A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Saturday, June 29, 2019

SERIKALI YAPOKEA MADINI YENYE THAMANI YA MABILIONI YA FEDHA

JUMLA ya madini yenye thamani ya Sh.3,125, 704,456.12 yamekabidhiwa kwa Serikali kupitia Hazina baada ya kutaifishwa kutokana na kubainika yalikuwa yanatoroshwa nchini.

Mbali na kukabidhiwa madini na vito, pia Serikali imekabidhiwa fedha za kigeni ambazo nazo zimetaifishwa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madini, vito na fedha hizo kwa Katibu Mkuu Hazina Dotto James, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga amefananua kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) katika vipindi tofauti kati ya mwaka 2017 na mwaka 2018 imeendesha kesi mbalimbali.

Amesema kesi hizo zilikuwa zinahusiasana na utoroshaji au kukutwa na madini bila kuwa na kibali na katika uendeshaji wa kesi hizo washtakwa walitiwa hatiani na kuamriwa kulipa faini au kutumikia kifungo gerezani pamoja na amri ya kutaifishwa madini na fedha walizokutwa nazo wakati wakisafirisha madini hayo.

"Madini yaliyotaifishwa ni kilo 25.546 za dhahabu ,zaidi ya kilo 76,020.20(tani 76) za Colored gemstone, Tanzanite pamoja na fedha za kigeni za mataifa mbalimbali 15 zenye thamani ya Sh.1,023,608, 515.12.

"Kwa kuwa madini hayo yametunzwa sehemu mbalimbali kiasi kwamba uwezekano wa kupotea au kumbukumbu zake kupotea na kwa kuwa mali zote zinazotaifishwa zinakuwa mali za Serikali na Katibu Mkuu Hazina ndiye msimamizi wa mali hizo" ameeleza.

"Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anakabidhi kilo 25.5 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 913,954.72 sawa na Sh.bilioni 2,102,095,941,"amesema Mganga.

Akifafanua madini na vito, amesema kuna tani 76 na Carrats 2849 zenye thamani ya Dola za Marekani 2,638,349.95 sawa na Sh.bilioni 6,068,204.885 na Carrats 2,849 zenye thamani ya Dola za Marekani 3,803.32 sawa na Sh. milioni 888,409,000.

Pia Tanzanite gramu 888 zenye thamani ya Dola 3,197 sawa na Sh.bilioni 7,353,348 na fedha za kigeni za mataifa 15 ambazo ni sawa na Sh.1,023,608,515.12.

Hata hivyo Mganga baada ya kukabidhi madini hayo na fedha kwa Katibu Mkuu Hazina ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa watumishi wa madini ambao wanashindwa kutoa taarifa kwa wakati kuhusu madini na kuwataka kufanya hivyo ili awe nafasi ya kufuatilia na kuchukua hatua mapema.

Akizungumza baada ya kukadhiwa madini na fedha hizo, Katibu Mkuu Hazina Dotto James amewahakikishia Watanzania wote kuwa mali yao iko salama na itatumika kufanya maendeleo kulingana na uamuzi wa Serikali kuhusu mali hizo.

"Tunaamini Benki Kuu ya Tanzania(BoT) itatunza mali hizi bila wasiwasi wowote kama ambavyo wamekuwa wakitunza kwa siku zote na pale ambapo Serikali itaamua namna ya kuzitumia kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi wake basi itazichukua,"amesema James.

Wakati huo huo Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema inasikitisha kuona watu wasiokuwa na nia njema wakitorosha madini wakati wananchi wakiendelea kuteseka."Kwa kweli inasikitisha sana kuona watu wanaendelea kutorosha madini wakati wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.Bungeni wabunge kila siku wanalalamika maji! maji! halafu kuna watu wanatorosha madini." ameeleza.

"Ni aibu Waziri wa Fedha kuendelea kuomba misaada wakati mali tunazo za kutosha...tena misaada mingine masharti yake ni magumu. Nitoe rai kwa Watanzania tuwe macho na wote ambao wanatabia ya kupora mali zetu na kuzitorosha,"amesema Waziri Mpango.

Waziri wa Madini Dotto Biteko ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa wote ambao wamefanikisha kupatikana kwa madini na fedha hizo huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuwa wachimbaji madini ambao wenye tabia ya wizi wa kutosha madini watambue kwa sasa hawana nafasi tena.

Pia amesema kuna baadhi ya watanzania ambao wamekuwa wakifanya utapeli kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii kwa kujifanya wana madini na kisha kuchukua fedha za raia wa mataifa mengine, ambapo amesema wenye tabia hiyo wajue siku zao zinahesabika kwani Serikali haiko tayari kuendelea kuwavumilia wenye tabia hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augustino Mahiga amesema Tanzania kuna madini mengi ambayo hayawezi kuisha leo wala kesho na vema Watanzania wakawa macho kwa kuhakikisha madini hayo yanatunzwa kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwa niaba ya Serikali sehemu ya vipande vya Madini ya Dhahabu ambayo ilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt.Agustine Mahiga, Waziri wa Madini Dotto Biteko pamoja na Kamishina wa Madini Profesa Abdukalim Mruma wakiwa wamishika vipande vya madini ya dhahabu ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga amezikabidhi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwa niaba ya Serikali Madini, vito na Fedha za mataifa mbalimbali zilizokamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga akionyesha juu kwa Mawaziri na Wanahabari Fedha za Kimarekani (Dollar) kabla ya kumkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwa niaba ya Serikali Fedha hizo pamoja na Madini na Vito ambavyo vilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwa niaba ya Serikali sehemu ya Fedha za Mataifa mbalimbali pamoja na Madini na Vito ambavyo vilikamatwa na kutaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James akikagua sehemu ya fedha za mataifa mbalimbali mara baada ya kukabidhiwa kwa niaba ya Serikali Fedha na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga amabazo zilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini vikiwemo pia Madini na vito mbalimbali, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga akionyesha juu kwa Mawaziri na Wanahabari moja kipande cha madini ya Pie light kabla ya kumkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James kwa niaba ya Serikali Madini, Vito na Fedha za mataifa mbalimbali ambavyo vilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 

Masanduku yaliyoifadhiwa Madini,Vito pamoja na fedha za Mataifa mbalimbali zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi zikiingizwa Ukumbini tayari kwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) Biswalo Mganga kukabidhi kwa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT). 
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dotto James akizungumza na wanahabari mara baada ya kukabidhiwa kwa niaba ya Serikali Madini, vito mbalimbali na Fedha kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga ambazo zilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt.Agustine Mahiga akizungumza na wanahabari katika hafla ya kukabidhi Madini, vito mbalimbali na Fedha kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga ambazo zilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 
Waziri wa Madini Dotto Biteko akizungumza na wanahabari katika hafla ya kukabidhi Madini, vito mbalimbali na Fedha kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Biswalo Mganga ambazo zilikamatwa na kuitaifishwa kwa mujibu wa Sheria zilizotokana na Kesi mbalimbali za Uhujumu Uchumi nchini, katika ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam Juni 29, 2019 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages