A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Thursday, February 7, 2019

Makamu wa pili wa Rais afanya mazungumzo na Rais wa mazingira UN


Na. Thabit Madai.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefanya mazungumzo na Rais wa Taasisi inayosimamia mazingira ya Umoja wa Mataifa Bwana Siim Valmar Kiislar katika Ofisi yake iliyomo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi liliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Rais wa Taasisi hiyo amesema wakati umefika kwa Mataifa yote Ulimwenguni kuwa na mfumo Mmoja unaoeleweka wa utunzaji wa Mazingira utakaosaidia kuifanya Dunia iendelee kubakia salama.

Alisema tabia ya baadhi ya Mataifa kuendelea kukwepa mikataba na baadhi ya kanuni zinazowekwa Kimataifa pamoja na kuweka vikwazo vyenye nia ya kulinda maslahi yao binafsi vitapelekea kuongezeka kwa wasi wasi utakaoifanya Dunia hii ibakie katika mazingira hatarishi.

Rais huyo akiongoza Ujumbe mzito wa Taasisi hiyo amekuja kushuhudia uzinduzi wa Kampeni ya Kidunia ya uzinduzi wa usafi wa Mazingira katika Fukwe ya Forodhani Visiwani Zanzibar ulioambatana na ujio la Mashua ya Mazingira iliyotengenezwa kutokana na malighafi ya Plastiki kutoka Nchini Kenya.

Bwana Siim Valmar ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wananchi wake kwa umakini wao wa kusimamia masuala ya Mazingia katika kuitikia kampeni ya Kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya Tabia Nchi.

Alisema kitendo cha Zanzibar kufanikiwa katika mapambano yake ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya Plastiki mbali ya kuwa mfano kwa Mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika, lakini pia kimeleta faraja kwa Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi yake hiyo  inayosimamia masuala ya Mazingira.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar bado inaendelea kuathirika na mabadiliko ya Tabia Nchi akatolea mfano ufukwe wa Bahari ya Msuka uliopo kaskazini mwa Kisiwa cha Pemba ambao tayari umeshaliwa na mawimbi ya Bahari kwa sehemu kubwa.

Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo wa Taasisi ya Umoja wa Mataifa unaosimamia Mazingira kwamba Zanzibar imeanza mikakati ya kupiga marufuku matumizi na uingizwaji wa Mifuko ya Plastiki tokea mwanzoni mwa Miaka ya 90 na kufanikiwa vyema katika azma yake ya kulinda mazingira.

Alisema ujio wa mashua ya Mazingira katika Visiwa vya Unguja na Pemba utasaidia mfano wa Darasa kwa Wananchi waliowengi kuwa na muelekeo wa jitihada za mapambano dhidi ya mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumbwa Dunia hivi sasa na kuleta athari kubwa ya Kimazingira.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages