"Tunawasihi
wafanyabiashara kote nchini kutopandisha bei ya sukari katika mwezi
mtukufu wa Ramadhani ili kuepuka taharuki inayoweza kujitokeza"
23 Machi 2022: Dar es Salaam
— Kampuni ya Sukari ya Kilombero na kusambaza sukari chini ya chapa ya
“Bwana Sukari” inapenda kuwatoa hofu wananchi, hususani wapenzi na
watumiaji wa sukari ya Kilombero “Bwana Sukari” kuhusu upungufu wa
sukari katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza
mwanzoni mwa mwezi Aprili.
Hayo yamesemwa na Fimbo Butallah, Mkuu
wa Idara ya Biashara siku ya Jumatano, 23 Machi, 2022 katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za kampuni hiyo jijini Dar
es Salaam.
Tamko hilo limekuja kutokana na historia ya kupanda
kwa bei za bidhaa nyingi za vyakula kila uanzapo mfungo wa mwezi mtukufu
wa Ramadhani na kusababisha adha kubwa kwa wananchi, hususan waumini
wanaofunga katika mwezi huo. Kutokana na hilo, kampuni ya Sukari ya
Kilombero imewasihi wafanyabiashara wote, wa jumla na rejareja wanaouza
bidhaa za “Bwana Sukari” kutopandisha bei, jambo ambalo limekuwa
likiwakandamiza watumiaji wa sukari ambapo matumizi yake huongezeka
zaidi katika mfungo wa Ramadhani.
Akizungumza mbele ya waandishi
wa habari, Fimbo alisema, “Tunafahamu kuwa katika uchumi wa soko huria,
sisi kama wazalishaji haturuhusiwi kuwapangia wafanyabiashara bei ya
kuuza bidhaa. Hata hivyo tunao wajibu mkubwa wa kuwashauri kuhusu
upandishaji holela wa bei, haswa pale ambapo sisi kama wazalishaji wa
sukari hatujapandisha bei ya bidhaa hiyo. Tunawasihi wafanyabiashara
kote nchini kutopandisha bei za sukari katika mwezi mtukufu wa Ramadhani
ili kuepuka taharuki inayoweza kujitokeza.”
Akizungumzia suala
la uhaba wa sukari ambao mara nyingi hujitokeza katika mfungo wa
Ramadhani, Fimbo alisema kuwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero inayo akiba
ya kutosha kulivusha taifa katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani
na kuongezea kuwa tayari kampuni imepata kibali cha kuagiza sukari
kutoka nje ya nchi ili kuziba pengo la uzalishaji.
“Tumekwishaanza
taratibu za uagizaji wa sukari ambayo inatarajiwa kuanza kuingia nchini
muda wowote kuanzia hivi sasa. Tunapenda kuwatoa hofu wananchi kuhusu
upandaji holela wa bei ya sukari, hususan chapa ya “Bwana Sukari” kwani
kampuni imeandaa mikakati thabiti kukabiliana na tatizo hilo katika
msimu huu”, alisema Fimbo.
Kampuni ya Sukari ya Kilombero, ambayo
inamilikiwa na Kampuni ya Illovo Sugar Africa kwa Asilimia 75 na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 25 ipo katika
maandalizi ya mradi wake wa upanuzi ambao utakuza uwezo wa kampuni hiyo
wa kutengeneza sukari na kupunguza uhaba wa sukari nchini kupitia chapa
yake ya “Bwana Sukari”.
Post Top Ad
Your Ad Spot
Wednesday, March 23, 2022
Home
BIASHARA
KILOMBERO YAWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI WA SUKARI KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI
KILOMBERO YAWAHAKIKISHIA WANANCHI UPATIKANAJI WA SUKARI KATIKA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI
Tags
BIASHARA#
Share This
About kilole mzee
BIASHARA
Labels:
BIASHARA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment