Mbio za hisani za Benki ya CRDB zimekuwa na mafanikio makubwa kwa kukusanya shilingi milioni 200 kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo zaidi ya watu 4,000 walishiriki.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizo za hisani zenye lengo la kusaidia jitihada za Serikali katika kutoa huduma bora za afya kwa watoto na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusiana na magonjwa wa moyo kwa watoto.
“Kupata huduma bora za afya ni haki ya kila binadamu, haki ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kila binadamu, hususan watoto wetu na vijana katika kukua vizuri na kuwa na afya njema,” alisema Mama Samia.
Makamu wa Rais pia aliwapongeza washiriki na makampuni yaliyoshiriki kuandaa CRDB Bank Marathon kwa kuungana kwa pamoja kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia upasuaji wa watoto, huku akiwataka watu wote kuendeleza jitihada hizo. “Upo usemi usemao ukiokoa maisha ya mtu umeikokoa dunia, jitihada hizi zisiishie hapa, tuendelee kushirikiana na Taasisi yetu ya Moyo katika kurejesha tabasamu kwa Watoto wetu,” alisisitiza.
Akitoa hotuba yake, katikati ya shangwe na nderemo za mziki, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema mbio hizo za hisani zimefanikiwa kuvuka lengo la kiwango kilicho wekwa cha shilingi milioni 200. Nsekela alisema mbio hizo za hisani zilizokuwa na kauli mbiu ya Kasi Isambazayo Tabasamu zimeweza kuwaunganisha washiriki kwa pamoja kuchangia fedha hizo zinazoelekezwa kwenye upasuaji wa moyo kwa watoto.
Nsekela alisema kwa muda mrefu Benki ya CRDB kupitia sera yake ya kusaidia jamii (CSR Policy) imekuwa ikiisaidia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kufanya upasuaji kwa watoto. Ili kuongeza ushiriki wa jamii kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwamo changamoto ya upatikanaji wa huduma bora afya kwa watoto, Benki ya CRDB imeanzisha mbio hizo za hisani ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka.
“Michezo ina nguvu ya kuwahamasisha watu kushiriki katika mabadiliko chanya. Nifuraha kubwa sana kwetu kuona mbio hizi za hisani za CRDB Bank Marathon zinachochea mabadiliko chanya katika jamii na kuongeza ushiriki wa watu katika kutatua changamoto na kuleta maendeleo.
“….nimefarijika kuona watu wengi wemaungana nasi katika jitihada za kusambaza tabasamu kwa watoto wetu. Mafanikio haya tusingeyafikia isipokuwa kwa kujitoa kwao. Tunawashukuru washiriki wote na makampuni yaliyoshirikiana nasi kuwezesha kufikia lengo,” aliongezea Nsekela.
Naye Waziri wa Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni Dkt. Harison Mwakyembe aliipongeza Benki ya CRDB na wadau walioshiriki katika mbio hizo za hisani kwa mchango wao walioutoa kusaidia upasuaji wa moyo kwa watoto.
“Benki ya CRDB imeonyesha sio tu ni bora kwa kutoa huduma bora kwa wateja, lakini pia ipo mstari wa mbele katika kusaidia jamii kwasababu uongozi wa benki hii unaelewa taifa lolote lenye mafanikio ni lazima kuwekeza katika afya ya watoto,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe alisema Benki ya CRDB imedhihirisha kuwa wapo Watanzania ambao wanauwezo wa kuongoza taasisi kubwa nchini na kwa mafanikio makubwa huku akibainisha kuwa miaka ya nyuma mabenki mengi yalikuwa yakiendeshwa na watu kutoka nje.
No comments:
Post a Comment