Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akigonga kengele kuashiria kuorodhoreshwa rasmi kwa Hati Fungani ya Benki ya Azania ijulikanayo kama Bondi Yangu, katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Hafla iliyofanyika katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine aliziasa taasisi zingine kuiga mfano wa Azania Bank wa kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa nchi kwa njia za kidijitali.
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema kuwa mauzo ya hatifungani ya benki ya Azania yamepata mafanikio ya asilimia 210.9, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 63.27 kimepatikana ikilinganishwa na shilingi bilioni 30 zilizopangwa kupatikana.
Aidha, asilimia 70 ya mauzo ya hatifungani imetoka kwa wawekezaji mmoja mmoja yaani Retail Investors na asilimia 30 imetoka kwa Kampuni na Taasisi. Kati ya wawekezaji wote walioshiriki, asilimia 98.4 ni wawekezaji wa ndani na asilimia 1.6 ni wawekezaji wa kigeni.
Hayo yamesemwa leo Januari 24,mwaka 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA. Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko la Hisa la Dar es Saaam.
“Leo sekta ya masoko ya mitaji ina furaha kubwa kwa kuwa Mgeni Rasmi wetu Waziri wa Fedha Dk.Mwigulu Nchemba umewezesha kufikia mafanikio ya hatifungani hii kwa kiwango cha hali ya juu na kwa ufanisi mkubwa, kwani ulikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hatifungani hiyo iliyofanyika Novemba, 4 mwaka 2024.
“Na leo wewe ni Mgeni Rasmi katika hafla ya kuorodhesha hatifungani hii katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE). Tunakushukuru kwa kuwezesha mafanikio haya makubwa kwa kiwango cha hali ya juu."
“Mafanikio haya yana maana kubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya fedha, kwani inaonesha imani waliyonayo wawekezaji kwa benki ya Azania na masoko ya mitaji, ambapo masoko ya mitaji hapa nchini yamekuwa na bidhaa mpya na bunifu zinazokidhi matakwa ya wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,”amesema CPA.Mkam
Ameongeza kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho wa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Saluhu Hassan, akisaidiwa na Waziri wa Fedha kuisimamia Sekta ya Fedha.
Amefafanua baadhi ya mazingira hayo wezeshi ni uwepo wa vivutio vya kuwekeza katika masoko ya mitaji, ambapo katika mwaka wa Fedha 2021/2022, kupitia Sheria ya Fedha uliwezesha kuidhinishwa maombi ya kuweka kivutio cha kuwekeza katika hatifungani za kampuni na taasisi kwa kuondoa kodi ya zuio kwenye faida ya hatifungani za kampuni na taasisi. Hiyo imekuwa mojawapo ya vivutio kwa wawekezaji kwenye hatifungani ya Benki ya Azania.
Pia uwepo wa punguzo la kiwango cha chini chaushiriki katika uwekezaji kwenye hatifungani ya benki ya Azania, kilichoidhinishwa na CMSA kutoka shilingi milioni moja hadi Sh. 500,000). Punguzo hilo limewezesha ushiriki wa wawekezaji wengi, ikiwa ni pamoja na wawekezaji mmoja mmoja(retail investors) ikijumuisha makundi maalum, hususan vijana na wanawake.
Aidha ubunifu wa kuweka malipo ya riba ya hatifungani kwa wawekezaji kufanyika mara nne kwa mwaka badala ya mara mbili, ambapo CMSA imeidhinisha wawekezajikulipwa riba kila baada ya miezi mitatu (3)badala ya miezi sita (6).
“Hatua hii pia imekuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji, kwani inawezesha wawekezaji kuwa na ukwasi na kipato katika muda mfupi, na hivyo kuwezakukidhi mahitaji mengine.Poa elimu ya uwekezaji inayotolewa kwa umma na wadau katika sekta ya fedha kuhusu fursa na faida zinazopatikana katika masoko ya mitaji.”
CPA.Mkama amesema mafanikio ya hatifungani ya benki ya Azania ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa kuwa na njia mbadala za upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza na kukuza biashara; na kugharamia shughuli za maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.
Amefafanua kuwa kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji; na kwenye Waraka wa Matarajio wa benki ya Azania, Fedha kupitia mauzo ya hatifungani hii zitatumika kutekeleza mkakati wa benki ya Azania wa kukuza na kuendeleza biashara, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs) ambazo zinatoa huduma katika sekta za uchumi; na ambazo zinatoa huduma kwa makundi ya wanawake na vijana.
Hivyo kwa mantiki hiyo hatifungani hiyo inawezesha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kuwezesha Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kwa Kampuni Ndogo na za Kati za Ujasiriamali 2023/24 – 2028/29,
Ambapo kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs)ambazo ni kichocheo na kiungo muhimu katika sekta ya kilimo, viwanda na biashara zitafaidika na hivyo kuchagiza maendeleo na ustawi wa sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla hapa nchini.
“Tunawapongeza sana Bodi na Menejimenti ya benki ya Azania kwa kuchukua hatua hii ambayo ni kichocheo muhimukatika maendeleo ya uchumi. Kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Benki ya Azania katika Soko la Hisa leo hii, kunaongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 8.17 na kufikia Shilingi bilioni 837.31, kutoka Shilingi bilioni 774.04.
“Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza Bodi na Uongozi wa benki ya Azania; pamoja na taasisi na wataalamu wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Ninatambua kwamba, kazi hiyo haikuwa ndogo na rahisi lakini mmeweza kufanya kazi yenu vizuri na hivyo kufanikisha hatua hii kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa."
“Natoa mwito kwa Benki zingine za Biashara, Taasisi za Fedha, kampuni binafsi na Mashirika ya Umma kutumia fursa zilizopo katika masoko ya mitaji kama ambavyo Benki ya Azania imetumia fursa ya kupata shilingi bilioni 63.27 kupitia masoko ya mitaji kwa kuuza hatifungani.
“Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)itaendelea kuweka mazingira wezeshi na shirikishi kwa ajili ya kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kupata rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mikakati yenye lengo la kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.”
Mgeni rasmi Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko la Hisa la Dar es Saaam leo. Hafla hiyo imefanyika leo katika Ofisi za DSE, jijini Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA. Nicodemus Mkama akizungumza mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko la Hisa la Dar es Saaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Esther Mang'enya akizungumza mbele ya wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa toleo la kwanza la hatifungani ya Benki ya Azania (Azania Bond Yangu) katika Soko la Hisa la Dar es Saaam leo.
No comments:
Post a Comment