Na Khalfan Akida - DODOMA.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako leo Juni 17 ametangaza ratiba ya Masomo na mitihani kwa ajili ya kukamilisha mwaka wa Masomo wa 2020 ikiwa ni takribani saa 24 kupita toka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufi kutangaza rasmi kufungua Shule zote zilizokua zimefungwa kutokana na janga la Corona.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ndalichako amesema muhula wa kwanza wa masomo utamalizika Agosti 28 mwaka huu na kuanza kwa muhula mpya utakaoishia Desemba 18 mwaka huu.
Aidha Waziri huyo wa Elimu Nchini amesema ili kukamilisha muhtasari wa Masomo Shule zitalazimika kufundisha kwa masaa mawili zaidi ya muda wa kawaida wa Mwalimu kufundisha darasani kila siku ili kufidia muda uliopotea ambapo ameongeza kuwa maelekezo ya kuongeza muda huo yatawahusu wanafunzi wa madarasa ya awali pia.
Ameongeza kuwa kutokana na janga la Corona lilivyokuwa na kutikisa hali za kiuchumi za wananchi anazishauri Shule binafsi kutumia busara kwa kukaa na Bodi za Shule ili kwa pamoja kuangalia njia nzuri ya ulipwaji wa ada utakaowasaidia wazazi kuweza kulipa bila ya kuwepo kwa malalamiko yoyote.
"Hili la ada nishauri tu Bodi za shule zikae na wazazi na kuangalia ulipaji wa ada bila kuumizana. Lakini nishauri tu kwamba kama Mzazi hajalipa ada ya awamu ya kwanza basi ni vema ailipe lakini pia hautokua uzalendo kama shule zitakataa kuwapokea watoto wa kitanzania kisa tu hajalipa ada," Amesema Prof Ndalichako.
Kuhusu mihula ya Masomo kwa wanafunzi wa Kidato Cha tano Waziri Ndalichako amesema wataripoti shuleni Juni 29 kama ilivyotangazwa na Mh Rais na wataanza Masomo yao kwa kukamilisha muhtasari wa kidato cha tano na mitihani itafanyika Julai 24 na kuanza Masomo yao ya Kidato cha sita Julai 27 mwaka huu.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ametangaza ratiba za mitihani ambapo mitihani ya Kidato cha Nne itaanza Novemba 23 hadi Desemba 11, Kidato cha Pili itaanza Novemba 9 hadi 20, Darasa la Saba Oktoba 7-8 na Darasa la Nne Novemba 9 hadi 20 mwaka huu, huku akiagiza Shule zote kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya katika kujikinga na ugonjwa wa Corona wawapo Mashuleni
No comments:
Post a Comment