Serikali
imesema inajiandaa kuupokea mradi wa ‘Global Learning XPRIZE’
unaowawezesha watoto walio nje ya mfumo rasmi kujifunza stadi za msingi
za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kupitia Michezo iliyowekwa kwenye
tableti, kutoka kwa wadau wanaoufadhili baada ya kumalizika muda wa
majaribio. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka TAMISEMI
anayeshughulikia elimu nje ya mfumo rasmi na Elimu ya Watu Wazima,
Odilia Mushi wakati akizungumza katika mkutano uliokutanisha wadau
mbalimbali ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO), na taasisi mbalimbali za serikali.
“Kama
serikali mradi unapomalizika tunaangalia namna ya kuuendeleza.
Tutaendelea kushirikiana na halmashauri zetu zilizoko kwenye mradi
wauone kama ni wa kwao na kwamba badala ya watoto kuzurura mitaani
wanaendelea kujifunza,” amesema Mushi na kuongeza. “Tunaagiza wale
wahusika, wadau wa elimu katika ngazi zote za kijiji hadi mkoa wa Tanga
waone kama hiki kilicholetwa kwetu ni zawadi,na ni lazima kuuendeleza
ili kupunguza watoto walioko nje ya mfumo rasmi; kwa maana hiyo
inatakiwa tuwe na ushirikiano kuona changamoto baada ya huu mradi
kumalizika ili kuzifanyia kazi.”
Akielezea
utekelezaji wa mradi huo tangu ulipoanza na ulipofikia, Afisa Msaidizi
wa Mradi kutoka UNESCO, amesema hadi sasa watoto zaidi ya 2000 kutoka
vitongoji 141 katika wilaya 6 za mkoa wa Tanga wamenufaika na mradi huo.
“Baada ya miezi 15 ya mradi kukamilika, mradi utakabidhiwa kwa serikali
ili kuendelea kuusimamia, ambapo tumekutana leo Tarehe 13/3/2018 na
wawakilishi kutoka Baraza la Mitihani la Tanzania (BMT) , Taasisi ya
Elimu Tanzania (TET) na TAMISEMI ili kuweza kuangalia ni jinsi gani
watoto walio katika mradi wataingia katika mfumo rasmi katika ngazi
husika,” amesema.

No comments:
Post a Comment