CHAMA Cha Mapinduzi(CCM)
Zanzibar, kimewaonya baadhi ya Wanasiasa kuacha tabia za kutafuta ‘Kiki’
za kisiasa kwa kuwachafua viongozi wa Serikali na Chama badala ya
kusifia maendeleo yaliyofikiwa nchini.
Onyo hilo limetolewa na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, katika
kongamano la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja iliyoandaliwa na UWT
iliyofanyika Amani Mkoa Zanzibar.
Dk.Mabodi ambaye pia ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM, aliwashauri wanasiasa hao kama wameshindwa kazi
za kisiasa bora watafute kazi zingine za kujiingizia kipato kwani
wananchi hawahitaji siasa za kuuza maneno na porojo bali wanahitaji
maendeleo endelevu.
Dk.Mabodi, alisema genge hilo la wanasiasa
limekuwa likitangatanga kila kona wakibeza na kupotosha juhudi na hatua
kubwa zinazofanywa na Serikali zote mbili.
Naibu Katibu Mkuu
huyo Dk.Mabodi, aliweka wazi kwamba ni aibu na fedheha kubwa kwa kundi
hilo kukosa uzalendo wa hata kuthamini maendeleo yanayofanywa na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo wao ni Sehemu ya Serikali hiyo.
Alisema
Chama Cha Mapinduzi kwa awamu mbali mbali kabla na baada ya mfumo wa
vyama vingi nchini kimetatua kero na changamoto za wananchi bila kujali
tofauti za kisiasa.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi, alisema Dunia
nzima inatambua kwamba CCM ni Chama Kiongozi na mwalimu wa siasa
zilizokuwa hai na zinazojali utu na kutimiza mahitaji ya Wananchi.
Kiongozi
huyo aliwambia wanasiasa hao wanaotoka katika moja ya Chama cha
Upinzania Zanzibar kuwa waache mtindo huo wa siasa chafu bali wajipange
kushindana kwa Sera za maendeleo yaani waonyeshe mambo waliyoyatekeleza
kwa wananchi kama inavyofanya CCM.
“ Tushindane kwa Sera na sio
maneno na vituo, CCM ina mengi ya kujivunia kwani tumefanya na
tunaendelea kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 katika
sekta za Afya,Maji,Elimu na miundombinu ya barabara,anga,nchi kavu,
baharini na kila sehemu tunahakikisha wananchi tunawafikia.
Tunayo
mengi ya kujivunia na kutamba sasa na nyie wenzetu semeni yenu
mliyowafanyia wananchi ?,,.sio mnasubiri sisi tufanye eti nyie muanze
kupotosha na kukosoa twambieni Unguja na Pemba wapi mmejenga
shule,hospitali,visima vya maji safi na salama hata msaada mdogo tu wa
kijamii kwani ruzuku mnapata.”, alihoji Dk.Mabodi.
Dk.Mabodi
aliweka wazi kwamba kwa mwenendo huo wanaokwenda nao wanasiasa hao ni
kielelezo tosha cha kuonyesha Dunia kwamba Zanzibar kwa sasa hakuna
Chama cha upinzania chenye maono,hoja na Sera imara za kushindana na
CCM.
“ CCM tunaendelea kutamba na kusonga mbele kimaendeleo kwa
kasi ya 4G huku wenzetu wakihaha na kurusha mawe kwenye kiza, huku sisi
tukitekeleza kwa wakati ahadi tulizotoa kwa wananchi kupitia uchaguzi
mkuu uliopita.
Dk.Mabodi, aliwasihi wananchi wa makundi yote
kuendelea kumtia moyo na kumuunga mkono Rais huyo mwenye dhamira ya
kweli ya kuleta maendeleo ya nchi.
Alisisitiza Wanaccm kuendelea kudumisha umoja na mshikamano,upendo na kulinda maslahi ya Chama kwa vitendo.
Alisema uongozi shirikishi ni moja kati ya sifa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kitaaluma.
Alieleza kuwa kutokana na uongozi wake huo ndio maana amekuwa akikumbukwa na jamii.
Hata hivyo alisema mageuzi ambayo anayafanya katika diplomasia ni kwa maslahi ya watanzania.
Aliwakumbusha
Wanaccm hao kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi katika zoezi
la sensa ya Watu na Maakazi ili Serikali ifanikishe mipango ya maendeleo
inayoendana na mahitaji ya wananchi.
Pamoja na hayo aliwataka
Wana CCM kujipanga vizuri juu ya uchaguzi wa Chama unaofanyika mwaka huu
kwa kuhakikisha wanapatikana viongozi imara,waadilifu na wachapakazi.
Wakati
huo huo Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi,
amesema Rais Samia amekuwa na ushirikiano mkubwa na Zanzibar katika
shughuli mbali mbali za maendeleo.
Rais Mwinyi Aliyaeleza hayo alipotoa salamu zake za pongezi kwa kutimiza mwaka mmoja kwa njia ya simu katika mkutano huo.
Alisema
tangu kuwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania rais Samia amekuwa
akiisaidia Sana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupeleka mbele
Mipango ya kimaendeleo.
"Niseme tu kwamba nafarajika sana na uwepo wake na nitowe shukrani za dhati katika ushirikiano wake kwa SMZ", alisema.
Dkt. Mwinyi alisema misaada mengi ambayo yanaonekana kwa sasa yamepatikana kupitia kwake.
Hivyo aliwataka wanaccm pamoja na wananchi wote kwa ujumla kumuunga mkono rais Samia katika kutekeleza majukumu yake.
Nae
Makamu Mwenyekiti wa UWT Thuwaiba Edington Kisasi amesema wana kila
sababu ya kumpongeza kutokana na mambo mengi na makubwa aliyoyafanya kwa
kipindi kifupi cha uongozi wake.
Aidha alisema kuendelea
kudumisha Amani na utulivu no sifa kubwa ambayo rais Samia na
wataendelea kuwa nae bega kwa bega katika kufanikisha Mipango ya
maendeleo kwa nchi yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa mjini kichama Talib Ali Talib, alisema Safari ya mwanamke kuwa
kiongozi ilianza mwaka 1964 na aliekuwa rais wa Kwanza Zanzibar marehemu
Abeid Amani Karume.
Alisema Karume Mara tu baada ya nchi kupata
uhuru kazi aliyoifanya ni kuwapa wanawake fursa za kuwa viongozi katika
serikali yake.
Akitoa mada kuhusu mchango wa rais Samia katika
kuimarisha maendeleo ya uchumi na jamii Tanzania Bara na Zanzibar kada
wa CCM dkt. Sada Mkuya amefanikiwa kurejesha mahusiano mazuri ya
kimataifa ambayo yalikuwa yametetereka.
Mkuya ambae ni Waziri wa
Nchi, Afisi ya Rais fedha na Mipango alisema kupitia hatua hiyo
imepelekea kuvutia wawekezaji, kukuza biashara,kuimarisha muungano,
usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa fursa za uchumi wa Zanzibar na
kuwataka Wanaccm kutumia fursa kwa kuyafanyia kazi mazingira mazuri
aliyoyaweka.
No comments:
Post a Comment