A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Friday, September 27, 2019

TBS Yashiriki Mikutano Ya Mashauriano, Yatoa Elimu

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara uliofanyika Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wawezeshaji (hawapo pichani). Lengo la mikutano hiyo iliyofanyika mikoa ya kusini ya Ruvuma, Mtwara na Lindi kuanzia Septemba 24 hadi jana Septemba 26, mwaka huu ilikuwa ni kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji kwa lengo la kutatua changamoto hizo. Miongoni mwa waliotoa mada ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf Ngenya. Na na Chalila Chbuda


Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kuhusu fursa wanazopata wafanyabiashara na wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi viwango, kuhamasisha wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure pamoja na kuzipatia majibu changamoto wanazokumbana wadau wake mbalimbali.

Shirika hilo limetoa elimu hiyo wakati wa mikutano ya mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kwa ajili ya kusikiliza changamoto zinazowakabili kwenye mikoa ya Kusini ambayo ni Ruvuma, Mtwara na Lindi kuanzia Septemba 24, mwaka huu. Mikutano hiyo ilimalizika jana mkoani Lindi.

Ufunguzi wa mkutano Songea, ulifanyika chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Ndeme na kuhudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjelina Mabula, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya  Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  Mussa Sima, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Anjellah Kairuki na wakuu wa wilaya zote.

Akitoa mada kwa nyakati tofauti kwenye mikutano hiyo, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, aliwaeleza washiriki hao kuhusiana na mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo yameleta mabadiliko katika Sheria ya Viwango Na: 2 ya mwaka 2009.

Kufuatia mabadiliko hayo, Dkt. Ngenya alisema shirika hilo kwa sasa inatekeleza baadhi ya majukumu ambayo awali yalikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambayo kwa sasa inajulikana kama TMDA.

Alisema kufuatia mabadiliko hayo majukumu ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi yanafanywa na TBS. 

Akieleza fursa zinazotolewa na shirika hilo kwa wajasiriamali nchini, Dkt. Ngenya, alisema ni pamoja kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha bila malipo kwa miaka mitatu lengo likiwa ni kuwawezesha kupanua soko la bidhaa zao na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara. 

Alisema Serikali imeanzisha utaratibu huo ili kuwasaidia
wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Alitoa wito kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla 
kuichangamkia fursa hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inasisitiza uchumi wa viwanda.

“TBS kama taasisi wezeshi inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa bure kwa wajasiriamali wadogo na wakati, lengo likiwa ni kuendeleza viwanda vya Tanzania, hivyo ni vyema wakathibitisha ubora wa bidhaa zao ili wasipate vikwazo vyovyote katika kupata soko ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Ngenya.

Alisema kuwa endapo wajasiriamali hao watathibitisha bidhaa zao
itawasaidia kuzalisha bidhaa endelevu ambazo zitakuwa na soko kila
mahali ikiwemo masoko ya kikanda.

Dkt. Ngenya, alifafanua kuwa lengo la TBS ni kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa, bila kuathiri taratibu na sheria za nchi. Kutokana na umuhimu huo, alisema ndiyo maana shirika hilo limeshiriki mikutano hiyo kama taasisi wezeshi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages