Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) imetangaza kuzipiga mnada mali za
wadaiwa sugu 7,065 watakaoshindwa kulipa madeni yao ndani ya siku saba
kuanzia jana.
Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo, Beng’i Issa alisema jana Machi 6
kwamba uamuzi huo ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la mikopo
chechefu au isiyolipika iliayo.
“Mpaka sasa mikopo isiyolipika imefia Sh7.9 bilioni hivyo kuongeza ugumu
kidogo katika kuhakikisha tunapata mtaji wa kutosha,” alisema Issa.
Ndani ya muda walioutoa, alisema wateja wanaodaiwa wanapaswa kulipa
madeni yao ambayo ni ya muda mrefu, “Wengi wameshapitiliza siku 90 za
kutorejesha madeni yao kinyume na utaratibu na makubaliano na benki,”
alisema
Kwa watakaoshindwa kulipa fedha hizo ndani ya muda uliotolewa wa benki
kuchukua hatua za kisheria kabla ya kunadisha dhamana zao, amesema wenye
dhamira ya kulipa waende kwenye tawi lolote la benki hiyo wakiwa na
mpango mahususi wa jinsi watakavyofanikisha malipo yao.
Januari 4, wakati Benki Kuu Tanzania (BoT) inatangaza kufuta leseni za
baadhi ya benki nchini, TWB ilipewa agizo la kuongeza mtaji ndani ya
miezi sita ili kukidhi mahitaji ya ukwasi unaohitajika.
Kulingana na masharti ya taasisi za fedha na benki za biashara nchini,
kila moja inatakiwa kuwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi mahitaji
ya kila siku.
Wakati TWB ikipewa onyo hilo, benki za Covenant, Efatha, Benki ya
Wananchi Njombe, Kagera Farmer’s Cooperative Bank na Benki ya Wananchi
Meru zilifutiwa leseni.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania, Japhet Justine
amesema sheria inawaruhusu kuuza mali au dhamana za wateja walizoweka
endapo watashindwa kurejesha mkopo kwa wakati waliokubaliana.
“Mbali na kupiga mnada mali zao, taarifa zao tutazipeleka Benki Kuu ya
Tanzania wasiweze kupata mkopo katika benki nyingine yoyote nchini,”
alisema Justine.
Alisema tangu kutolewa kwa taarifa ya awali kuwa benki ipo katika hali
mbaya, wamekusanya zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa wadaiwa walionao,
hatua ambayo alisema ni nzuri.
Kwa sasa, alisema wapo katika maongezi na wadau mbalimbali kuwawezesha
kupata mtaji waliowekewa na Benki Kuu na kwamba mwelekeo unaonekana kuwa
mzuri.
“Baada ya benki yetu kupewa maagizo ya kuongeza mtaji na Benki Kuu
tunapokea wateja na wageni wengi wanaohitaji ufafanuzi kuhusu fedha zao
lakini wote wanaelewa,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment