JAMHURI
ya Muungano wa Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu ya kupiga kura
ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine huku
ikisisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula (Mb) ametoa ufafanuzi huo wakati akifanya mahojiano na mojawapo
ya vyombo vya Habari kutoka China na kuongeza kuwa Sera ya Tanzania
kuhusu namna ya kutatua changamoto za migogoro inapojitokeza ni kwa
kutumia njia za kidiplomasia.
Balozi
Mulamula amesisitiza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania haijabadilika tangu uhuru na kuongeza kuwa Tanzania inaamini
hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika hasa panapokuwepo na utashi na
nia njema ya kumaliza mgogoro na kwamba njia ya kidiplomasia ndio
chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro kati
ya Urusi na Ukraine.
“Sisi
msimamo wetu na Sera yetu na msingi wetu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje
ni kutofungamana na pande zozote, hivyo kutokupiga kura ni kuonesha
msimamo wa Tanzania,” amesema Balozi Mulamula
Alipoulizwa
endapo Tanzania imeathirika na vita inayoendelea kati ya Urusi na
Ukraine, Balozi Mulamula amesema madhara yanayotokana na vita hiyo
yanajionesha dhahiri huku akitaja baadhi ya madhara hayo kwa baadhi ya
wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Urusi kukatisha masomo
yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika pamoja na ongezeko la
bei ya petroli na gesi duniani.
Kutokana
na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi Tanzania ililazimika
kuwaondoa raia wake nchini Ukraine hususan wanafunzi takribani 300
waliokuwa wakisomea masuala ya udaktari nchini humo.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula akiwa katika mahojiano na moja ya vyombo vya Habari vya China.
Mahojiano hayo yalifanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula akihojiwa na mmoja wa waandishi wa habari kutoka China.
No comments:
Post a Comment