KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua mradi wa
Lango la Naabi wenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 na ujenzi wa
Serengeti Media Centre unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Korea
(KOICA) wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 1.5 katika Wilaya ya
Serengeti mkoani Mara.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii , Mhe. Ally
Juma Makoa (Mb) amesema miradi hiyo ina manufaa makubwa kwa Taifa katika
kuongeza idadi ya watalii nchini.
“Tunaishukuru
sana Wizara kwa wazo zuri la kujenga Serengeti Media Center ambayo
itasaidia kuitangaza nchi yetu Kitaifa na Kimataifa kwa sababu wageni
watapata taarifa zote za hifadhi hii kupitia picha na matangazo,”
amefafanua Mhe. Makoa.
Akizungumzia
mradi wa Lango la Naabi Mhe. Makoa amesema kuwa lango hilo litaleta
taswira nzuri na litaongeza thamani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ambayo
mara tatu mfululizo imechukua tuzo mbalimbali.
Naye,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema
mradi wa Serengeti Media Centre umekamilika kwa asilimia mia moja na kwa
upande wa mradi wa Lango la Naabi utakamilika kwa kadri fedha
zinavyoendelea kuletwa.
Aidha,
Mhe. Masanja amemuahidi Mwenyekiti wa Kamati hiyo kutekeleza maelekezo
yote yaliyotolewa na kamati na kwamba Wizara itasimamia miradi hiyo
vizuri.
Amesema,
lengo ni kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutekeleza
ahadi zake kwa wananchi kwa nguvu zote ili kufikia malengo
yaliyotarajiwa kwa wananchi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi ambayo ni kufikisha watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025
na pia kuongeza mapato yatokanayo na watalii kutoka Dola za Kimarekani
bilioni 2.6 hadi Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment