Ruvuma. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
ambaye ndiye mshika leseni za vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi
asilia kwa niaba ya Serikali, anafanya kazi bega kwa bega na mwendeshaji
wa Kitalu hicho kuhakikisha masharti ya leseni yanatekelezwa kwa
ufanisi na kwa wakati.
Ufuatiliaji
wa utekelezaji wa kazi zinazoendelea katika Kitalu cha Ruvuma na vitalu
vingine vilivyo katika hatua ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na
gesi asilia nchini hufanywa na Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa
Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA) kwa mujibu wa
Sehemu ya 12(2) ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015. Miongoni mwa maeneo
yanayoangaziwa na PURA wakati wa kaguzi za ufuatiliaji ni masuala ya
kitalaamu na ushirikishwaji wa watanzania katika kazi zinazotekelezwa.
Gari aina ya bulldozer ikisafisha njia zitakazotumika wakati wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma.
Kazi
ya tathmini ya uharibifu wa mazao katika Kijiji cha Maranje Kilichopo
Kata ya Mtiniko. Pichani ni wathamini kutoka kampuni ya Tansheq,
mwenyekiti wa Kijiji cha Maranje na baadhi ya wanakijiji ambao maeneo
yao yamepitiwa na magara yanayosafisha mistari itakayotumiwa wakati wa
kazi ya uchukuaji wa data.
Mjiolojia
kutoka TPDC, Bw. Lucas Luhanga (mwenye kofia nyeupe) akifanya mahojiano
na mthaminishaji, Bw. Eric kutoka kampuni ya Tansheq kuhusiana na
rekodi iliyofanyika. Katikati ni Bw. Issa Nangoma, mwenyekiti wa Kijiji
cha Maranje iliyopo Kata ya Mtiniko (Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara)
Gari aina ya bulldozer ikisafisha njia zitakazotumika wakati wa uchukuaji wa data za mitetemo za 3D katika Kitalu cha Ruvuma
No comments:
Post a Comment