A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, June 18, 2020

MMILIKI WA HOTELI YA FORODHANI STONE TOWN ZANZIBAR KUSHIKILIWA KWA KUTOLIPA STAHIKI ZA WAFANYAKAZI.




Na: Salum Humud Salum - ZANZIBAR



Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mheshmiwa Hassan Khatib Hassan ameagiza kushikiliwa kwa mmiliki wa hoteli ya Forodhani Stone Town Michael Jaffar hadi atakapokamilisha taratibu za malipo ya mishahara ya  wafanyakazi wa hoteli hiyo.


Mhe. Hassan amefikia uamuzi huo katika kikao cha pamoja kilichoshirikisha wajumbe kutoka Kamisheni ya kazi, Idara ya uhamiaji na Kamisheni ya utalii kufuatia malalamiko ya wafanyakazi wa hoteli hiyo.


Amesema serikali ya Mkoa imechukua uamuzi huo kutokana na mmiliki wa hoteli kukosa uaminifu na kufanya udanganyifu katika malipo ya mishahara na stahiki nyengine za wafanyakazi hao.


“Amekuwa akitafutwa kwa siku nyingi baada ya kupata malalamiko ya wafanyakazi wa hapa na baada ya kufanya mawasilianao na kamisheni ya kazi ndipo tukafikia uamuzi kuwa hati yake ya kusafiria izuiwe baada ya mwananchi mmoja kutupa taarifa za mahali  alipo,” alisema Mhe. Hassan.


Aidha Mhe. Hassan amesema serikali  ya mkoa huo haitavumilia kuona baadhi ya waajiri wanakosa uaminifu na kuwanyanyasa wafanyakazi wao kwa kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kutowalipa mshahara kwa wakati.
“Tulipofatilia tumemuona ndugu yetu huyu amechukua siku nyingi hajawalipa wafanyakazi na uongozi wa hoteli mishahara yao hatua ambayo ni kinyume na utaratibu wa sheria za kazi lakini pia ana deni la gari alilokodishwa na mambo mengine mengi,” alisema Mhe. Hassan.


Hata hivyo Mkuu wa mkoa amewataka wamiliki wa mahoteli mbali mbali katika mkoa huo kuendelea kuitumia vyema fursa ya uwekezaji kwa kufuata taratibu na sheria za nchi sambamba na kuheshimu haki za wafanyakazi wao.

Wakizungumza baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo, waliiomba serikali kuendelea kuwasaidia kudai haki yao kwani wamekuwa wakidai kwa kipindi kirefu na mmiliki kutoonesha dalili ya kuwalipa na kupelekea kuwaongezea ukali wa maisha.
“Sisi wafanyakazi tumaini letu pekee liko kwako, maana tunaishi katika mazingira magumu kwani tunadaiwa kodi ya nyumba lakini hata pesa za matumizi hatuna,” alieleza mmoja ya wafanyakazi hao.


Mapema Afisa kutoka kamisheni ya kazi Zanzibar Makame Jecha amesema pamoja na jitihada zilizochukuliwa na taasisi yake, ikiwemo kuiandikia barua Idara ya uhamiaji kuiomba kuzuwia hati ya kusafiria ya mmiliki huyo wamegundua kuwa tatizo alilonalo ni kutokuwa mkweli kulipa fedha hizo.


“Tangu tulipopokea kesi hii tumegundua tatizo kubwa alilonalo mmiliki wa hoteli hii ni kukiuka makubaliano tunayokubaliana nae lakini pia tumetafuta watu wake wa karibu kuwambia tatizo hili wanakataa kutoa ushirikiano na kutueleza kuwa huyu jamaa ni mkorofi,” alisema Makame.


Zaidi ya shilingi milioni 35 zinadaiwa na wafanyakazi 12 wa hoteli hiyo kwa ajili ya mishahara ya Zaidi ya miezi minne na gharama nyengine za kuendeshea biashara ya hoteli hiyo.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages