SERIKALI
ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 19 kwa ajili ya
ujenzi wa shule 56 za michezo hapa nchini.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan
akipokea Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA) U23 kutoka kwa Nahodha msaidizi wa Timu ya Taifa ya Vijana U23,
Reliant Lusajo tarehe 22 Agosti, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA IKULU).
Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameyasema
hayo Machi 12, 2022 katika mjadala wa Kitaifa ulioangazia Mafanikio
katika Sekta ya Michezo Kuelekea Mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.
"Serikali
ya Awamu ya Sita imejipanga kujenga shule 56 za michezo, hivyo kwa
ushirikiano wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Wizara ya
TAMISEMI (Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Wizara ya
Elimu (Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia) tayari imeshabainisha
shule hizo na Serikali katika bajeti ijayo itatoa shilingi Bilioni 19
kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo,"amesema Mheshimiwa Mchengerwa.
Mjadala
huo wa saa mbili na nusu umeratibiwa na Watch Tanzania kupitia mtandao
wa Zoom huku ukirushwa mubashara kupitia runinga mtandao mbalimbali kwa
udhamini wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Mtandao wa
Simu wa Airtel Tanzania.
Pia
Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema kuwa, timu ya Taifa ya Wanawake
chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls kushiriki michuano ya kufuzu
Kombe la Dunia ni moja wapo ya mafanikio makubwa ya kujivunia kupitia
uongozi wa Rais Samia huku akitambua msingi mzuri uliowekwa na Hayati
Baba wa Taifa katika kuhamasisha michezo nchini.
"Hatuwezi
kutaja mafanikio ya Sekta ya Michezo nchini bila kumtaja Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwani yeye alisisitiza sana
katika eneo hili la michezo hasa katika kuibua vipaji na kuongeza ajira
kwa Watanzania, eneo hili la Sekta ya Michezo kwa kipindi kirefu sana
Watanzania walitamani tupige hatua kama yalivyo mataifa mengine.
"Hivyo,
Serikali hii ya Mheshimiwa Rais Samia imejipanga kuhakikisha inaboresha
sekta hii ikiwemo ujenzi wa viwanja , vituo vya michezo (academy),
kuboresha sera za michezo na ununuzi wa vifaa vya kimichezo na vitu
vingine vyote vinavyotakiwa katika kuboresa michezo nchini.
"Katika
bajeti hii ya mwaka 2021/2022 Serikali imejipanga kujenga viwanja vya
burudani na michezo katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Geita na
takribani shilingi bilioni 10 za Kitanzania na zaidi zitatumika katika
ujenzi huo,"amefafanua Mheshimiwa Mchengerwa.
Amesema, kwa upande wa kiwanja cha Dodoma kitajengwa na kitakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji zaidi ya laki moja waliokaa.
"Serikali
ya Awamu ya Sita tayari imeshajipanga kufanya ujenzi mpya wa kiwanja
cha kisasa kabisa huko makao makuu ya nchi, Dodoma ambapo kiwanja
kitabeba watu zaidi ya 105,000,"amesema Mheshimiwa Mchengerwa.
Wakati
huo huo, Mheshimiwa Waziri amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais Samia imeendelea kutoa nafuu katika ujenzi wa viwanja vya
michezo nchini.
Pia
amesema kuwa, bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali imeondoa Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) katika uagizaji wa nyasi bandia kwa ajili ya
viwanja vya michezo nchini.
Dkt.Kigwangalla
Kwa
upande wake Mbunge wa Nzega Vijijini, Mheshimiwa Dkt.Hamisi Kigwangalla
amesema, mafanikio makubwa yanayoonekana kwa sasa katika Sekta ya
Michezo nchini yanatokana na namna ambavyo Mheshimiwa Rais Samia amekuwa
mdau mkubwa katika sekta hiyo.
"Rais
Samia amepitisha bajeti moja ndani ya Bunge, lakini katika mapendekezo
ya Serikali tumeona nia yake ya kuleta mabadiliko na mapinduzi katika
Sekta ya Michezo.Na tumemshuhudia mara kadhaa akifanya vikao na kuwatia
nguvu vijana wetu wa timu ya wanawake na walemavu. Hii inawapa nguvu
kupambana zaidi,"amesema Mheshimiwa Dkt.Kigwangalla.
Kidao Wilfred
Wakati
huo huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Bw. Kidao Wilfred amesema kuwa, kuna neema kubwa ambayo imeanza
kuonekana katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania kutokana na mazingira mazuri
ya uwekezaji ambayo yamewekwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
"Ligi
yetu (Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara) kwa mara ya kwanza imeanza kuvutia
wachezaji wengi wa kigeni. Wachezaji kutoka Zimbabwe, Angola, Uganda,
Nigeria, Ghana, Kenya, Rwanda, Burundi wapo katika Ligi yetu ya NBC,
huko nyuma wachezaji wetu walikuwa wanatoka kutafuta malisho bora, wao
wamegeuza Tanzania kuwa sehemu ya malisho, ni kwa sababu ya uwekezaji
uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
"Huko
nyuma vijana walikuwa wanacheza mpira kama wa ridhaa, sehemu kubwa ya
wachezaji wanawake sasa wanalipwa kama ajira rasmi, jambo ambalo ni
kubwa kwa mara ya kwanza watoto wa kike wanaishi kwa kutegemea ajira ya
mpira.
"Jambo
hili halijawahi kutokea kwa siku za nyuma, kwetu sisi ni mafanikio
makubwa mno, pia ndani ya mwaka mmoja ligi kuu hususani ya NBC imekuwa
na mafanikio makubwa, kwani wadau wameanza kuwekeza kwenye ligi
hiyo,"amesema Bw.Kidao.
Amefafanua
kuwa, huko nyuma mapato ya Ligi Kuu kwa wastani yalikuwa shilingi
bilioni 7 ndani ya mwaka mmoja, lakini anasema kuwa mapato ya ligi
yameongezeka hadi kufikia asilimia 200 ikiwa ni zaidi ya shilingi
bilioni 14.
Somoe Ng'itu
Akizungumza
katika mjadala huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA), Bi.Somoe Ng'itu amesema kuwa, ndani ya mwaka mmoja wa
uongozi wa Rais Samia madarakani, kumekuwa na ushindani mkubwa katika
mpira huo.
"Ushindani
umeongezeka sana, mpaka kwa makocha wa kiume kuwania kuomba nafasi ya
kuzifundisha hizi timu za wanawake. Hii inamaanisha safari tuliyokuwa
nayo kipindi cha nyuma na hii tuliyo nayo kwa sasa ni tofauti.
"Tumefikia
kiwango cha juu, kila mmoja anathamini huku kwa sababu kuna jambo, kwa
sababu ya hamasa iliyotolewa na Kiongozi Mkuu kwamba mpira huu wa
wanawake si tena wa watu wahuni, waliokosa kazi, umekuwa rasmi si tena
wa kujitolea kama miaka ya nyuma ambavyo ilikuwa inaonekana,"amesema
Bi.Somoe.
Aidha,
amesema kuwa, katika kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia ndoto ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu ya
kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa wamekuwa na ligi mbalimbali.
"Miaka
ya nyuma haikuwepo, kwa mara ya kwanza mwaka jana mwezi wa sita tangu
Rais aingie madarakani tulipata timu 24 kati ya timu 26 kutoka mikoa
yote ya Tanzania Bara ambazo zimeshiriki ligi daraja la kwanza kwetu,
ilikuwa ni faraja kubwa sana.Soka letu limekuwa na thamani kubwa kwa
sababu tumepewa thamani ile ambayo wanaume walikuwa wanapata,"amesema
Somoe.
No comments:
Post a Comment