DAR ES SALAAM: Kamwene
Lulu! Ndivyo unavyoweza kumsalimia mwanadada mrembo kutoka kiwanda cha
Bongo Muvi, Elizabeth Michael ‘Lulu’ ukikutana naye baada ya kuvunja
rekodi iliyowahi kuwekwa na mwanamama mjasiriamali kutoka Uganda,
Zarinah Hassan ‘Zari The Bosslady’ ambaye ni mzazi mwenza wa staa wa
Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
KAMWENE NI NINI?
Kamwene ni salamu inayotokana na kabila la Wahehe kutoka mkoani
Iringa inayomaanisha hujambo? Salamu hii imejichukulia umaarufu mkubwa
hivi karibuni baada ya kutumika katika sherehe za utoaji Tuzo za Sinema
Zetu za Kimataifa za Sziff zilizofanyika wikiendi iliyopita kwenye
Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar ambapo watoto wawili, Flora Kihombo
(11) na Rashid Msigalla (10) waliotwaa tuzo hizo walisikika wakisalimia
mashabiki “KAMWENE”!
TURUDI KWA LULU
Katika usiku huo wa tuzo, Lulu alikuwa mshereheshaji mkuu ‘MC’
sambamba na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Azam, Baruani
Muhuza. Katika tukio hilo, Lulu aliweka rekodi ya ulinzi mkali kwa
kulindwa na msafara ambao hakuna staa yeyote Bongo aliyewahi kufanyiwa
hivyo kwani hata ule wa Zari haukufikia kiwango hicho.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia msafara wa Lulu ambao ulianzia maeno
ya Kijitonyama katika Jengo la Millenium Tower jijini Dar, staa huyo
alivalia gauni jekundu ambapo muda mwingi hakutaka mtu wa pembeni
alishike zaidi yake huku nje ya jengo hilo magari ya kifahari
yakimsubiri likiwemo Range Rover Sport ambalo alilitumia kumbeba.
“Tulijua huenda anatengeneza filamu mwanzoni wakati anapodolewa,
kumbe alikuwa akifanya kweli. Mabodigadi walioshiba wawili walikuwa
wakimlinda kila kona, kuanzia anapambwa hadi anatoka katika jengo hilo.
Kifupi walikuwa hawachezi mbali mpaka anaingia kwenye gari huku
wakipeana zamu ya kufungua milango na kufunga,” kilisema chanzo.
ULINZI WAKE WASHTUA WENGI
Baada ya kutoka katika jengo hilo ambalo ilikuwa hatua yake ya kwanza
kujiremba, Lulu aliongozana na magari hayo ya kifahari yasiyopungua
matano pamoja na king’ora cha pikipiki ya Polisi, zote zikiwasha taa
mithili ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au kiongozi mkubwa anapita.
“Barabara nzima kutoka Kijitonyama kwa kutumia Barabara ya Ali Hassan
Mwinyi kisha kukata Mwenge na kuingia Barabara ya Sam Nujoma, magari
yalikuwa yakipisha hivyo kushtua watu walioshuhudia msafara huo uliojaa
mbwembwe kama zote. Hadi wanaingia Mlimani City, bado kuna wengine
walikuwa hawaamini anayeongozwa na msafara huo kama ni Lulu au ni
kiongozi mkubwa wa nchi.
MASTAA WAPIGWA NA BUTWAA
Baadhi ya mastaa ambao walikuwa wameshatangulia ukumbini hapo
kushuhudia utoaji tuzo hizo walipigwa na butwaa baada ya kumuona Lulu
akifunguliwa mlango na mabaunsa kisha kumsindikiza hadi ndani kwa ajili
ya kuvaa nguo nyingine. “Si vizuri kuwataja, lakini ni hawa mastaa
wenzake wakubwa tu wanaofanya naye filamu. Hawakuamini kwa jinsi
alivyoshuka kwa ulinzi mkali,” kilimaliza kudokeza chanzo ambacho ni
mmoja wa watu waliokuwa wakifuatilia kwa karibu tukio hilo la Lulu.
ANAVUNJAJE REKODI YA ZARI?
Oktoba, 2017, Zari akiwa katika uhusiano na Diamond alipata mualiko
wa kwenda kufungua duka jipya la Danube lililopo ndani ya Mlimani City
jijini Dar.
Katika siku hiyo inayoaminika ilikuwa rekodi mpya Bongo, mbwembwe
zilikuwa za kutosha kutokana na watu wengi kujazana katika jengo hilo
huku wengine wakimzingira Zari na kulitaja jina la wifi. Hata hivyo,
Lulu anatajwa kuvunja rekodi hiyo baada ya kumzidi Zari kwa idadi ya
magari ya kifahari na ulinzi mkali wa Polisi na mabaunsa.
STORI: Andrew Carlos, Risasi Mchanganyiko
No comments:
Post a Comment