Wizara ya Maliasili na Utalii
imeanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka kumi wa Kuenzi na
Kusherehekea Urithi wa Utamaduni unaotokana na Maisha ya Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyarere.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Francis Michael wakati
akifungua kikao kazi cha wataalam wa Wizara ya Maliasili na wadau
mbalimbali kuweka mikakati ya utekelezaji wa adhimisho la miaka 100 ya
Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma.
Dkt. Michael aliongeza kuwa
lengo la Wizara ni kuhakikisha urithi unaotokana na maisha ya Baba wa
Taifa unatumika katika kuliunganisha Taifa kijamii, kisiasa na kiuchumi
hivyo ameziagiza Taasisi zote za Wizara kushiriki kikamilifu katika
maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika Aprili13, 2022, Butiama Mkoa
wa Mara.
“Tangu kuzaliwa kwake, Mwalimu alionesha uzalendo kwa
nchi yake na kujitoa katika harakati mbalimbali za mapambano ya kudai
uhuru na kujenga uchumi sio wa Taifa lake tu bali kokote kule kulikokuwa
na uonevu”. Amesisitiza Dkt. Michael
Hata hivyo Dkt Michael
ameeleza kuwa jambo la muhimu ni kuhakikisha fursa hii inatumika
kutangaza utalii pamoja na kuonesha mchango wa Mwalimu Nyerere katika
sekta hiyo na kutaka Bodi ya Utalii Tanzania na Taasisi za Wizara
zishiriki ipasavyo kutangaza Adhimisho hilo.
Akielezea
maandalizi ya adhimisho hilo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale
nchini Dkt. Kristowaja Ntandu ameleza kuwa hadi sasa Taasisi na wadau
zaidi ya 10 zimejitokeza kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii
katka maadhimisho hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya
Taifa Dkt. Noel Lwoga ametaja matukio yatakayo pamba maadhimisho hayo
kuwa ni pamoja na matembezi, mchezo wa bao, burudani mbalimbali za
muziki wa dansi, ngoma za asili, kughani mashairi, maonesho ya Wizara na
Taasisi mbalimbali.
“Maadhimisho haya pia yataambatana na hafla
ya kifamilia itakayofanywa na ukoo wa Mwalimu Nyerere ikihusisha ibada
kanisani, midahalo, makongamano na Semina, Onesho maalum la mchango wa
Mwalimu Nyerere katika maendeleo ya nchi pamoja na Kalamu ya Mwalimu”.
Aliongeza Dkt Lwoga
Adhimisho hilo ni sehemu ya Mpango wa miaka
10 wa Kuenzi na Kusherehekea Urithi wa Utamaduni unaotokana na Maisha ya
Mwalimu Julius Nyarere ambao kwa nyakati mbalimbali litakuwa
likiadhimishwa kila mwaka Aprili 13 na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mfano wa namna uwanja wa tukilo la maadhimisho ya miaka 100 ya Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma utakavyo kuwa
Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael na wajumbe wengine wakifuatilia uwasilishaji wa maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Francis Michael akifunfua kikao kazi cha wataalam wa Wizara ya Maliasili na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya utekelezaji wa adhimisho la miaka 100 ya Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga akizungumza na wanahabari juu ya maadalizi ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment