Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akiwapongeza wanafunzi wa
vyuo vikuu ambao wamechaguliwa kushiriki programu ya mafunzo ya uongozi
kwa wahitimu wa vyuo vikuu “Graduate Development” inayoendeshwa na
Benki ya CRDB. Kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya
CRDB, Siaphoro Kishimbo.
Benki
ya CRDB imezindua program ya mafunzo ya uongozi kwa wahitimu wa vyuo
vikuu “Graduate Development Program,” ambayo inalenga katika kuwaandaa
wahitimu wa vyuo kuwa wabobevu katika masuala ya benki, na kuwajenga
katika uongozi.
Akizungumza
katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika hoteli ya Serena,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB alisema programu hiyo itasaidia
kujenga viongozi wa kesho wa benki hiyo na kuifanya kuendelea kuwa
shindani katika soko nchini.
“Benki
yetu inakua kwa kasi sana kwa maana ya kupanuka kwa mtandao wa matawi
nchini, lakini pia tupo Burundi na tupo katika mchakato wa kwenda Congo
DRC. Ukuaji huu unatuhitaji sisi kama Benki kuandaa viongozi wa kesho na
wafanyakazi ambao wataweza kuendana na mabadiliko katika soko,”
aliongezea Nsekela.
Programu
hii imezinduliwa kipindi muafaka ambacho Serikali na wadau wa maendeleo
nchini wanawekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo vikuu
nchini wanapata ajira na kutengenezewa mazingira ya kujiajiri.
“Leo
hii tukiwa tunazindua programu hii, tayari tunao vijana 32, watatu
kutoka Burundi, ambao wanapitia mafunzo haya ya Graduate Program. Vijana
hawa wanapitishwa katika mafunzo ya hali juu katika matawi, idara na
vitengo mbalimbali ndani ya Benki ili kuwajenga kuwa wabobevu, na baada
ya miaka mitatu ya programu wanapata ajira kamili,” alisema Nsekela huku
akibainisha kuwa programu hiyo ni moja ya jitihada za Benki ya CRDB
kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo
vikuu.
Akielezea
mchakato uliotumika kuwapata wanafunzi hao, Mkurugenzi Rasilimali Watu
Benki ya CRDB, Siaphoro Kishimbo amesema mwaka jana mwishoni benki hiyo
kwa kushirikiana na kampuni ya rasilimali watu ya Niajiri ilitangaza
nafasi za mafunzo hayo ambapo wanafunzi wengi waliomba na kupitishwa
katika mchakato wa usahili ambapo 32 walichaguliwa.
“Mpaka
sasa ni miezi mitano tokea vijana hawa wajiunge katika program hii.
Kama Benki tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la ajira kwa vijana,”
alisema Kishimbo huku akibainisha kuwa baada ya miaka mitatu ya kuhitimu
vijana wengine wanaohitimu vyuo vikuu wataajiriwa kupitia programu
hiyo.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema
Mori aliwapongeza vijana ambao wamepata nafasi ya kushiriki programu
hiyo huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi wa hali ya
juu.
“Nimeambiwa
mmeanza vizuri sana na mmeshaanza kuwa wabobevu katika maeneo ya awali
mliyopitishwa. Matarajio yetu ni kuwaona katika nafasi za uongozi baada
ya miaka hii mitatu kama alivyoeleza Mkurugenzi Mtendaji,” alisisitiza
Prof. Mori.
Akitoa
salamu za shukrani kwa niaba ya washiriki wa program hiyo, Aurelia
Haule aliushukuru uongozi wa Benki ya CRDB kwa kutoa fursa ya mafunzo na
ajira kwa vijana. Alisema kwa kipindi cha miezi mitano ya walichojiunga
na benki hiyo wamejifunza vitu vingi kuhusiana na uendeshaji na
usimamizi wa benki. “Ni imani yangu kuwa baada ya programu hii
tutakwenda kuwa wabobevu na kuisaidia benki yetu kupiga hatua kubwa
kiutendaji,” aliongezea Aurelia.
No comments:
Post a Comment