A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, May 4, 2021

KATIBU ITIKADI NA UENEZI CCM AANZA NA UMUHIMU WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI.

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Chama hicho pamoja na Serikali zake zinatambua na kuheshimu vyombo vya habari pamoja na wanahabari hasa kwa kutambua tasnia hiyo ina mchango mkubwa wa maendeleo ya Taifa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Shaka Hamdu Shaka  kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Mei 4,2021 amesema kila ifikapo Mei 4 ya  kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya Habari, hivyo CCM na Serikali zake zinatambua na kuheshimu vyombo vya habari.

"Serikali yoyote  duniani, vyama vya siasa, vyama vya kijamii, NGOS na mashirika  hiari ya kijamii na mashirika ya dini ili yafikie  malengo yake kisera, hutegemea kupata msukumo wa nguvu za kitaaluma  na kuungwa mkono na Vyombo vya Habari .

"Tasnia ya Habari inapokuwa huru na waandishi wakiandika kwa uwazi, uhalisia na  ukweli na kutumia kalamu zao kwa weledi na maadili husaidia kuharakisha maendeleo. Ni vigumu kwa sekta ya umma au sekta ninafsi kutimiza shabaha zake unapokosekana Uhuru wa Habari.

"Pamoja na uhuru wao, vyombo vya habari na waandishi wanatakiwa kuzingatia  na kuheshimu sheria za nchi, kufuata maadili, miiko na kanuni za taaluma ya uandishi wa habari unaojenga nchi badala ya kalamu zao kupotosha au kuchochea mifarakano,"amesema Shaka.

Amefafanua CCM kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) Sura ya 06, Fungu la 125, kitaendelea kuzielekeza Serikali zake kuheshimu tasnia ya habari huku wakiwahimiza  waandishi wa habari kuandika habari  zitakazojenga nchi badala ya zile za kulibomoa Taifa

"Chama kitahakikisha uhuru wa vyombo vya habari unaimarishwa na kulindwa, na kwamba wamiliki na wanahabari wanazingatia maadili na weledi katika kazi zao. Chama kinafurahi pale waandishi wa habari wanapoandika kwa kuzingatia weledi katika tasnia yao baada ya kupata habari kutoka vyanzo ama  mamlaka husika na si habari za kuifarakanisha jamii,"amesisitiza.

Aidha amesema CCM inavikumbusha vyombo vya habari  kutambua vina haki na wajibu wa mashambani na Wafanyakazi viwandani na kwamba kalamu zao zisiache kuandika ukweli kuhusu maendeleo  ya kilimo, mifugo, madini, uwekezaji, afya na jamii ya Watanzania, lakini vikosoe na kurekebisha kama kuna haja ya kufanya hivyo.

Pia vyombo vya habari  viendelee kufichua  na kupiga vita vitendo  vya ufisadi, vikemee ubadhirifu  wa mali za umma, wizi na kushamirisha mapambano  dhidi ya adui rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa Umma. 

Shaka amesema Chama hicho kitafanya kila linalowezekana kuimarisha vyombo vya habari vya Chama ili vifikishe habari za kisera na kimaendeleo kwa haraka na kwa uhakika katika jamii. Vyombo vya habari na waandishi wa habari  wana kazi na wajibu wa kueleimisha, kufundisha na kuburudisha jamii. "Kwa muktadha huo CCM inawataka wanahabari  kutimiza majukumu ya kufichua badala ya kuficha  ukweli kwa kuzingatia maadili na miiko ya kisheria iliyopo".

Ameongeza kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza angependa kusikia  habari za kweli zikiwafikia Wananchi kwa haraka mahali popote  walipo mijini au vijijini. 

"Ndiyo maana hivi karibuni aliielekeza Serikali  kuzifungulia TV za mitandaoni na kuwataka wamiliki na wahariri wao kufuata Sheria, kuheshimu maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia Kanuni zake, kama ilivyosisitizwa katika Ilani ya Uchauzi ya CCM,"amesema.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Shaka Hamdu Shaka

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages