Katika
kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi, Ubalozi wa Tanzania kwa
kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi uliopo Tanzania, Wizara ya Masuala
ya Uchumi na Wizara ya Mambo ya Nje za Uholanzi na Taasisi ya
Netherlands–African Business Council (NABC)kwa pamoja ziliandaa
Kongamano la Biashara na Uwekezaji lililofanyika hapa The Hague,
Uholanzi tarehe 31 Mei 2017.
Lengo
kuu la Kongamamo hilo, pamoja na kuendeleza na kukuza uhusiano mzuri
uliopo kati ya Tanzania na Uholanzi, nikutangaza fursa mbalimbali za
biashara na uwekezaji zilizopo nchini Tanzania hususan katika Sekta za
Kilimo, Ufugaji, Uvuvi na Miundombinu ya Kilimo.
Aidha,
Kongamano hilo lililohudhuriwa na Wawakilishi wa Makampuni takriban mia
moja (100) ni mwendelezo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa
kwenye Mkataba kati ya Tanzania na Uholanzi kuhusu Uingizwaji wa Mbegu
za Viazi kutoka Uholanzi uliosainiwa kwenye ziara ya Mhe. Martijn Van
Dam, Waziri wa Kilimo wa Uholanzi nchini Tanzania tarehe 16 Juni 2016.
Aidha,
Kongamano hii lilitanguliwa na ziara ya ujumbe kutembelea maeneo
mbalimbali ikiwemo mashamba yanayomilikiwa na wakulima na wafugaji
binafsi nchini Tanzania pamoja na kupata fursa za kusikiliza mada
mbalimbali zilizotolewa na wakulima/wafugaji na wakufunzi wa Chuo Kikuu
cha Wageningen kinachohusika na kufanya tafiti za Kilimo na Ufugaji.
Ujumbe
kutoka Tanzania uliongozwa na Mhe.Eng. Mathew Mtigumwe, Katibu Mkuu
anayeshughulikia Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi,
akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Wajumbe wengine ni:
ü Mhe. Yohana Budeba, Katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü Mhe. Irene F.M. Kasyanju, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi,
ü Bw. Twahir Nzallawahe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü Bibi Anuciata Njombe, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Mifugo na Masoko, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
ü Bw. Geoffrey Kirenga, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha kuendeleleza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT),
ü Bibi Jennifer Baarn, Naibu Mtendaji Mkuuwa Kituo cha kuendeleleza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT),
ü Professa Andrew Temu, Mkurugenzi wa Diligent Consulting Ltd na Mwanachama wa Bodi ya SAGCOT,
ü Bibi Jacqueline Mkindi, Mtendaji Mkuu wa Tanzania Horticulture Association (TAHA),
ü Bw. Hussein Sufiani Ally, Mkurugenzi wa AZAM Bakhresa Group,
ü Bibi Mona Mahecha, Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
ü Maafisa wa Ubalozi wa Tanzania Uholanzi Bw. Matiku Kimenya (MC), Bibi Naomi Z. Mpemba (CO) na Bibi Agnes K. Tengia (FS).
Kwa
upande wa Serikali ya Uholanzi, ujumbe uliongozwa na Mhe. Bibi Marjolijn
Sonnema, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kilimo, Wizara ya
Masuala ya Uchumi ya Uholanzi ambaye pia anakaimu kama Naibu Waziri wa
Kilimo. Wengine ni;
ü Mhe. Jaap Fredericks, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania,
ü Bw. Bert Rikken, Afisa anayeshughulikia Masuala ya Kilimo, Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania/Kenya,
ü Bibi Ingrid Korving, Afisa Sera Mwandamizi, Wizara ya Masuala ya Uchumi ya Uholanzi,
ü Bibi Hennie Wellen, Mratibu Wageni wa Kimataifa, Wizara ya Masuala ya Uchumi ya Uholanzi,
ü Bibi Theresia Mcha, Afisa Kilimo, Ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania.
Katika
Kongamano hili, Viongozi wa Ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Uholanzi
walionesha dhamira ya kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kusaini
Barua (Letter of Intent) ya kuanzishwa kwa Kituo cha Kuendeleza Zao la
Viazi nchini Tanzania (Centre for Development of the Potato Industry in
Tanzania- CD PIT). Aidha, Makampuni takriban kumi (10)
yanayojishughulisha na kilimo cha viazi, yalionesha utayari wa kuwa
wanachama kwa kushirikiana na Serikali za nchi hizi mbili katika
uanzishwaji wa Kituo hicho. Tukio hilo lilikamilishwa kwa Wawakilishi wa
Makampuni hayo kuweka saini kwenye Kadi/Bango kuonesha utayari wao.
Kituo
cha CD PIT kinatarajiwa kuanzishwa Mkoani Mbeya ambapo pamoja na kukuza
maendeleo ya sekta binafsi na kutoa ajira, kitatoa mafunzo ya kujenga
uwezo hususan katika uzalishaji na utafutaji masoko, kitaendesha tafiti
mbalimbali za kilimo ikiwemo pia kukuza uhusiano wa kibiashara kati ya
Tanzania na Uholanzi.
Ubalozi
kwa upande wake umeridhishwa na mwitikio mkubwa uliooneshwa na wadau
mbalimbali waliojitokeza kushiriki katika Kongamano hilo. Hii
inadhihirisha kuzidi kuimarika kwa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya
nchi hizi mbili.
Pamoja
na kubadilishana uzoefu, kujifunza na kufahamiana, Kongamano hilo
liliwezesha wadau kupata fursa ya kujadili pia changamoto
wanazokabiliana nazo katika shughuli mbalimbali za biashara na uwekezaji
wanazoziendesha nchini Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
The Hague, Uholanzi, 09 Juni 2017
Mhe. Mathew Mtigumwe, Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo, Mifugo na Uvuvi akisoma hotuba.
Mhe. Irene Kasyanju, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi akisoma hotuba ya ufunguzi.
Mhe. Marjolijn Sonnema, Katibu Mkuu na Kaimu Naibu Waziri wa Kilimo wa Uholanzi akisoma hotuba
Picha ya Pamoja ya Waheshimiwa Mabalozi wa Tanzania na Uhoalnzi na Makatibu Wakuu wa Kilimo na Uvuvi na Mkurugenzi wa TAHA.
Uwekaji saini wa makubaliano (letter of intent) ya kuanzishwa kwa kituo cha kuendeleza zao la viazi Tanzania .
No comments:
Post a Comment