RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi amesema kuwa kwa vile maji ni uhai lazima Serikali iongeze kasi
ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi kwa kuendeleza na kuanzisha
miradi mipya ya maji safi na salama.
Rais
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la
msingi la Mradi mkubwa wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Maji Safi
na Salama, huko Kwarara Kidutani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini
Magharibi ikiwa pia ni kipindi ambacho Dunia inaadhimisha Wiki ya Maji.
Katika
hotuba yake Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, utekelezaji wa mradi huo
uliowekwa jiwe la msingi ni katika kuyafikia malengo hayo huku
akisisitiza kwamba hatua hiyo ni ndani ya miaka miwili tu na hana shaka
ndani ya miaka mitano ijayo tatizo la maji litamalizika.
Amesema
kuwa, takwimu zinaonesha kwamba hali ya upatikanaji wa maji nchini hivi
sasa ni wastani wa asilimia 55 hadi kufikia mwaka huu wa 2022 na
kueleza kwamba kukamilika kwa mradi huo asilimia zitaongezeka na kufikia
76 huku juhudi zaidi zikichukuliwa katika kuhakikisha wananchi wote
wanapata maji safi na salama.
Rais
Dkt. Mwinyi ametoa wito wa wizara husika pamoja na Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA) kufanya kazi na kuwa wepesi wa kutatua changamoto za
huduma hiyo zinazowakumba wananchi.
Amesisitiza
kwamba, jukumu la ulinzi la miundombinu ya maji ni la watu wote na
kueleza kwamba wananchi wana jukumu la kuilinda miundombinu hiyo na
wasiwaruhusu watu wachache kuiharibu.
Aidha,
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, upatikanaji wa huduma za maji safi na
salama katika maeneo yote ya Unguja na Pemba ni miongoni mwa vipaumbele
vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hivyo,
ameongeza kuwa jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika
upatikanaji wa huduma za maji safi na salama ni utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020-2025, mipango mikuu ya maendeleo na
ahadi zilizotolewa katika kipindi cha kampeni.
"Leo
tarehe 21, Machi 2022 tupo hapa Kwarara Mkoa wa Mjini Magharibi,
kufungua ukurasa mwingine wa maendeleo ya sekta ya maji kwa kuweka jiwe
la msingi la mradi mkubwa wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji
katika maeneo mbalimbali ambapo huduma hii haipatikani kabisa,"amesema
Dkt.Mwinyi.
Rais
Dkt.Mwinyi amesema kuwa, mradi huo utanufaisha zaidi maeneo ambayo kwa
sasa yanaonekana kukua kwa haraka kutokana na wananchi wengi kujenga
makazi yao mapya na kuhamia maeneo hayo ya Wilaya ya Magharibi A na
Magharibi B pamoja na maeneo ya mpakani mwa Mkoa wa Mjini na Magharibi
na Mkoa wa Kusini Unguja yakiwemo Tunguu, Jumbi na Ubago.
Amesema
kuwa, maadhinisho hayo ambayo yanakwenda na ujumbe wa kauli mbiu
isemayo Rasilimali za Maji chini ya Ardhi ni Nyenzo ya Kukabiliana na
Mabadiliko ya tabianchi na kusisitiza kuwa na mipango mbadala na
mikakati itakayowezesha kukabiliana na changamoto za aina tabianchi.
Ameeleza
kwamba hali ya tabianchi ndio inayopelekea uwezo wa uzalishaji wa maji
katika vyanzo vilivyopo kupungua kama inavyoshuhudiwa katika vyanzo vya
Mwanyanya na Mtopepo.
Amesisitiza
kwamba katika hali kama hiyo ni lazima wananchi waendelee kupewa elimu
ya kuvilinda na kuvitunza vyanzo vya maji kwa kuepuka ujenzi karibu na
vyanzo hivyo na kuacha tabia ya ukataji wa miti na misitu pale vilipo.
Rais
Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuona haja ya kulipia maji ili
huduma za maji ziwe endelevu na kuwataka ZAWA kuendelea kuweka mita za
maji pamoja na kuhakikisha wanaotakiwa kulipa maji ni wale wanaoipata
huduma hiyo na siyo kwa kila mwenye mfereji (bomba) ndani hata ikiwa
maji hapati.
Nae
Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaib Hassan Kaduara ametoa pongezi
kwa Rais Dkt. Mwinyi hukua akiahidi kwamba Wizara yake itaendelea
kusimamia miradi yote ya maji ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa alieleza jinsi
wananchi wa Mkoa huo pamoja na Mikoa jirani watakavyofaidika na mradi
huo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ZAWA, Meja Jenerali Issa Nassor alieleza jinsi
mradi huo pamoja na miradi mengine ya maji itakavyotekelezwa na kuwataka
wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya miradi yote ya maji.
Mapema
Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Dkt. Salha Mohammed alisema kuwa mradi huo
unatekelezwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Benki ya Exim pamoja na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema
kuwa,mradi wote hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Dola za
Marekani Milioni 92.18 ambazo zimetolewa na Serikali ya India kupitia
Benki ya Exim ya India kwa njia ya mkopo wa masharti nafuu kwa
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliongeza
kuwa hadi hivi sasa wastani wa shilingi 702,626,900 zimetolewa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni sehemu ya mchango wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya gharama za malipo ya fidia kwa
mali na mazao ya wananchi yaliyoathirika na ujenzi wa mradi huo pamoja
na gharama za uendeshaji wa mradi.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali
Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum na Mwakilishi wa Kampuni ya L&T
Construction, Bw.Hari Prakash, (kushoto kwa Rais) baada ya kumalizika
kwa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Uhuishaji na
Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji wa Maji Zanzibar, mradi huo wa ujenzi
wa matangi ya maji katika eneo la Kwarara Kidutani Wilaya ya Magharibi
“B” Unguja.(Picha na Ikulu).
Sambamba
na hayo amesema kuwa, mradi huo umegawanyika sehemu tatu kwa
utekelezaji wake ambapo sehemu ya kwanza itatekelezwa na Kampuni ya
Megha Engineering Limited kutoka India na sehemu ya pili itatekelezwa na
Kampuni ya Afcons and Vijeta-VJ ya India na sehemu ya tatu itatekelezwa
na Kampuni ya Larsen& Toubro (L&T) Limited nayo ya India.
Nae
Mwakilishi wa jimbo hilo Ali Ameir Mrembo kwa niaba ya wananchi wa
jimbo hilo alitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dkt. Mwinyi kwa
kuwapelekea huduma hiyo muhimu katika kipindi kifupi alichokaa
madarakani.
No comments:
Post a Comment