
Meneja Miradi wa Benki ya Absa, Bi. Munira Chambuso akizungumza katika semina iliyoandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, ikihuhusu elimu ya fedha na usimamizi wa uwekezaji, jijini Dar es Salaam jana.
DAR ES SALAAM | Wanawake wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali nchini wamehimizwa kuendelea kujengewa uwezo wa elimu ya fedha ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, kukuza biashara zao na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Absa Tanzania na Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Akizungumza katika mafunzo hayo, Bi. Lukuvi amesema mpango huo ulianza mwaka jana kama sehemu ya ajenda ya uwajibikaji kwa jamii ya benki hiyo, inayolenga kuwawezesha wananchi, hususan wanawake wajasiriamali, kupata maarifa ya kifedha yatakayowasaidia kuwekeza kwa ufanisi na kuimarisha biashara zao.
Amesema mafunzo hayo yamewakutanisha wanawake wamiliki wa biashara kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kuwapa elimu kuhusu usimamizi wa fedha, uwekezaji na mikakati ya kuongeza mapato pamoja na kukuza biashara zao kwa njia endelevu.
“Tunafurahi kuona wanawake wengi wakishiriki mafunzo haya. Tunaamini elimu ya fedha ni nyenzo muhimu katika kuwajengea uwezo wa kufikia mafanikio ya kiuchumi na kuimarisha ustawi wa biashara zao,” amesema Bi. Lukuvi.
Aidha, ameishukuru TPSF kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mafunzo hayo na kubainisha kuwa ushirikiano huo utaendelea ili kuwafikia wanawake wengi zaidi na kuwapa fursa ya kupata elimu ya fedha na uwekezaji.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja wanawake kutoka sekta mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda vidogo, madini, utalii, sekta za ubunifu na ukandarasi, wakiwakilisha wanachama wa TPSF.
Katika mafunzo hayo, wataalamu wa Absa walitoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha ikijumuisha masuala ya bajeti, akiba na uwekezaji kwa lengo la kusaidia wajasiriamali kukuza biashara zao na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kiuchumi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa TPSF, Kinanasi Seif, amesema shirikisho hilo litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupitia programu za mafunzo na elimu zinazolenga kukuza biashara na kuimarisha uchumi wao.
Amesema TPSF imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za kuwawezesha wanawake katika nyanja tofauti za biashara huku ikitambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya sekta binafsi na uchumi wa taifa kwa ujumla.
“Tumefanikiwa kuwaleta pamoja wanawake wajasiriamali kutoka vyama mbalimbali ili wapate mafunzo ya elimu ya fedha na uwekezaji kutoka Benki ya Absa. Tunaamini maarifa haya yatawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kukuza biashara zao,” amesema Seif.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya TPSF na Benki ya Absa ni hatua muhimu katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kujengewa uwezo na kufikia maendeleo endelevu katika shughuli zao za kiuchumi.
Wakati huo huo, wataalamu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walitoa elimu kuhusu utii wa kodi kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za kodi katika kujenga biashara imara na endelevu.
Akizungumza katika semina hiyo, Afisa wa TRA, Zephaniah Usange Jamange, amesema kuwa pamoja na walipakodi kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi, ni muhimu pia kufahamu haki zao wanazostahili kupata kutoka kwa mamlaka hiyo.
Amesema miongoni mwa haki hizo ni usiri wa taarifa za kikodi, ambapo taarifa zote zinazowasilishwa na mlipakodi zinapaswa kubaki siri na haziwezi kutolewa kwa watu wasiohusika. Aidha, walipakodi wote wanapaswa kuhudumiwa kwa usawa bila upendeleo wowote.
“Walipakodi pia wana haki ya kupinga maamuzi yanayotolewa na maafisa wa kodi pale wanapoona hawajaridhika nayo. Maamuzi ya awali si ya mwisho, hivyo kuna fursa ya kukata rufaa kwa kufuata taratibu zilizowekwa,” amesema Jamange.
Kwa upande wa wajibu, TRA imewakumbusha wafanyabiashara kuhakikisha wanajisajili kwa TIN ndani ya siku tano tangu waanze biashara. Pia wafanyabiashara wanaofikia mauzo yanayostahili kwa mujibu wa sheria wanapaswa kutumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD) na kujisajili kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pale inapohitajika.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za pamoja za kukuza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi kwa kuwapatia ujuzi wa usimamizi wa fedha, uwekezaji, utii wa kodi na uendeshaji bora wa biashara, hatua inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa biashara zao na maendeleo ya uchumi wa taifa.

Meneja wa Huduma za Jamii na Matukio wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kutoka kushoto), akizungumza na baadhi ya washiriki, katika semina iliyoandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati ikihusu elimu ya fedha na usimamizi wa uwekezaji, jijini Dar es Salaam jana.

Mkurugenzi wa Wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Kinanasy Seif akizngumza katika semina iliyoandaliwa na Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi hiyo kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, ikihusu elimu ya fedha na usimamizi wa uwekezaji, jijini Dar es Salaam jana.

Meneja Bidhaa Kitengo cha Biashara wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Devroda Kagusa, akizungumza katika semina iliyoandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, Ikihusu elimu ya fedha na usimamizi wa uwekezaji, jijini Dar es Salaam jana.

Ofisa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Zephania Mange, akitoa elimu kuhusu wajibu wa mlipa kodi katika semina iliyoandaliwa na Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kwa wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati, Ikihusu elimu ya fedha na usimamizi wa uwekezaji, jijini Dar es Salaam jana.

Wawakilishi kutoka Benki ya Absa na TPSF, wakipiga picha ya kumbukumbu pamoja na washiriki wa semina hiyo pamoja na wawezeshaji wengine, mara baada ya kumalizika kwa semina hiyo, jijini Dar es Salaam jana.
No comments:
Post a Comment