Meneja Mradi wa Legal Services Facility LSF, Ramadhan Masele (kushoto), akizungumza na wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba wakati wa kikao chakujadili namna
watakavyoweza kushirikiana na serikali namna ya kuboresha na kurahisisha
upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi hafla hiyo imefanyika jana jijini Dodoma.
Meneja Mradi wa Legal Services Facility LSF, Ramadhan Masele, akizungumza wakati wa hafla
hiyo.
Wabunge Tanzania wameombwa kuunga mkono kazi za wasaidizi wa
kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria, ambao ni nguzo muhimu katika
kuwasaidia mamilioni ya Watanzania kutoka katika vitendo vya kikatili,
manyanyaso na udhalimu.
“Ni kweli kwamba wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada
wa kisheria wengine wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaoteswa na
kunyayaswa, lakini hawawezi kazi hii kwa ufanisi bila kusaidiwa au kuungwa
mkono na watu kama vile wabunge,” Ramadhani Masele, Meneja wa Programu wa
Taasisi ya Msaada wa Kisheria (LSF) wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya
siku mbili kwa wabunge kuhusu wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za kisheria
nchini, uliofanyika Dodoma jana.
LSF ni shirika lisilokuwa la kiserikali lilioanzishwa Mwaka
2011, linalofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark
(DANIDA) na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID). LSF inatoa
fedha kwa mashirika mbalimbali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za
wasaidizi wa kisheria Tanzania Bara na Zanzibar.
Lengo kuu la semina ya wabunge, ni kuwawezesha wabunge kujua
masuala mbalimbali, ikiwemo namna wasaidizi wa kisheria wanavyotoa huduma zao,
idadi ya wilaya wanazofanya kazi, na aina ya kesi wanazozishughulikia, msaada
wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria, kazi za LSF na ushiriki wake
katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 17 ya Umoja wa Mataifana
Semina hii ya mafunzo inakuja wakati kuna ongezeko la matukio ya
uvunjaji wa haki za binadamu nchini, kama vile watu kuteswa, ukatili wa
kijinsia, udhalilishaji wa kijinsia, kuwashambuliwa wanawake kwa kuwapiga,
uporaji wa ardhi na matukio mengine yanayofanana na hayo.
Kwa kupatia ufadhili kutoka LSF, wasaidizi wa kisheria na watoa
msaada wa kisheria wameweza kuwasaidia wanawake, wanaume na wasichana maskini
na makundi ya watu wengine wananyimwa haki zao, kupata huduma za kisheria kwa
gharama nafuu au bila gharama yoyote na huduma bora za msaada wa kisheria na
hivyo kupata haki zao, kwa mujibu wa meneja Mpango wa LSF.
“Lakini wasaidizi wa kisheria na watoa msaada wa kisheria
wengine wangeweza kutoa huduma na kuwafikia watu wengi zaidi ambao haki
zimeminywa au kuvunjwa kama wakiungwa mkono na wabunge,” aliongeza Masele, huku
akisema kwamba “wanawake na wanaume wanaoteswa, kudhalilishwa au
kufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambao haki zao za ardhi na mirathi zimevunjwa,
wanaishi katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wenyewe.”
Pamoja na mambo mengine, alisema semina ya mafunzo itawasaidia
wabunge kufahamu masuala yanayohusu wasaidizi wa kisheria, jinsi wanavyofanya
shughuli zao na jinsi gani wasaidizi wa kisheria wanavyoweza kushirikiana na
wabunge kupanua wigo wa huduma za msaada wa kisheria.
“Lengo kuu kuwasaidia watanzania wengi wanaohitaji msaada wa
kisheria na kupata haki zao zilizokiukwa. Ni muhimu kwa wabunge kuungana na
wasaidizi wa kisheria kwa sababu wananchi wenye matatizo wanatoka katika
majimbo yanayoongozwa na wabunge,” alisisitiza Masele.
Kwa mujibu wa maelezo ya LSF, semina hii itawawezesha wa bunge
kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na wasaidizi wa kisheria, ambao kwa sasa
wanafanya kazi katika wilaya 170 nchini, namna ya kuwasiliana nao, namna ya
kupata huduma zao na kueneza taarifa za huduma zao majimboni kwao.
“Taarifa muhimu kama hizi zitarahisha kazi za wabunge na
wasaidizi wa kisheria katika kutatua matatizo/kero mbalimbali za wananchi
katika majimbo yao—migogoro ya ardhi, ndoa na mimba za utotoni, mirathi,
wanaume kutelekeza familia zao nk,” inasema sehemu ya taarifaya LSF.
Mada za kimkakati zilitolewa na wataalamu wa LSF kwenye semina
iliyohudhuriwa na wabunge kutoka Kamati ya Kudumuya Bunge ya Katiba na Sheria
na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii.
No comments:
Post a Comment