A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Wednesday, September 8, 2021

ITC ZAWANYIMA NAFASI WACHEZAJI WA YANGA SC KUWAKABILI RIVERS UNITED FC

 Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV


Klabu ya Soka ya Yanga imetangaza kuwakosa Wachezaji wake wapya na muhimu, Khalid Aucho, Fiston Mayele na Djuma Shabani katika mchezo wa hatua za awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United FC ya Nigeria mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili ya Septemba 12, 2021.

Yanga SC imetangaza kuwakosa Wachezaji hao kupitia kwa Afisa Habari wake, Haji Sunday Manara, amesema kuwakosa Wachezaji hao halikuwa kosa la Yanga kutokana na kupeleka maombi ya Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa wakati uliopangwa.

“Kuwakosa Wachezaji hawa hayakuwa makosa yetu sisi Yanga, mfano Mayele, Djuma mikataba yao ilikuwa mwisho tarehe 31, sisi tulipeleka DR Congo maombi ya ITC na tulipoingia nao mikataba wakasema tusubiri hadi tarehe 31 wakati dirisha lilikuwa linafungwa”, amesema Haji Manara.

Manara amedai kuwa Yanga SC ilipeleka maombi hayo ya ITC kwa wakati uliopangwa lakini pia imeshindikana kupatikana kwa Hati hizo kwa wakati uliopangwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Kwa upande wa Mchezaji Khalid Aucho, Manara ameeleza kuwa Aucho alikuwa na mgogoro wa maslahi na Klabu yake ya zamani ya Makkasa SC ya Misri, baadae Mchezaji huyo alikuwa huru na kusajiliwa na Yanga SC kwa wakati sahihi wa usajili.

Manara amesema, “Aucho alikuwa anacheza Misri hivyo kutokana na mgogoro uliopo kati yake na timu yake ya zamani, ndio maana wamezuia ITC yake, hivyo imeshindikana kupatikana ITC hiyo kwa mujibu muda uliopangwa na CAF wakazuia ITC ya Mchezaji huyo wa Kimataifa kutoka Uganda”.

“Tumefanya jitihada kuwasiliana na CAF lakini hawajatoa majibu yoyote kwa Wachezaji hao kucheza, tumewaandikia barua Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) kupitia TFF kuomba kupata ITC za Wachezaji wote kwa muda kabla ya mchezo huo dhidi ya Rivers United”, ameeleza Manara.

Amesema ikitokea FIFA kushindwa kutoa majibu kuhusu ITC za Wachezaji hao, Yanga SC itacheza mchezo huo kutumia Wachezaji wake waliopo sasa. Pia amewataka Wanayanga kutoa hofu kuhusu Kikosi chao ambacho kimefanya maandalizi ya kutosha chini ya Kocha Mkuu, Nassredine Nabi kwa ajili ya mchezo huo.

Hata hivyo, CAF hawajatoa majibu kupitia TFF kuhusu idadi ya Watazamaji watakaoruhusiwa kuingia kutazama mchezo huo. Ndani ya masaa 24 kuanzia sasa CAF watatoa majibu ya kiwango cha Mashabiki wanaoruhusiwa kuingia Uwanjani kushuhudia mchezo huo kabla ya Klabu hiyo kutangaza viingilio vya mchezo husika.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages