KAMISHNA
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania, Dkt. Gerald Ndika amewataka mahakimu nchini kutokiuka viapo
vyao wakati wa utoaji haki ikiwa ni pamoja na kutopokea rushwa.
Pia
amezitaka kamati za maadili kushirikiana kwa karibu na mihimili yote
mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama ili kuweza kuboresha utoaji
wa haki kwa wananchi.
Dkt.Ndika
ametoa kauli hiyo wakati Tume ya Utumishi wa Mahakama imefanya ziara
mkoani Tanga kwa lengo la kuangalia namna ya kuboresha miundombinu yake
na kuboresha huduma kwa wananchi.
Amesema,
lengo la ziara ya tume hiyo mkoani Tanga ni kukaa na kamati za maadili
za wilaya na mkoa ili kupokea maoni na changamoto za uvunjifu wa
maadili kwa watumishi wa mahakama ili kuboresha shughuli za utendaji na
utoaji haki ikiwa ni pamoja, na kuzingatia viapo vyao.
"Mahakama
ya Tanzania imeaminiwa na wananchi katika suala la utoaji haki,ukisha
kiuka viapo kwa njia yeyote ile aidha kupokea rushwa tayari umeacha ule
wajibu wako kama wakili,kutokuchelewesha haki bila sababu za
msingi,"aliongeza.
Kamishna
Ndika amesema lengo la tume kukutana na watumishi hao ni kujadili
changamoto mbalimbali ndani ya mhimili huo huku ikisisitiza utoaji haki
kwa wananchi.
Aidha,
Kamishna Ndika amewataka Mahakimu na majaji kuzingatia kanuni na sheria
mbalimbali zinazowaongoza katika kazi zao bila kukiuka wakati wa utoaji
haki pamoja na kutokuchelewesha haki kwa wananchi,
"Tumewasisistiza
watumiaji wote wa Mahakama wazingatie sheria kwa kutokwenda na kukiuka
maadili yao katika utoaji haki kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na
kutochelewesha haki za wananchi bila sababu za msingi,"alibainisha
Dkt.Ndika.
Aliongeza
kuwa, kwa upande wa kamati za maadili, "tunawaasa wale wote wanaoziunda
hizo kamati washirikiane kwa karibu na mihimili yote mitatu ili tuweze
kuboresha utoaji haki hapa nchini kwa maslahi ya nchi yetu,"alisistiza
Dkt.Ndika.
Sambamba
na hayo Mkuu wa Mkoa wa Tanga ,Adam Malima amesema kuwa licha ya
kufurahishwa na ujio huo wa Tume mkoani Tanga ambao utasaidia kuboresha
shughuli za kimahakama, lakini pia amesema watahakikisha wanaimarisha
ushirikiano baina yao na watendaji wa mahakama kwa kuzingatia utoaji wa
haki kwa kila mwananchi.
"Serikali
ya mkoa wa Tanga tumefarijika sana kwa ujio wenu , tutaendelea kufanya
kazi kuwa kutegemeana, tutawatumia pia viongozi wa dini tukitambua
nafasi ya kila mmoja,"alisema Malima.
Tume
hiyo imeketi kwa siku mbili mkoani Tanga kwa lengo la kukutana na
watumishi wa mahakama ili kusikiliza changamoto na maoni kwa lengo la
uboreshaji shughuli za utendaji wa mahakama ambapo kwa mwaka huu wa 2022
tayari imeshapita katika mikoa mitatu ya Tanga, Morogoro na Pwani.
No comments:
Post a Comment