Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora akifungua mkutano
wa wadau wa Utekelezaji wa Mradi wa Maji Simuyu. Mradi huo mkubwa uko
katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kutekelezwa. Kushoto ni Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Eng. Emmanuel Kalobelo.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Eng. Emmanuel Kalobelo
akifunga kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora.
Katibu
Mkuu Prof. Faustin Kamuzora (watatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya
pamoja na washiriki wa kikao kazi wanaohusika na utekelezaji wa Mradi
wa maji wa Simiyu mara baada ya ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika
katika Ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Na Yusuph Mlandula
Serikali
ya Tanzania kupitia Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate
Fund) imepata fedha za kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa
Victoria hadi Mkoa wa Simiyu ambapo fedha za Mradi huo zitapitia Benki
ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Hayo
yamesemwa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin
Kamuzora wakati wa kikao kazi kilichojumuisha wadau wanaohusika na
utekelezaji wa Mradi wa maji wa Simiyu, mradi unaofadhiliwa na Mfuko wa
mabadiliko ya tabianchi ambapo imebainika kuwa utekelezaji wake utaanza
mara moja.
Aidha,
Prof. Kamuzora amesema kuwa fedha hizo zinapitia Benki ya Maendeleo ya
Ujerumani kutokana na sababu kwamba Serikali ya Ujerumani imekua
ikifadhili miradi mbalimbali ya maji hapa nchini. “Ili kupata fedha
kutoka katika mfuko huu ni lazima zipite kwenye taasisi ambayo
imethibitishwa “accredited entity”alisisitiza Profesa Kamuzora.
Prof.
Kamuzora amesema kuwa huu ni mradi mkubwa sana na wenye manufaa kwa
wakazi wa Simiyu ambapo Mfuko wa Mabadiliko ya tabianchi umetoa kiasi
cha 102,700,000 EURO, Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) itachangia
25,900,000 EURO na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itagharamia kiasi cha 13,100,000 EURO. Vilevile jamii inayozunguka mradi
itachangia kiasi cha 1,500,000EURO, hivyo mradi wote unatarajiwa
kugharimu kiasi cha EURO 143,000,000 na utatekelezwa ndani ya kipindi
cha miaka mitano.
Mradi
huo pia una lengo la kuimarisha afya za wakazi hao, kuhimiza uzalishaji
endelevu na maendeleo ya jamii inayozunguka kwa kuwapatia maji safi na
salama kwa miji na vijiji ambapo mradi utapita pamoja na kuhimili
mabadiliko ya tabianchi hususan kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu.
Akitoa
maelezo ya awali juu ya Mradi huo Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi
ya Makamu wa Rais na Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabia Nchi
anayeiwakilisha Afrika Bw. Richard Muyungi, amesema kuwa ni mradi
mkubwa sana na wa kwanza duniani kupatiwa fedha kupitia mfuko huo ambazo
si mkopo. “Ni fedha zisizo za mkopo, ni msaada hivyo katika awamu ya
kwanza takriban watu 395,000 katika Wilaya ya Busega, Bariadi na Itilima
watanufaika na mradi huo”
Kupatikana
kwa mradi huu na utekelezaji wake utasaidia sana changamoto zitokanazo
kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ukame
uliokithiri na utasaidia kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi
katika Wilaya husika.
Kikao
cha Wadau cha kujadili utekelezaji wa Mradi wa maji wa Simiyu,
kimeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambao ni Wasimamizi wa Fedha za
Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi hapa nchini na wanadhamana ya
kuhakikisaha fedha za Mfuko huo zinatumika ipasavyo ikiwa ni pamoja na
kuendana na mipango nchi iliyojiwekea.
No comments:
Post a Comment